CHANZO NA ATHARI ZA MAGONJWA YA AKILI KATIKA JAMII

Kuna magonjwa mengi tofauti ya akili yanayoathiri ubongo wa binadamu na magonjwa haya ni kama yale yajulikanayo kwa majina ya bipolar disorder, huzuni ya kupindukia, schizophrenia, hali ya wasiwasi na yamagonjwa ya akili disorders yanayoathiri vile ambavyo mtu huwaza na huhisi. 
Chanzo kamili cha hakijulikani lakini kinachojulikana ni kwamba haya magonjwa hayatokani na kasoro ya kitabia au kasoro yoyote ya kiutu. 

Kutokana na tafiti mbalimbali, haya ni magonjwa kama magonjwa mengine kwasababu kadha wa kadha zinazodhaniwa ndizo sababishi za magonjwa hayo. 

Baadhi ya sababu hizo ni mabadiliko katika umbo la bongo ambapo mabadiliko hayo huathiri ubongo, hisia na tabia za mtu, mazingira ya mtu, uhusiano wake na watu wengine, maisha ya jamii na masaibu ya maisha kwa wakati mwingine huchangia magonjwa ya kichaa. 

Kwa mujibu wa taarifa mbalimbali, jamii tuishiyo, wanaume na wanawake wana nafasi sawa ya kuathiriwa maishani ingawaje wanaume ndio mara nyingi huathiriwa mapema maishani mwao. 

Tafiti zinaonyesha kuwa kuna aina mbili ya magonjwa ya akili na dalili za haya magonjwa zimetofautiana, mfano Psychosis, hii hutokea pale Mtu hushikwa na hali ya wendawazimu na kuchanganyikiwa, Mood disorders hutokea pale mtu hushikwa na huzuni ya kupindukia, wasiwasi, woga, ukosefu wa usingizi, ukosefu wa hamu na mambo ambayo mtu hupenda kufanya na ukosefu wa hamu ya kula hivyo mabadiliko haya ambayo yanaweza kutokea ghafla au pole pole hufanya iwe vigumu kusoma, kufanya kazi au kuwa na uhusiano wa kawaida na watu wengine. 

Karibia magonjwa yote ya akili yanatibika au madhara yake kupunguzwa kupitia matibabu, psychotherapy au mashauri lakini Uponyaji wa haya magonjwa hurahisishwa wakati watu wanapoelewa na kuwatunza kwa njia ya kiutu wale ambao wameathiriwa. 

Katika jamii mbalimbali, mtu aliyeathiriwa mara nyingi hubaguliwa na kutengwa na watu wengine kwasababu ya hali aliyonayo au wakati mwingine kutoelewa tabia ya mtu mwenye ugonjwa huo. 

Ni jambo la muhimu kuzingatia tabia za mila ya aliyeathiriwa wakati anapotibiwa ili aweze kupona na hatunabudi kuonyesha upendo na uelewano ambao utamsaidia mgonjwa huyo kurejea katika hali yake ya kawaida kama wengine. 

Tafiti zinaonyesha kuwa ugonjwa wa akili huathiri mara nyingi watu wa umri kuanzia miaka 15 hadi 25 kwa mara ya kwanza, ingawaje ugonjwa huo unaweza kutokea baadaye maishani. 



Theluthi moja ya walioathiriwa na ugonjwa wa akili hukumbwa na kipindi kimoja ama vichache vifupi tu maishani ingawa kwa wengine huendelea kuathiriwa kwa kurudiarudia maishani mwao ambapo mwanzo wa ugonjwa huu unaweza kutokea ghafla na dalili kali kuonekana zaidi wiki zinazofuata au unaweza kuathiri mtu polepole, na kuonekana kwa miezi au hata miaka. 

Hapo mwanzoni, aliyeathiriwa hujitenga na watu, huwa na huzuni na hali ya wasi wasi, yeye pia huwa na mawazo ya kustaajabisha au hofu nyingi hivyo kuna haja na umuhimu wa kufahamu dalili kwa mtu huyo ili aweze kupata matibabu mapema. 

Utambuzi mapema wa dalili hizo na kuchukua hatua zifaazo kutibu kwa mgonjwa wa akili ni muhimu kwani kutoelewa ugonjwa huu kunasababisha unyanyapaa, upweke na ubaguzi unaoweza kuathiri wale walio patwa na ugonjwa wa akili na jamii zao pia zinazowatunza. 

