ATIWA MBALONI KWA WIZI WA MTOTO MCHANGA

Image result for ASKARI POLISI
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia mwanamke mmoja Mkazi wa Kijiji cha Mchangani aliyefahamika kwa jina la Mode Barnaba kwa kosa la wizi wa mtoto mchanga aitwaye PETER BELINO mwenye umri wa miezi mitatu.

 
Tukio hilo limetokea mnamo tarehe 02.10.2016 majira ya saa 10:00 asubuhi katika Kijiji cha Ndaga, Kata ya Ndanto, Tarafa ya Ukukwe, Wilaya ya Rungwe, Mkoa wa Mbeya.
Inadaiwa kuwa mama mzazi wa mtoto huyo aitwaye ANNA BELINO FABIAN [25] Mkazi wa Ndaga wakati wa tukio hilo alikuwa anasukwa nywele nyumbani kwake na ndipo mtuhumiwa aliomba amshike mtoto na kisha kutoweka naye.
Baada ya mama mzazi kutoa taarifa Polisi, msako mkali ulifanyika na mtuhumiwa alikamatwa majira ya saa 12:00 mchana akiwa na mtoto huyo eneo la Stendi kijiji cha Mchangani akiwa katika harakati za kupanda gari kuelekea Mbeya Mjini.
Mtuhumiwa amefikishwa katika Mahakama ya Mwanzo Wilaya ya Rungwe tarehe 04.10.2016 na kesi imetajwa kusikilizwa tarehe 18.10.2016.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Naibu Kamishna wa Polisi DHAHIRI A. KIDAVASHARI ametoa wito kwa wazazi na walezi kuwa makini na watoto wao ikiwa ni pamoja na kuweka uangalizi wa kutosha ili kuepuka vitendo vya wizi wa watoto.
Aidha ametoa wito kwa jamii kushirikiana na Jeshi la Polisi hasa kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu ili kuzuia vitendo hivyo

Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 753 336 000 au +255 625 917 902

Masengwa blog Ipo Play Store…Download HAPA ,Uwe unapata habari zote kwa urahisi zaidi
 Bofya Hapa
Powered by Blogger.