ZANZIBAR HEROES YAWASHUSHIA KIPIGO WANYARWANDA KOMBE LA CHALENJI
Wawakilishi wa Zanzibar katika michuano ya CECAFA Senior Challenge inayoendelea nchini Kenya, Zanzibar Heroes wameanza michuano hiyo kwa kasi baada ya kuichapa timu ya taifa ya Rwanda (Amavubi) kwa mabao 3-1.
Wakitupa karata yao ya kwanza, Heroes walijipatia bao la kuongoza mnamo dakika ya 34 kupitia kwa Mudathir Yahya Abas aliyefunga kwa kichwa baada ya kupokea krosi safi kutoka kwa Mwinyi Haji.
Bao hilo lilidumu hadi mapumziko na kuwafanya mashujaa hao wa visiwa vya karafuu kwenda kifua mbele.
Rwanda walikuja juu katika dakika za mwanzo za kipindi cha pili na kufanikiwa kuandika bao la kusawazisha katika dakika ya 52 lililofungwa na Muhadjiri Hakizimana ambaye ni mdogo wa damu wa kiungo wa Simba Haruna Niyonzima.
Wakati Amavubi wakishambulia kwa kasi kwa nia ya kuongeza bao la pili, Vijana wa kocha Hemed Moroco walifanya shambulizi la kushtukiza katika dakika ya 72 na yule kijana kutoka Manungu, Turiani Morogoro anayezitoa udenda timu kubwa nchini Tanzania, Mohammed Issa kufanikiwa kuandika bao la pili kwa shuti zuri lililombabatiza beki wa Rwanda na kutinga wavuni.
Baada ya bao hilo, Zanzibar Heroes waliituliza presha ya Wanyarwanda ambao walikua wakijitahidi kwa kila hali kutaka kusawazisha, lakini ngome ya Zanzibar iliendelea kuwa imara.
Wakishuhudiwa na ndugu zao Kilimanjaro Stars kutoka Tanzania Bara, Heroes waliamsha shangwe tena baada ya kushindilia kambani bao la tatu lililofungwa na Kassim Khamis katika dakika ya 86 ya mchezo.
Mpaka mchezo unamalizika, Zanzibar 3-1 Rwanda.
Zanzibar Heroes watarudi tena dimbani siku ya Alhamisi kuvaana na ndugu zao, Kilimanjaro Stars.
Masengwa blog Ipo Play Store…Download HAPA ,Uwe unapata habari zote kwa urahisi zaidi
No comments: