WAZIRI MKUU WA ETHIOPIA KUFANYA ZIARA NCHINI KWA SIKU MBILI



Waziri Mkuu wa Ethiopia, Hailemariam Dessalegn anatarajia kufanya ziara ya kitaifa ya siku mbili nchini kesho, Machi 31 na Aprili 1.

Ziara hiyo ni mwaliko wa Rais John Magufuli kwa Dessalegn kufuatia mazungumzo waliyoyafanya huko Addis Ababa, Ethiopia baada ya mkutano wa wakuu wa nchi wa Umoja wa Afrika (AU).


Akizungumzia ziara hiyo leo, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Dk Susan Kolimba amesema baada ya kuwasili nchini, Waziri Mkuu huyo atakuwa na mazungumzo ya faragha na Rais Magufuli na baadaye ujumbe wa Ethiopia na Tanzania watakaa pamoja na kuzungumza.


 Dk Kolimba amesema viongozi hao watashuhudia utiaji saini mikataba mitatu katika maeneo ya biashara, uwekezaji, utalii na diplomasia.


"Madhumuni ya ziara hiyo ni kukuza uhusiano uliopo baina ya Tanzania na Ethiopia pamoja na kujadili fursa za ushirikiano katika maeneo mbalimbali ikiwemo uwekezaji na biashara," amesema Dk Kolimba.


Siku itakayofuata, Aprili Mosi, Dessalegn atafanya ziara katika bandari ya Dar es Salaam na baadaye siku hiyo ataondoka kurejea Ethiopia.


Dk Kolimba amesema Ethiopia imeonyesha nia ya kufungua ubalozi wake hapa nchini. Kwa sasa Ethiopia inawakilishwa nchini na Balozi wake aliyepo Nairobi, Kenya.


Dessalegn alitembelea Tanzania mwaka 2015 na kushiriki uzinduzi wa kiwanda cha kutengeneza dawa za kuulia viluwiluwi vya mbu wanaoeneza Malaria. Pia, alishiriki sherehe za kuapishwa kwa Rais Magufuli zilizofanyika Novemba 2015.


Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 753 336 000 au +255 625 917 902

Masengwa blog Ipo Play Store…Download HAPA ,Uwe unapata habari zote kwa urahisi zaidi
 Bofya Hapa
Powered by Blogger.