SERENGETI BOYS WAIPIGA BURUNDI 3-0
Timu ya taifa ya Tanzania chini ya miaka 17, Serengeti Boys, leo imeibuka na ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi ya vijana wenzao wa Burundi katika mchezo wa kirafiki uliopigwa kwenye Uwanja wa Kaitaba, Kagera.
Katika mchezo huo ambao Serengeti Boys inautumia kwa ajili ya maandalizi yao kabla ya kwenda Gabon kushiriki michuano ya Kombe la Mataifa Afrika kwa vijana chini ya miaka 17, ulishuhudiwa mpaka mapumziko timu hiyo ikiwa mbele kwa mabao 2-0.
Mabao hayo yalifungwa na Muhsin Makame dakika ya 20 na Nickson Kibabage, huku Yohana Mkomola akimalizia msumari wa mwisho dakika ya 72 kwa njia ya mkwaju wa penalti na kukamilisha idadi hiyo ya mabao 3-0.
Baada ya leo kumalizana na Burundi, Jumatatu ijayo kikosi cha Serengeti Boys kinatarajiwa kucheza mchezo wa mwisho wa kirafiki jijini Dar es Salaam dhidi ya Ghana kabla ya kwenda Morocco kuweka kambi ya mwisho ya kujiandaa na michuano hiyo ya vijana.
Katika michuano hiyo itakayoanza kuunguruma Mei 14, mwaka huu, Serengeti Boys imepangwa Kundi B sambamba na timu za Mali, Niger na Angola. Kama Serengeti Boys itafanya vizuri kwenye michuano hiyo, basi itajikatia tiketi ya kwenda kushiriki michuano ya Kombe la Dunia chini ya miaka 17 itakayofanyika hapo baadaye nchini India.
Masengwa blog Ipo Play Store…Download HAPA ,Uwe unapata habari zote kwa urahisi zaidi