MAHARUSI WAFARIKI DUNIA BAADA YA KUTOKA KUOANA

INASIKITISHA! Pengine hilo ndiyo neno rahisi linaloweza kutumiwa kuelezea mkasa wa kufariki kwa maharusi waliotoka kufunga ndoa mkoani Arusha pamoja na watu wengine watatu wakiwamo mama mlezi na dada wa bwanaharusi.

Wafu katika tukio hilo lililotokana na mvua zinazoendelea kunyesha kufurisha maji yaliyolisomba gari lililowabeba wahusika, ni maharusi wawili, Minis Loyi (25) na Nembris Mungaya (20).

Maharusi hao na watu wengine watatu walikufa maji baada ya gari walilokuwa wakisafiria wakitoka kufunga ndoa kusombwa na majira ya saa 4:00 usiku, juzi. Tukio hilo lilitokea baada ya mvua kubwa kunyesha mfululizo juzi

kuanzia majira ya alasiri hadi usiku na kusababisha mafuriko katika mito mingi mkoani Arusha.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo, alisema jana kuwa tukio hilo lilitokea juzi katika Kijiji cha Timbolo kilichopo Kata ya Shambasha, katika eneo la chini ya Mlima Meru, wilayani Arumeru.

Kamanda Mkumbo alisema ajali hiyo ilitokea wakati maharusi na ndugu zao wakirejea kijijini kwao Kyoga baada ya kufunga ndoa ya kimila iliyofanyika kwenye Kijiji cha Timbolo.



Alisema abiria hao walitumia gari aina ya Toyota Premio, lenye namba za usajili T 579 BSG lililokuwa likiendeshwa na Yusuf Jacob (35).



Wengine waliokufa, kwa mujibu wa Kamanda Mkumbo ni mama mlezi wa bwana harusi, Inoti George (40) na dada wa bwana harusi, Shengai Saiguran (30).

Alimtaja mwingine aliyekufa kuwa ni mtoto Ngaisi Monuo (11) na kwamba, wote ni wakazi wa Kijiji cha Kyoga.

VIFO VINGINE VYA MAJI


Mbali na tukio hilo, Kamanda Mkumbo alisema, mtu mwingine katika Kijiji cha Kerian, Babu Robikeki (33) alisombwa na maji na kufariki dunia pia wakati akivuka mto, juzi.

Aidha, alisema dereva wa pikipiki (bodaboda) Seuli Meseyeki (37) alikufa maji baada ya pikipiki yake yenye namba za usajili T 726 DFD aina ya T. Better kusombwa na maji pia katika eneo la Olorien Ngaramtoni wakati anavuka kwenye maji yaliyofunika barabara.

Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 753 336 000 au +255 625 917 902

Masengwa blog Ipo Play Store…Download HAPA ,Uwe unapata habari zote kwa urahisi zaidi
 Bofya Hapa
Powered by Blogger.