MWANAUME AJIUA KWA KUNYWA SUMU KISA MAPENZI
WATU wawili wamekufa katika matukio tofauti mkoani Rukwa, akiwemo mkazi wa kijiji cha Isasa wilayani Nkasi, Charles Gervas (60) aliyejiua kwa kunywa sumu kutokana na kinachoelezwa kuwa ni wivu wa mapenzi.
Pamoja na vifo hivyo, mkazi wa kitongoji cha Mafulala, manispaa ya Sumbawanga, Joel Mwenga (48), anashikiliwa na Polisi kwa tuhuma za kuteketeza kwa moto nyumba ya Maria Kakoko (26) kwa wivu wa mapenzi.
Taarifa za awali za Polisi zinaeleza kuwa, Gervas alichukua uamuzi wa kujiua kwa sumu baada ya kukataliwa na mkewe Maria Mtete (35) ambaye alimtaka mume huyo ampatie talaka kwa kuwa amempata mwanaume mwingine ambaye ni wa rika lake.
Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Rukwa, George Kyando, amethibitisha tukio hilo na kueleza kuwa ni la usiku wa kuamkia jana katika kijiji cha Isasa, wilayani Nkasi. Alisema Gervas alifariki dunia akiwa anapatiwa matibabu katika Kituo cha Afya katika kata ya Kirando, mwambao mwa Ziwa Tanganyika wilayani Nkasi.
“Mzee huyo alikunywa sumu ambayo haijajulikana mara moja, aliamua kukatiza maisha yake kwa kuchukua uamuzi huo baada ya kukataliwa na mkewe (Maria Mtete) ambaye alidai waachane kwa kuwa alikuwa amepata mwanaume mwingine,” alieleza Kamanda.
Alisema mwili umehifadhiwa katika chumba cha maiti katika Kituo cha Afya cha Kirando kwa uchunguzi ili kubaini aina ya sumu aliyokunywa. Aidha, Kamanda alisema mke wa marehemu alitoroka baada ya tukio hilo.
Katika tukio jingine kwenye kitongoji cha Kaloleni mashambani kijijini Kate wilayani Nkasi, Andrew Matandiko (16) alikufa baada ya kupigwa na radi juzi saa 4:00 mchana.
Katika tukio la moto, Kamanda Kyando alisema Mwenga anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kuchoma nyumba ya Kakoko kwa moto. Alisema tukio hilo ni la Machi 05, mwaka huu saa 5:30 usiku. Kamanda alisema chanzo ni wivu wa mapenzi.
Chanzo-Habarileo
Masengwa blog Ipo Play Store…Download HAPA ,Uwe unapata habari zote kwa urahisi zaidi