
Akizungumza na Wahariri wa Michezo jana kwenye Hoteli ya Kilimanjaro Kempinsk Dar es Salaam,alisema kuwa mpango wa Simba ni kutoka kisasa kuanzia ofisi na uwanja.
"Tumejipanga, hili la Uwanja wa Bunju, na hadi kufikia mwisho wa mwezi huu, tutazikomboa nyasi za Uwanja wa Bunju ambazo ziko bandarini hadi sasa.
"Kuna mfadhili amekubali kutujengea uwanja na hili zaidi itakuwa uwanja wa kuchezea na kama uwanja una mambo mengi, suala hili hadi mwisho wa mwaka Simba inaweza kuwa katika hatua nzuri.
"Kingine ni kujenga ofisi za kisasa, Simba inataka kwenda na mabadiliko, itakuwa na ofisi za kisasa kabisa, na tunataka kuwa na chumba maalumu cha wanahabari, media centre kwamba habari zitakuwa zinarushwa kutoka klabuni.
"Hapa itakuwa kila kiongozi anapatikana hapo," alisema Salim bila kutaja eneo litakalojengwa ofisi za Simba.
Kuhusu wachezaji wanaomaliza mikataba yao, Salim 'Try Again' alisema kuwa mpango wa klabu yake ni kuhakikisha inawabakisha wachezaji muhimu wa timu hiyo.
Wachezaji wanaomaliza mikataba yao mwishoni mwa msimu ni pamoja na kiungo mshambuliaji, Ramadhani Kichuya, Said Ndemla, Ibrahim Mohamed 'MO' na Muzamiru Yassin.
"Hakuna mchezaji atakayeachwa Simba, tunafahamu mikataba yao inamalizika lakini kama viongozi tumekaa nao na tumewaambia tuko nao pamoja, wafanye kazi mambo mazuri yanakuja," alisema.
Akizungumzia suala la MO kulalamikiwa na kocha wake, Pierre Lechantre, Salim amesema kuwa wamekutana na mchezaji husika, wamezungumza naye na yeye akawaleza matatizo yake na akaahidi kubadilika.
Hivi karibuni, Kocha wa Simba, Pierre Lechantre alisema kuwa mchezaji huyo amekuwa na tabia ya kutokuja mazoezini na akija anakuwa na sababu nyingi kila mara jambo ambalo
linaathiri kiwango chake na akasema hatoweza kumtumia.
"Simba sio timu ya sikukuu ambayo unaamua leo uje kesho usije . Mchezaji mwenye weledi sahihi na kazi yako huwezi kuacha kuyapa kipaumbele mazoezi ya mwalimu wako, masilahi ya
timu na kipaji chako” alisema Lechantre kwa ukali.
Salim alisema baada ya kumalizana na suala la mchezaji huyo, kuanzia sasa klabu haitavumilia utovu wa nidhamu wa mchezaji yeyote.
"Hakuna mchezaji aliye juu ya klabu, uwe maarufu kwa jina, uwe maarufu kwa nini, hatua za kinidhamu zitachukuliwa tu juu yake," alisema.
Kuhusu hisa za MO, alisema: "Tumekuwa na mazungumzo marefu na Serikali, lakini niseme tu tumefikia mahala pazuri na hivi karibuni tutakuja na majibu."
Amesema kuwa ni kweli mpango wa Simba ni kugawana asilimia 50-50 kuwa mdhamini anachukua nusu sawa na wanachama, lakini Serikali inataka 51-49 hatua aliyosema inakanganya na kuhitaji mazungumzo zaidi.
Hili la bima kwa wachezaji, siku moja baada ya Rais wa TFF, Wallace Kariua kusema klabu za Ligi Kuu zitabanwa kwa kushindwa kuwawekea bia wachezaji wake, Simba imekuwa ya kwanza kujisafisha.
"Tumewakatia bima wachezaji wetu, zaidi ya Sh300mil, hii ina maeneo mengi na kwa mchezaji mmoja akiumia anaweza kupata hata Sh110mil kutegemea na alivyoumia uwanjani,"
amesema Salim.
Tags:
michezo