LEMA KUFUNGUKA YA MOYONI LEO


MBUNGE wa Arusha Mjini, Godbless Lema leo anatarajiwa kuhutubia wananchi wa jimbo lake katika uwanja wa Shule ya Msingi Ngarenaro baada ya kuachiwa kwa dhamana na Mahakama Kuu Kanda ya Arusha.

Hatua hiyo imeelezwa kuwa ni mtego kwake, kwani inaweza kumjenga kisiasa ama kumharibia kutokana na kile atakachotamka katika mkutano huo wa hadhara.

Lema aliyekaa gerezani kwa zaidi ya miezi minne, aliachiwa kwa dhamana Machi 3 mwaka huu na Jaji Fatuma Maghimbi na wadhamini wawili, waliosaini hati ya dhamana ya thamani ya Sh milioni moja kila mmoja.

Gari la matangazo lilikuwa likipita kila kona ya Jiji la Arusha na kutangaza kuwepo kwa mkutano huo na kuhamasisha wananchi wa Jiji la Arusha, kujitokeza kwa wingi kuhudhuria mkutano huo bila ya kukosa, kwani mbunge huyo ana ujumbe mzito kwa ajili yao.

Hata hivyo, si Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Amani Gulugwa wala Lema mwenyewe aliyekuwa tayari kueleza ajenda ya mkutano huo, kwani simu zao za kiganjani zilikuwa zikiita bila ya kupokewa.

Hata hivyo, mmoja wa madiwani wa Chadema waliotakiwa kutokosa katika mkutano huo, ambaye aliomba kuhifadhiwa jina lake, alisema kuwa mkutano huo unatarajiwa kuanza saa 9 mchana katika shule hiyo ya Ngarenaro.

Diwani huyo alisema lengo la mkutano huo wa hadhara wa Lema ni kutaka kuwashukuru wale wote walioshiriki kwa namna moja ama nyingine kufika gerezani, kumfariji na kumwombea kwa siku zote akiwa mahabusu katika Gereza la Kisongo, nje kidogo ya Jiji la Arusha.

Alisema pili ni kutaka kujua kero walizonazo wananchi wa jimbo la Arusha Mjini maana kwa muda aliokaa gerezani ni muda ambao huenda kero zimekuwa nyingi ili aweze kuzifanyia kazi mbali ya yeye alizonazo ambazo anataka kuwaeleza wananchi namna ambavyo ataanza kuvifanyia kazi.

“Hakuna kipya zaidi ya hicho na huenda mkutano huo utakuwa wa amani kubwa sana na wananchi wanahamu ya kumwona mbunge wao waliomkosa kumwona zaidi ya miezi minne,’’ alisema diwani huyo.

Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu jana, Kamanda wa Polisi Mkoani Arusha, Charles Mkumbo alisema kuwa taarifa ya kufanyika kwa mkutano hupelekwa na viongozi wa vyama vya siasa kwa wakuu wa polisi wa wilaya (OCD) na ofisi hiyo ndio wenye jukumu la kuweka ulinzi katika mkutano huo.

Mkumbo alisema huenda taarifa za kuwepo kwa mkutano huo zimeshawasilishwa kwa kiongozi huyo wa wilaya na yeye ndiye mwenye mamlaka ya kuweka ulinzi katika mkutano ili kila kitu kiwe salama mwanzo wa mkutano na mwisho wa mkutano.

Alisema mara nyingi viongozi wa vyama vya siasa katika Jiji la Arusha wanapotaka kufanya mikutano ya hadhara huwasiliana na OCD wa Arusha Mjini na viongozi hao wanajuwa taratibu.

Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 753 336 000 au +255 625 917 902

Masengwa blog Ipo Play Store…Download HAPA ,Uwe unapata habari zote kwa urahisi zaidi
 Bofya Hapa
Powered by Blogger.