Bwana Thaddeus Kamisa ni mwanafunzi aliyehitimu Shahada ya mambo ya Jamii (Sociology) katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino kilichopo jijini Mwanza ambaye pia amewahi kufanya kazi katika baadhi ya Mashirika yanayojihusisha na watu wenye Ugonjwa wa Akili kama vile Basic Needs anabainisha dalili mbalimbali kuu za magonjwa ya akili. 


Bwana Kamisa alisema kuwa, baadhi ya dalili za ugonjwa wa akili ni pale mtu kuwa na Maono ya uwongo ama imani ya uwongo ya kudhulumiwa, kujilaumu au mambo makubwa au kutawaliwa na mwengine inaweza kupelekea kupatwa na ugonjwa huo. 

Mtu huyo hufikiri kwamba watu fulani wanapanga njama dhidi yake ama ana nguvu zisizo za kawaida na wakati mwingine waathiriwa watajitenga na kujificha ili kukwepa hizo dhuluma anazoziwaza. 

Anaeleza kuwa, mtu kupotewa akili ni dalili nyingine ambapo kwa kawaida inahusisha kusikia sauti inayotokea lakini sio sana ikiwemo kuona, kugusa, kuonja au kunusa mambo mengine anayodhani ni ya kweli ingawa havipo. 

Pia mawazo ya fujo yanachangia hasa hutokea pale mtu huyo pindi anapopatwa na ugonjwa kama huo kuongea kwake huathirika mpaka ni vigumu kufahamu maongezi yake muda mwingine anakuwa anatamka maneno kwa njia isiyoeleweka na isiyo na maana. 

“ Dalili nyingine za ugonjwa wa akili hutokea pale mtu anapokosa hamu ya kutenda mambo ya kawaida ya kila siku, kama kufua au kupika na kupoteza uwezo kufanya hivyo, kukosa hamu ya kutenda, uhamisisha na moyo wa kujituma siyo uvivu bali ni vile ambavyo ugonjwa umemuathiri ”, alisema Kamisa. 

Kamisa anaendelea kusema kuwa, wakati mwingine matatizo ya kufikiria uwezo wa mtu kuwa na kina, kukumbuka, kupanga na kutunga pia huathirika, hivyo inakuwa ni vigumu zaidi kufikiri, kuwasiliana na kufanya shughuli za kawaida. 

Akizungumzia kuhusu baadhi ya magonjwa ya akili ambayo yanaweza kuwaathiri baadhi ya vijana wa Tanzania, alisema kuwa, matumizi ya pombe na madawa ya kulevya, haswa bangi na madawa mengine yajulikanayo kama ‘amphetamine’ yanaweza kusababisha mtindio wa ubongo kwa vijana hao pia kwa watu ambao wanaweza kuathiriwa na mpumbao wa ubongo kiurahisi ingawaje matumizi ya madawa hausababishi mpumbao wa ubongo una uhusiano mkubwa na kipindi cha kuathiriwa kurudi. 

“ Kwa mujibu wa takwimu za Kitaifa inasadidika kuwa asilimia 61% ya wagonjwa wa akili katika wilaya ya Ukererewe mkoani Mwanza ni vijana hali ambayo inachangia ongezeko la umasikini katika jamii ”, alisema Kamisa. 

Aliendelea kusema kuwa, tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa asilimia 20 ya vijana wote duniani wana tatizo la afya ya akili ambapo asilimia 85 ya vijana hao wanaishi katika nchi masikini ikiwemo Tanzania. 

Kamisa alifafanua kuwa, kwa mujibu wa Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2002, Tanzania inakadiliwa kuwa na watu wapatao milioni 45 na kati yao vijana ni zaidi ya asilimia 35. 

Aidha alibainisha kuwa, Sera ya maendeleo ya Taifa ya Vijana inasema kuwa kijana ni mtu mwenye umri kati ya miaka 18 hadi 35 ikitofautiana na ile ya Umoja wa Mataifa ambayo inayoonyesha kuwa ni mtu kuanzia miaka 18 hadi 24. 

