WACHIMBAJI madini 15 waliofukiwa mgodini katika kata ya Nyarugusu
wilaya ya Geita mkoa wa Geita na kupelekwa hospitali ya mkoa huo,
waliruhusiwa juzi.
Waliruhusiwa baada ya kupata matibabu huku baadhi ya ndugu zao wakionekana kushangazwa na hatua hiyo.
Katika muda wa chini ya saa 24 waliyokuwa wanapata matibabu hospitalini, manusura hao vijana walionekana kuwa na furaha tele.
Waliishukuru serikali na wadau wengine, kwa kuchukua hatua za haraka, zilizofanikisha kuokoa maisha yao.
Alipokutana nao muda mfupi baada ya kutolewa wodini, Mkuu wa Mkoa wa
Geita, Meja Jenerali mstaafu, Ezekiel Kyungu alipongeza viongozi wa
hospitali ya mkoa kwa kuwatibu manusura wa ajali hiyo baada ya kutolewa
kutoka mgodini chini ya umbali wa mita 60 huku wakiwa wanakabiliwa na
njaa.
‘’Tunamshukuru Mungu kwamba mko salama baada ya ajali mliyopata
ambayo ilishtua kila mmoja wetu. Nimearifiwa kwamba mmepatiwa matibabu
yenye weledi wa kutosha, kiasi kwamba sasa mnarejea nyumbani mkiwa na
afya njema, nachukua nafasi hii kumshukuru kila mmoja aliyeshiriki
katika operesheni ya uokozi,’’ alisema Mkuu huyo wa Mkoa.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa, serikali imeshatoa maelekezo kwa mgodi
husika, unaomilikiwa kwa ushirikiano kati ya mwekezaji kutoka China, RZ
Union Mining Ltd na Mtanzania, Ahmed Mubarak kuendelea kufungwa kwa muda
wa siku tano, ukisubiri uchunguzi unaoendelea juu ya nini
kilichosababisha ajali hiyo na mbinu za kufanya ili kuzuia ajali kama
hiyo.
Alisema tukio la ajali ya Nyarugusu, pia limeiamsha serikali kuchukua
hatua za kukabiliana na hali ya operesheni dhidi ya wachimbaji wadogo
na wa kati mkoani Geita haraka iwezekanavyo kuhusu hatua za usalama.
Alikuwa ananukuu maelekezo yaliyotolewa na Naibu Waziri wa Nishati na
Madini, Dk Medard Kalemani aliyetembelea mkoa huo Jumapili baada ya
ajali katika mgodi huo wa Nyarugusu.
Hatua nyingine kali ya serikali itafuatia kwa wawekezaji wa madini,
ambao sasa watatakiwa kutoa mikataba ya uhakika kwa wafanyakazi wao,
ikiwa ni pamoja na kuweka kipengele cha kulipwa fidia, iwapo watapata
ajali katika operesheni za uchimbaji wa madini.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, mmoja wa maanusura wa ajali hiyo,
Anicet Masanja alisema wamefanikiwa kuishi na kunusurika kwa siku nne
kutokana na mwamba na hewa ndani ya shimo walilokuwemo ardhini, uliozuia
mchanga kuwaporomokea walipokuwa wanapambana kutafuta njia ya kujikoa.
‘’Isingekuwepo umbile zuri la mwamba na miundombinu kuwa imara,
tungekuwa tunazungumza lugha nyingine leo. Kwa ujumla tunamshukuru Mungu
kwa muujiza uliojitokeza na juhudi za hospitali ya mkoa na wadau
wengine, zilizofanikisha kuokolewa maisha yetu,’’ alieleza Masanja.
Wakati huo huo, Wizara ya Nishati na Madini imesema inapenda
kuufahamisha umma kuwa kazi ya kuwaokoa wachimbaji 15 waliofukiwa na
kifusi Januari 26, mwaka huu kwenye mgodi wa dhahabu eneo la kijiji cha
Mawemeru, Nyarugusu wilayani Geita limekamilika kwa mafanikio.
Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Nishati na Madini jana, ilieleza
kuwa ajali ya kufukiwa wachimbaji hao iliyohusisha Watanzania 14 na raia
mmoja wa China, ilitokea kwenye leseni ya uchimbaji wa kati wa madini
ya dhahabu yenye Namba ML 492/2013, inayomilikiwa na Ahmed Mubarak Adam.
Chanzo cha ajali hiyo, kwa mujibu wa wizara hiyo, ilikuwa ni kuanguka
kwa shafti ya mgodi huo na kufukiwa na kifusi wakati wachimbaji hao
wakifanya kazi mgodini chini ya ardhi.
Akizungumza baada ya kuokolewa wachimbaji hao, Naibu Waziri wa
Nishati na Madini, Dk Medard amewashukuru wadau wote walioshiriki kwa
hali na mali, kufukua kifusi na hatimaye kufanikiwa kuwatoa wachimbaji
chini ya ardhi wakiwa hai.
Dk Kalemani aliwaomba Watanzania kuendelea na moyo huo, pale majanga
kama haya yanapotokea. Pia, aliagiza ukaguzi wa kina, ufanyike kwenye
migodi mingine ya wachimbaji wadogo na ya kati eneo la Nyarugusu na
kwingineko nchini ili kuhakikisha kuwa migodi inakuwa salama kwa
wachimbaji wa migodi husika.
CHANZO;
Imeandikwa na Pius Rugonzibwa,
Habari leo -Geita