GRUMETI FUND YATOA ELIMU YA STADI ZA MAISHA KWA VIJANA 100 SERENGETI

  

Shirika la Grumeti Fund limeendelea kuweka alama katika maendeleo ya jamii baada ya kutoa mafunzo ya stadi za maisha kwa zaidi ya vijana 100 wanaofadhili kimasomo na Shirika hilo kutoka vijiji  22  vya wilaya za Serengeti na Bunda, mafunzo ambayo yanalenga kuwawezesha vijana kuwa na uwezo wa kujitegemea na kukabiliana na changamoto za kimaisha kwa kutumia mbinu mbadala na chanya.

Akizungumza baada ya mafunzo hayo, Bi. Elizabeth Magoto ambaye ni Afisa Elimu, Idara ya Maendeleo ya Jamii kutoka Shirika la Grumeti Fund amesema kuwa shirika hilo mbali na kutoa elimu ya stadi za maisha pia, Shirika hilo linawasaidia vijana katika kuwapatia ufadhili wa kimasomo huku akiongeza kuwa katika kundi hili la vijana, mafunzo yalijikita zaidi katika kuwajengea uwezo wa kujitambua, stadi za biashara, teknolojia, mawasiliano bora sambamba na usimamizi wa fedha.

"Leo tumekutana na vijana zaidi ya 100 lengo likiwa ni kufundisha stadi za maisha kwani zipo stadi ambazo vijana wanatakiwa kuwa nazo lakini hazifundishwi mashuleni hivyo Grumeti Fund tunaamini kuwa kwa kuwajengea vijana msingi imara wa stadi za maisha, tunatengeneza jamii yenye uelewa mpana ambayo inaweza kushiriki kikamilifu katika shughuli za kimaendeleo bila utegemezi" alisema Bi. Elizabeth 

Aidha Bi. Elizabeth amebainisha kuwa programu hii ni sehemu ya mikakati ya muda mrefu wa Shirika Hilo kutengeneza kizazi cha vijana chenye kujiamini, kujitambua sambamba na kupambana na umaskini na ukosefu wa ajira kwani kupitia mafunzo haya vijana wanakuwa na ujasiri wa kuanzisha miradi midogo midogo ya ujasiriamali.
Kwa upande wake Afisa Miradi Grumeti Fund Idara ya Maendeleo ya Jami Ndg. Philip Kitasho, amewataka vijana walionufaika na mafunzo hayo, kutumia muda wa likizo kuanzisha biashara ndogondogo huku wakitumia ujuzi waliopata katika mafunzo jambo ambalo litaounguza utegemezi wao kwa wazazi na kuwataka kusambaza ujuzi huo kwa vijana wengine ili jamii nzima iweze kunufaika.

Nao baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wamelishukuru Shirika la Grumeti Fund kwa elimu hiyo huku wakiaidi kuyaweka katika vitendo yote waliyofundishwa na kuwa mabalozi wema wa mabadiliko katika jamii zao, wakitumia maarifa waliyopata kujenga maisha bora na yenye tija kwa ajili ya mustakabali wa jamii zao na Taifa kwa ujumla.


Post a Comment

0 Comments