OMOG AMFUNIKA LWANDAMINA

Wakati kundi kubwa la mashabiki wa Simba likionekana kutokuwa na imani na kocha wao Joseph Omog, uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini raia huyo wa Cameroon ndiye kocha bora nchini kwa mwaka 2017.

Omog aliyeanza kuinoa Simba Julai 2016, ndiye kocha aliyefanya vizuri zaidi na kupata mafanikio makubwa kulinganisha na makocha wengine 15 wanaofundisha timu zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara.

Ndani ya mwaka huu, Omog ameiongoza Simba kutwaa ubingwa wa mashindano ya Azam Sports Federation Cup na kuiwezesha timu hiyo kukata tiketi ya kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika mwakani.

Hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa timu hiyo kushiriki mashindano ya kimataifa baada ya miaka minne.

Mbali na kuipa Simba ubingwa wa Azam Sports Federation Cup, mwaka huu kocha huyo ameiongoza timu hiyo kutwaa Ngao ya Jamii na kumaliza nafasi ya pili katika mashindano mawili tofauti ambayo ni Ligi Kuu msimu uliopita na Kombe la Mapinduzi.

Ukiondoa kigezo cha mataji ambacho Omog amewapiku wapinzani wake wakuu George Lwandamina wa Yanga aliyenyakua ubingwa wa Ligi Kuu msimu uliopita na mwenzake wa Azam FC, Aristica Cioaba aliyetwaa Kombe la Mapinduzi, kocha huyo wa Simba anabebwa na takwimu za matokeo ya timu yake ambazo zimewa a cha mbali makocha wengine.

Ndani ya mwaka huu, Omog ameiongoza Simba kucheza michezo 35 ya mashindano tofauti na timu hiyo ilivuna pointi 74, ikishinda michezo 21, kutoka sare moja, kufungwa mechi tatu huku ikifunga mabao 56 na kufungwa 20.

Pointi hizo 74 katika michezo 35 zinaifanya Simba kuwa na wastani wa pointi 2.11 kwa kila mchezo, idadi ambayo ni kubwa kulinganisha na timu zote zilizopo Ligi Kuu.

Mwaka huu, Simba imeshiriki Ligi Kuu, Kombe la Azam Sports Federation na Kombe la Mapinduzi.

Takwimu zinaonyesha kocha wa Azam FC, Aristica Cioaba anamfuatia Omog kwa kufanya vizuri mwaka huu ambapo katika mechi 34 alizoiongoza kwenye Ligi Kuu, Kombe la Mapinduzi, Azam Sports Federation na Kombe la Shirikisho Afrika, amekusanya pointi 70 ambazo ni wastani wa pointi 2.06 kwa kila mechi.

Azam ikiwa chini ya Cioaba, mwaka huu imeibuka na ushindi mara 20, kutoka sare 10 na kupoteza mechi nne. Ikifunga mabao 36 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 14.

Anayeshika nafasi ya tatu kufanya vizuri ni Lwandamina ambaye licha ya timu yake kuvuna idadi kubwa ya pointi kuliko Simba na Azam, anaangushwa na takwimu za timu yake kucheza idadi kubwa ya mechi kulinganisha na wenzake Cioaba na Omog.

Lwandamina aliyeipa Yanga ubingwa wa Ligi Kuu msimu uliopita, ameiongoza timu yake kupata pointi 75 katika michezo 38 ambazo ni wastani wa pointi 1.97 kwa kila mechi, akiibuka na ushindi katika mechi 21 kutoka sare 10, kupoteza michezo mitano huku ikifunga mabao 65 na kufungwa 23.

Hans Pluijm wa Singida United, anashika nafasi ya nne kutokana na kuiwezesha timu yake kupata pointi 20 katika michezo 11 ambazo ni sawa na wastani wa pointi 1.82 kwa kila mchezo.

Mecky Maxime wa Kagera Sugar yupo nafasi ya tano akipata pointi 40 ambazo ni sawa na wastani wa 1.54 kwa mechi.

“Tunaheshimu kila kinachofanywa na kocha wetu ndio maana uongozi una imani na Joseph Omog,” alisema Ofisa Habari Simba Haji Manara.

Makocha na wachambuzi wa soka, Kennedy Mwaisabula na Joseph Kanakamfumu walisema takwimu za Omog zinawasuta mashabiki na wanachama wa Simba ambao hawamkubali.

“Kuna shida kubwa ya ufahamu wa soka kwa mashabiki wa soka ndio maana unaona hili linatokea. Binafsi sijaona kocha bora kwenye Ligi Kuu kama Omog,” alisema Mwaisabula.

“Simba ina amini kikosi chao kinatakiwa kupata ushindi kila mechi, lakini kiufundi ina wachezaji wachache ambao wako kwenye ubora,”alisema Kanakamfumu.

Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 753 336 000 au +255 625 917 902

Masengwa blog Ipo Play Store…Download HAPA ,Uwe unapata habari zote kwa urahisi zaidi
 Bofya Hapa

No comments:

Powered by Blogger.