
Sare ya Simba ya mabao 3-3 dhidi ya Stand United imewapa ahueni wapinzani wao wakubwa Yanga ambao wanahitaji ushindi katika mechi mbili tu ili kuwafikia kwani wekundu wa Msimbazi wamefikisha pointi 46 na Yanga ikiwa na 40.
Kukosekana kwa John Bocco na Emmanuel Okwi katika mchezo wa jana kunatajwa kuwa moja ya sababu ya kuikosesha timu hiyo ushindi huku uzembe wa safu ya ulinzi nao ukiwagharimu.
Simba ilianza mchezo huo kwa kasi na dakika ya sita Asante Kwasi aliipatia Simba bao kwa shuti la kawaida baada ya Nicholas Gyan kuwatoka mabeki wa Stand United na kupenyeza pasi iliyomkuta mfungaji.
Timu hiyo iliendelea kutafuta ushindi na dakika ya 23 Laudit Mavugo aliipatia Simba bao la pili kwa shuti kali baada ya wachezaji wa Simba kugongeana pasi vizuri kabla ya Shomari Kapombe kutoa pasi kwa mfungaji aliyeukwamisha mpira wavuni.
Kuingia kwa bao hilo hakukuwakatisha tamaa Stand United kwani walijipanga na kufanya shambulizi lililowawezesha kupata bao la kwanza dakika ya 35 lililofungwa na Tariq Seif kwa kichwa akimalizia krosi ya Aron Lulambo.
Stand walizidi kulishambulia lango la Simba kama nyuki na kufanikiwa kupata bao la pili lililofungwa na Aron Lulambo aliyepiga kona iliyokwenda moja kwa moja wavuni na kumshinda kipa Aishi Manula.
Kona hiyo ilitokana na beki wa Simba,James Kotei kuokoa shambulizi lililokuwa likielekea golini kwao.
Kipindi cha pili timu zote zilianza mpira kwa nguvu na dakika ya 61 Nicholas Gyan aliipatia Simba bao la tatu akimalizia mpira uliotemwa na kipa wa Stand United,Mohammed Makaka wakati akipangua kona ya Mzamiru Yassin.
Dakika sita baadae Stand United walisawazisha bao hilo kupitia kwa Brigimana Blaise aliyempiga chenga beki Erasto Nyoni na kuachia shuti kali lililotinga wavuni.
Baada ya kufunga bao hilo Blaise ambaye alishangilia kwa kuvua jezi na kuwaonyesha mashabiki wa Simba alitolewa baada ya kuumia na nafasi yake kuchukuliwa na Sixtus Sabilo.
Ligi hiyo itaendelea tena keasho kwa Azam kuikaribisha Singida United kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi, Kagera Sugar itacheza na Majimaji kwenye Uwanja wa Kaitaba Bukoba, Njombe Mji itakuwa mwenyeji wa Ruvu Shooting Uwanja wa Sabasaba Njombe wakati Prisons wataikabili Mbao kwenye Uwanja wa Sokoine Mbeya.
Tags:
michezo