WAANDISHI WA HABARI WAUAWA KWA SHAMBULIO LA ISRAEL


Shirika la utangazaji la Al Jazeera limeripoti leo kuwa mwandishi wake wa habari anayefanya kazi na moja ya chaneli zake ameuawa katika shambulio la Israel akiwa ndani ya gari lake kaskazini mwa Gaza.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Hussam Shabat, aliyekuwa akihusiana na Al Jazeera Mubasher, aliuawa katika shambulio la ndege zisizo na rubani za Israel lililolenga gari lake siku ya Jumatatu mchana, karibu na sheli ya mafuta katika mji wa Beit Lahia. Shirika la ulinzi wa raia la Gaza limethibitisha kifo chake.

Aidha, shirika hilo limethibitisha pia kifo cha Muhammad Mansour, mwandishi wa habari wa Televisheni ya Palestine Today, yenye uhusiano na Islamic Jihad, ambaye aliuawa katika shambulio la anga lililopiga nyumba yake katika mji wa Khan Yunis asubuhi ya siku hiyo hiyo.

Msemaji wa ulinzi wa raia wa Gaza, Mahmud Bassal, amesema kuwa zaidi ya magari 10 yamelengwa na mashambulizi ya anga katika maeneo mbalimbali ya Ukanda wa Gaza.

Katika taarifa yake, Jumuiya ya Wanahabari wa Palestina imelaani vifo vya Shabat na Mansour, ikivitaja kuwa “uhalifu uliorikodiwa kwenye rekodi ya ugaidi wa Israel.” Jumuiya hiyo imesema kuwa zaidi ya waandishi wa habari 206 na wafanyakazi wa vyombo vya habari wameuawa tangu kuanza kwa vita, vilivyotokana na shambulio la Hamas dhidi ya Israel Oktoba 7, 2023.

Israel ilianza tena mashambulizi makali ya anga katika Ukanda wa Gaza wiki iliyopita, na kufuatiwa na operesheni za ardhini, baada ya kusitisha makubaliano ya wiki sita ya kusitisha mapigano na Hamas.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Gaza, inayoendeshwa na Hamas, watu 730 wameuawa tangu Israeli kuanza tena mashambulizi Machi 18, ikiwa ni pamoja na 57 waliouawa katika saa 24 zilizopita.

Post a Comment

0 Comments