Ugonjwa wa akili kwa namna moja au nyingine umekuwa ukilikumba zaidi kundi la vijana ambao ni nguvu kazi ya taifa huku ikidaiwa kuwa matumzi ya dawa za kulevya yana mchango mkubwa katika hilo. 

Ili Taifa changa kama Tanzania liweze kupiga hatua za haraka za maendeleo kwa vijana, Serikali pamoja na wadau wa maendeleo na jamii hawanabudi kuungana kwa pamoja katika kukabiliana na tatizo hilo ambalo limekuwa likichangia kwa kiasi kikubwa kupunguza nguvu kazi ya taifa hata kuwa kundi hatarishi katika jamii kwa sababu ya kufanya matukio ya kuhatarisha maisha. 

Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizoridhia Mikataba mbalimbali kuhusu afya ya akili licha ya tatizo hili kutokabiliwa kikamilifu kutokana sababu mbambali zikiwemo za umasikini na ukweli kuwa wagonjwa wanaendelea kuongezeka licha ya kuwa hakuna takwimu sahihi. 

Takwimu za Kanisa Katoliki nchini Tanzania zinaonyesha zaidi ya wagonjwa wa akili 68,000 wamepatiwa huduma za afya katika kituo cha Shirika la Mitume la Brothers of Charity kilichopo Marumba mkoani Kigoma kati yao wagonjwa 25,000 walilazwa na kuruhusiwa kuondoka baada ya kupata nafuu na Wagonjwa wa akili 43,000 walipata huduma kwa nyakati tofauti wakitokea majumbani mwao baada ya kupewa maelekezo sahihi ya matumizi ya dawa. 

Uchunguzi wa afya ya akili duniani uliofanyika mwaka 1990 ulibaini kuwa, maradhi hayo yalichangia asilimia 10.5 ya usumbufu na ufanisi duni ikilinganishwa na magonjwa mengine katika jamii na kwamba ifikapo mwaka 2020 magonjwa hayo yatachangia aslimia 15 ya usumbufu na ufanisi duni katika kukabiliana na maisha. 

Takwimu zinaonyesha kuwa kati ya magonjwa 10 yanayoongoza kusababisha hali ya ulemavu duniani, matano kati ya hayo ni magonjwa ya akili yanayochangia asilimia 28 ya maisha duni katika jamii. 

Pia inaelezwa kuwa, ugonjwa wa Sonona (‘Depression’) ni hatari sana katika jamii na kwamba ni ugonjwa mtambuka kwa sababu baadhi ya watu huupata kutokana na kuwa na vina saba vya ugonjwa huo, dawa za kulevya na misongo ya mawazo. 

Hali halisi ni kwamba limekuwa jambo la kawaida sana kuwaona baadhi ya wagonjwa wa akili wakiokota makopo,vyakula jalalani na wengine kushinda wakizurura mchana kutwa mitaani pasipo kutambua hatma ya maisha yao, hivyo jamii inapaswa kuwasaidia watu wa aina hii kwa kuwapatia misaada ya malazi na chakula. 

Daima jamii ikumbuke kwamba, siyo tu kuwa watu wote wenye matatizo ya akili walitumia dawa ya kulevya bali kuna waliozaliwa wakiwa na tatizo hilo, na wengine ilitokana na msongo wa mawazo, kutokana na hali hiyo ni vema tukatambua kuwa kila aliye na akili timamu leo anaweza kuwa mgojwa wa akili kesho. 

Kwa ujumla wananchi na viongozi wa kijamii wote kuna umuhimu mkubwa wa kulisemea kundi hilo kutokana na matatizo makubwa yanayowakumba, badala ya kufikiria manufaa yetu na kuwaacha wakiwa gizani wasijue la kufanya katika jamii. 

Ifahamike pia watu hawa wana haki zao zinazolindwa kama watu wengine kwani kuna umuhimu wa kuwathamini na kuwapatia mahitaji yao yote ya msingi badala ya kuendelea kuwaona kama mizigo katika familia na jamii, hivyo wanastahili matibabu, chakula na mahitaji yao mengine muhimu.

Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 753 336 000 au +255 625 917 902

Masengwa blog Ipo Play Store…Download HAPA ,Uwe unapata habari zote kwa urahisi zaidi
 Bofya Hapa
Powered by Blogger.