Taarifa ya siku ya tisa ya ziara mahsusi ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhe January Makamba kutembelea mikoa ya Kaskazini mwa Tanzania ambapo ametembelea na kukagua Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro iliyopo katika wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha.
Ziara hiyo inalenga kukagua shughuli za hifadhi ya Mazingira, kusimamia utekelezaji wa sheria za mazingira, kuangalia namna bora zaidi ya kusaidia serikali za mitaa na mamlaka za wilaya na mikoa ili kuzijengea uwezo mkubwa zaidi wa kusimamia hifadhi na sheria za mazingira pamoja na kuweka mahusiano bora zaidi katika utunzaji wa Mazingira kati ya Serikali Kuu, Serikali za Mtaa, watu binafsi na taasisi za mazingira.
Akiwa katika mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro yenye ukubwa wa kilometa za mraba 8,292 na ambayo inatumika kwa matumizi mseto ya ardhi ambapo uhifadhi wa maliasili unafanyika pamoja na ufugaji, Waziri Makamba amepata wasaa wa kutembelea na kukagua shughuli za utunzaji na uhifadhi wa mazingira katika hifadhi hiyo ambayo ina hadhi ya eneo mseto la urithi wa Dunia (Mixed World Heritage Site).
Waziri Makamba ametembelea na kukagua maeneo ya hifadhi ikiwemo eneo la kreta ambapo amejionea changamoto kubwa ya mimea vamizi (Alien/Invasive Plant Species) inayokua kwa kasi ndani ya eneo hilo suala ambalo ni tishio katika mfumo wa asili wa ekolojia kwani wanyama wanayatenga maeneo hayo.
Katika ukaguzi wake pia Waziri Makamba amegundua kuwa kuna taasisi zilizo ndani ya hifadhi hasa katika mzunguko wa kreta ambazo zinatumia maji yaliyo ndani ya kreta kwa shughuli za kila katika uendeshaji wa taasisi hizo. Taasisi hizo hutegemea maji yanayotoka kwenye chanzo cha maji cha Lerai suala ambalo Waziri Makamba amesema ni tishio kubwa kwa hifadhi kwa miaka ya mbeleni.
Baada ya kutembelea na kukagua shughuli za utunzaji wa mazingira ndani ya hifadhi Waziri Makamba amekutana na kuzungumza na Baraza la Wafugaji Ngorongoro ambalo ni chombo rasmi kilichoanzishwa chini ya sheria ili kwa uzoefu wake lisaidie kubaini mahitaji halisi ya wafugaji wenyeji. Katika mkutano huo ambao Waziri Makamba ambaye aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro Rashid Taka, amepokea taarifa fupi ya Mazingira ya mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro iliyoainisha changamoto kadhaa za kimazingira zinazoikumba hifadhi. Changamoto hizo ni pamoja na kuongezeka kwa idadi ya watu na mifugo katika hifadhi hivyo kuongeza uharibifu wa mazingira pamoja na shughuli za kibinadamu, kuongezeka kwa mimea vamizi (kama alivyojionea Waziri ndani ya kreta), pamoja na athari za mabadiliko ya ya tabia nchi kunakopelekea kupungua kwa malisho na maji ya mifugo.
Kabla ya Waziri kupata wasaa wa kuzungumza Mwenyekiti wa Baraza la Wafugaji Ngorongoro Edward Maura amempongeza Waziri Makamba kwa kufika kuzungumza na baraza hilo ambalo kisheria ni chombo rasmi cha uwakilishi wa wananchi wote wa Ngorongoro. Mwenyekiti huyo ameainisha kuwa jamii ya Kimasai inafanya jitihada kubwa za kutunza na kuhifadhi mazingira ndani na nje ya hifadhi na kwamba ni mwiko kwa jamii hiyo kukata miti na hivyo wao ni jamii rafiki kwa mazingira na wizara inayoshughulikia mazingira kwa ujumla. Pamoja na hayo Mwenyekiti huyo wa Baraza la Wafugaji amemuomba Waziri Makmba kumaliza utata na mgongano wa muda mrefu unaopeleke kuchelewa kuanzishwa kwa Ranchi ya RAMAT ndani ya hifadhi hiyo ambayo itasaidia wafugaji kupunguza idadi ya mifugo kwa kufuga idadi ndogo ya mifugo lakini wenye tija na manufaa zaidi.
Waziri Makamba alipata pia wasaa wa kuwasikiliza wajumbe kadhaa kutoka katika baraza ambao walitilia msisitizo suala la uanzishwaji wa ranchi, kutoa maombi kupatiwa majiko banifu il kupunguza ukataji wa miti huku pia wakipendekeza kutolewa maelekezo ya majengo na nyumba zinazopaswa kujengwa ndani ya hifadhi na zaidi wamesisitiza umuhimu ushirikishwaji wa baraza hilo katika zoezi la uwekaji alama (beacons) kuzunguka eneo la kreta ili kusaidia kuainisha maeneo ya malisho ya mifugo.
