
Baada ya Obrey Chirwa kuepuka kifungo cha TFF na pia kupona majeraha yake, ni dhahiri atamlazimu kocha Mkuu wa Yanga George Lwandamina kupangua safu yake ya ushambuliaji.
Lwandamina amekuwa akiwatumia Ibrahim Ajib na Donald Ngoma kama washambuliaji wa kati. Hata hivyo wawili hao wameshindwa kuipa Yanga matokeo katika mchezo wa kwanza dhidi ya Lipuli.
Tabia za uchezaji wa Ngoma na Ajib zinafanana, wanapenda kucheza mpira muda wote hivyo kuwafanya wasitulie kwenye namba zao.
Ni tofauti na wachezaji Obrey Chirwa na Amissi Tambwe ambao hupenda zaidi kubaki kwenye namba zao wakivizia nafasi za kufunga.
Wawili hao msimu uliopita walifunga jumla ya mabao 23, Chirwa akifunga mabao 12 huku Amissi Tambwe akifunga 11.
Ngoma anaweza kuinufaisha zaidi Yanga kama atacheza na mmoja wa washambuliaji hao.
Chirwa ana uwezo mkubwa wa kumiliki mpira, nguvu na kasi. Pia mshambuliaji huyu mwenye umri wa miaka 23 huweza kuisaidia timu katika ukabaji pale inapoelemewa.
Upo uwezekano mkubwa Lwandamina akamtumia kama mshambuliaji wa kati huku Ngoma akamchezesha nyuma yake kama namba 10 wakati Ajib akimuhamishia pembeni.
Watatu hao wana nafasi ya kucheza pamoja wakati huu ambao Tambwe bado anasumbuliwa na majeraha lakini atakapokuwa fiti ni dhahiri haitakuwa jambo la kushangaza kumuona Ngoma au Ajib mmoja wao akianzia benchi