HAYA NDIO MATOKEO YA YANGA DHIDI YA SINGIDA UNITED

TIMU ya Singida United imeshindwa kutumia vizuri Uwanja wa nyumbani, Namfua mjini hapa baada ya kulazimishwa sare ya 0-0 na mabingwa watetezi, Yanga SC katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara. 

Sare hiyo ya pili mfululizo na Jumamosi iliyopita kutoka 1-1 na mahasimu wa jadi, Simba inaifanya Yanga ifikishe pointi 17 baada ya kucheza mechi tisa, wakati Singida inafikisha pointi 14 baada ya mechi tisa pia. 

Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Emmanuel Mwandembwa wa Arusha, aliyesaidiwa na Joseph Pombe wa Shinyanga na Khalfan Sika wa Pwani, dakika 45 za kipindi cha kwanza timu zote zilishambuliana kwa zamu. 

Yanga ndiyo waliokuwa wa kwanza kulijaribu lango baada ya dakika ya 12, Ibrahim Ajib kupiga vizuri shuti la mpira wa adhabu lililokwenda nje kidogo, kufuatia winga Geoffrey Mwashiuya kuchezewa rafu nje kidogo ya boksi. 

Mwashiuya akaikosesha Yanga bao la wazi dakika ya 14 baada ya kukutana na mpira uliookolewa na mlinda mlango Peter Manyika, lakini akapiga fyongo ukaenda nje kabisa, huku lango la Singida United likiwa wazi kufuatia kipa huyo kutoka kwenda kuokoa awali na kuchelewa kurudi. 

Singida United wakajibu kwa mashambulizi mawili mfululizo, dakika ya 16 shuti la kiungo Kenny Ally kutoka nje kidogo ya boksi likienda nje kidogo ya lango la Yanga na dakika ya 20 mshambuliaji Mzimbabwe, Tafadzwa Kutinyu akapiga juu ya lango akiwa kwenye nafasi nzuri. 

Beki Salum Kipaga akafanya kazi nzuri dakika ya 24 kwa kuokoa mpira wa adhabu uliopigwa na Ajib kutoka nje kidogo ya boksi ambao uliwapita wachezaji wa Singida United waliokuwa wameweka ukuta. 

Singida United wakacharuka dakika tano za kuelekea mwisho wa kipindi cha kwanza kwa mashambulizi mfululizo kwenye lango la Yanga – lakini kali zaidi ni la dakika ya 43 Tafadzwa Kutinyu alipopokea pasi nzuri ya Danny Usengimana na kupiga shuti kali lililopanguliwa na kipa Youthe Rostand. 

Kipindi cha pili, Singida United walirudi kwa kasi zaidi na kuanza kulishambulia la Yanga mfululizo na dakika ya 54 walikaribia kupata bao baada ya kona iliyopigwa na kiungo Kigi Makassy kuunganishwa kwa kichwa na Salum Kipaga na kupita nje pembeni na kupenya kwenye nyavu iliyochanika kuingia ndani, lakini refa akawa makini na kuamua sahihi. 

Mshambuliaji Mzambia wa Yanga, Obrey Chirwa akaonyeshwa kadi ya njano dakika ya 65 akituhumiwa kujiangusha kwenye boksi la Singida wakati anadhibitiwa na beki wa timu hiyo, lakini akatoka nje anachechemea kwenda kutibiwa kabla ya kurejea kuendelea na mchezo. 

Singida wakapata pigo dakika ya 69, baada ya mchezaji wao, Salum Kipaga kuumia na kushindwa kuendelea na mchezo, nafasi yake ikichukuliwa na Rolland Msonjo. 

Na timu hizo zikaendelea kushambuliana kwa zamu hadi filimbi ya mwisho. 

Kikosi cha Singida United kilikuwa; Peter Manyika, Michael Rusheshangonga, Shafik Batambuze, Salum Kipaga/Rolland Msonjo dk69, Juma Kennedy, Mudathir Yahya, Deus Kaseke/Michelle Katsavairo dk63, Kenny Ally, Danny Usengimana/Atupele Green dk81, Tafadzwa Kutinyu na Kiggi Makassy. 

Yanga SC; Youthe Rostand, Hassan Kessy, Andrew Vincent, Gardiel Michael, Kelvin Yondan, Pato Ngonyani/Raphael Daudi dk88, Pius Buswita, Papy Tshishimbi, Obrey Chirwa, Ibrahim Ajib na Geoffrey Mwashiuya/Emmanuel Martin dk59. 

Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 753 336 000 au +255 625 917 902

Masengwa blog Ipo Play Store…Download HAPA ,Uwe unapata habari zote kwa urahisi zaidi
 Bofya Hapa

No comments:

Powered by Blogger.