Kabla ya kufikia muafaka juu ya suala la Ranchi ya RAMAT waziri Makamba pamoja na Baraza la Wafugaji wamepokea mrejesho kutoka mamlaka zinazohusika katika mradi huo wa ranchi zikiwemo Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro pamoja na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) juu ya kiini cha ucheleweshwaji wa mradi huo. Katika sababu hizo NEMC wameanisha kuwa baada ya kupokea tathmini ya awali ya ukaguzi wa athari kwa mazingira (preliminary Environmental Impact Assesment) waliona umuhimu na kuagiza kufanyika kwa ukaguzi kamili wa tahmini ya athari kwa Mazingira (Full Environmental Impact Assesment) hasa baada ya eneo lililotengwa kuainishwa kuwa ni njia na eneo la mazalia ya wanyama lakini pia uwepo wa madini ya floridi (Flouride) katika maji ya eneo hilo madini ambayo si rafiki kwa mifupa na meno.
Baada ya kupata maelezo ya kina Waziri Makamba aliainisha maagizo kadhaa kuhusiana na hifadhi ya mazingira kwa ujumla katika hifadhi ya Ngorongoro lakini pia kuhusiana na suala la mradi wa ranchi.
Waziri Makamba ameagiza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kuwapa adhabu na kuwaandikia faini wawekezaji wote ambao hawana na cheti cha mazingira au cheti cha ukaguzi wa mazingira.
“Haiwezekani wewe una hoteli tena ndani ya eneo nyeti kama Ngorongoro lakini hauna cheti cha mazingira ninawaagiza NEMC kufika hapa kuwaandikia adhabu na faini wote ambao hawana cheti za mazingira, kila mmoja bila kujali ukubwa wake wale ukubwa wa jina lake. Sheria na mahitaji ya kuwa na cheti imewekwa mwaka 2005 leo miaka 12 baadaye bado unasema upo kwenye mchakato, hakuna kisingizio na hii isiishie kutokuwa na cheti tu, kila mmoja aainishiwe makosa yake na alipe faini”. Alisisitiza Waziri Makamba
Pili Waziri Makamba ametoa miezi 6 kwa kampuni na taasisi zote zinazotumia maji toka ndani ya kreta kuacha kutumia maji hayo na badala yake watumie maji kutoka katika chanzo cha Loksale ambacho hakipo ndani ya eneo kreta.
Pia Waziri Makamba ameitaka Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro ndani ya miezi 6 kuandaa ramani ya mfumo wa kijiografia (Geographical Information System -GIS) itakayoonesha mito,vijito,chemichemi na mitiririko ya maji kwa eneo lote la hifadhi ili kufahamu rasilimali hizo ziko wapi, zinaelekea wapi na hali yake ikoje. hatua hiyo itasadia katika kufahamu taarifa sahihi pamoja na kurahisisha uhifadhi wake.
Akizungumzia suala la uwekaji wa alama za mipaka Waziri Makamba amesema hiyo ni hatua sahihi ya uhifadhi na ili kuhakikisha mifugo inaendelea kunawiri, ambapo ameagiza ndani ya miezi 3 mamlaka iwe imeweka alama hizo na ihakikishe imeweka alama za mipaka (beacons) zilizo wazi zinazofahamika na kuonekana na wafugaji lakini pia katika uwekaji wa alama hizo wadau wote wanaohusika likiwemo Baraza la Wafugaji washirikishwe na kuridhia alama hizo.
Katika kushughulikia tatizo la mimea vamizi iliyovamia na kutawala sehemu kubwa ya eneo la kreta Waziri Makamba amebainisha kwamba sera mpya ya mazingira inayokuja inatambua magugu vamizi kama changamoto mpya na kubwa ya kitaifa na ili kukabiliana na tatizo hilo katika eneo hifadhi lazima utafiti mpya wa kisayansi ufanyike ili kupata mbinu mpya na mbadala za kukabiliana na tatizo hilo .
Waziri ameagiza kuundwa kwa jopo la wataalamu wa sayansi watakaofanya utafiti wakiongozwa na Tume ya Utafiti Tanzania (COSTECH), Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori (TAWIRI), Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi , Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA) pamoja n taasisi husika za kisayansi zinazohusika na tafiti ambapo ameagiza ndani ya miezi 3 kuwe na majibu ya awali ya hatua za kisayansi za kuchukua.
Na mwisho katika kufikia muafaka wa suala la ranchi Waziri Makamba ameagiza wataalamu ndani ya wiki moja kukagua eneo mbadala lililopendekezwa awali na wafugaji na kama ikithibitika kabisa linafaa basi mradi huo uhamie katika eneo hilo mara moja.
Waziri Makamba ameeleza maagizo na maelekezo yote yanayotolewa ni kwa mujibu wa sheria ya mazingira hivyo utekelezaji wake unatakiwa uanze mara moja.
“Bahati nzuri sheria ya Mazingira kifungu cha 12 na 13 inanipa mamlaka ya kutoa maagizo na maelekezo kwa mtu, taasisi, wizara au ofisi yoyote kufanya shughuli yoyote kwa muda maalumu na mtu huyo atalazimika kuyafuata maagizo hayo hivyo tutaandika barua tukinukuu kifungu hicho kwamba maelekezo haya tumetoa kwa mujibu wa mamlaka ya kisheria tuliyo nayo kupitia sheria ya mazingira”. Alifafanua zaidi Waziri Makamba
Waziri Makamba anatarajiwa kukamilisha ziara yake hivi leo ambapo atatembea na kukagua eneo la Ziwa Natron .
Hapa chini ni picha za ziara hiyo;
Tags:
habari