
Bwawa la Kufua Umeme la Mwalimu Nyerere.
SERIKALI ya Awamu ya Sita imepongezwa kwa kukuza uchumi wa nchi. Hayo yamesemwa hivi karibuni na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba kuwa uchumi wa nchi umetulia.
Tutuba alisema uchumi wa Tanzania Bara unatarajiwa kuendelea kukua kwa kasi na Pato la Taifa (GDP) linatarajiwa kukua kwa takribani asilimia sita katika nusu ya pili ya mwaka wa fedha 2024/2025.
Alisema ukuaji huo unatarajiwa kuchangiwa na hali nzuri ya hewa, upatikanaji wa pembejeo kwa wakati na uwekezaji unaoendelea kufanyika katika miundombinu ya umwagiliaji, huduma za usafirishaji, uwepo wa umeme wa uhakika na utekelezaji wa sera ya fedha na ya bajeti.
Mtaalamu wa uchumi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Haji Semboja amesema katika miaka minne ya Rais Samia uchumi wa nchi unakua kwa sababu ametekeleza kwa vitendo kaulimbiu ya ‘Kazi Iendelee’.
“Ametekeleza miradi ya kiuchumi aliyoiacha mtangulizi wake ambayo mingi ilikuwa iko asilimia 20 hadi 30, lakini Samia ndani ya muda mfupi baadhi imefika asilimia 100 na imefungua fursa za uchumi,” alisema Profesa Semboja.
Alitaja miradi hiyo ni ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) na sasa kuna safari za treni za abiria kati ya Dar es Salaam na Dodoma.
Aidha, mradi mwingine ni kuendelea na ujenzi wa Bwawa la Kufua Umeme la Mwalimu Nyerere katika Mto Pangani (JNHPP) ambalo miaka minne iliyopita ujenzi wake ulikuwa chini ya asilimia 30 na leo umefika asilimia 99.
“Kwa mambo haya na miradi mingine ya kiuchumi imesaidia kukuza uchumi na hii inampa Rais Samia msingi wa kujua tunapokwenda, hatutakwama tena kwenye reli ya SGR na mingine,” alisema Profesa Semboja.
Aliongeza: “Kuna shughuli na uchumi zimeanzishwa na zinakwenda vizuri, si mtu mmoja ana shughuli kila mtu ana kitu cha kufanya kinachomletea kipato, siku hizi hakuna tena kumsikia mtu akisema ninaishi kwa mjomba, kila mtu ana wivu wa kutafuta fursa inayomletea kipato kwa sababu fursa zimefunguka ni nyingi za kiuchumi”.
Mhadhiri wa uchumi UDSM, Profesa Humphrey Moshi alisema pamoja na changamoto alizozikuta ikiwemo vita ya Urusi na Ukraine, athari za janga la Covid-19 na kuadimika kwa Dola za Marekani, Rais Samia ametekeleza miradi ya kimkakati yenye manufaa makubwa kwa uchumi wa nchi.
Mchambuzi wa uchumi, Gabriel Mwang’onda alisema katika miaka minne ya Rais Samia Uchumi umeendelea kuimarika.
“Tumetoka kwenye Covid-19 namna pekee ya kupima uchumi ni mapato ya ndani ya nchi (GDP), ambayo takwimu zinaonesha tunapanda vizuri, tumetoka kwenye ukuaji wa asilimia nne hadi 5.9 kuelekea kwenye sita… maana yake uchumi unakua,” alisema Mwang’onda.
Aliongeza: “Tumeona pia kwenye sekta ya uzalishaji bajeti ikiongezeka, ajira mpya kwenye sekta ya afya, usambazaji wa dawa ikifika zaidi ya asilimia 80 kutoka asilimia chini ya hizo”.
Katika uzalishaji Mwang’onda alisema Tanzania ndani ya miaka minne imeimarisha uzalishaji wa mahindi Afrika na kuwa nchi ya pili ikiipita Nigeria lakini pia imekuwa nchi ya pili kwenye uzalishaji wa tumbaku na ni nchi pekee inayotoa ruzuku ya mbolea kwa asilimia kubwa kwa wakulima.
0 Comments