Waziri wa Nishati na Mlezi wa Mkoa wa Shinyanga Kiserikali, Mhe. Deogratius Ndejembi akiongozana na Mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita na viongozi wengine wa serikali kukagua mradi wa barabara ya Kahama–Bulyanhulu Jct–Kakola unaowezeshwa na migodi ya Barrick-Twiga nchini.
Sehemu ya barabara iliyowekwa lami katika Mradi wa Barabara ya Kahama–Bulyanhulu Jct–Kakola, unaowezeshwa na migodi ya Barrick-Twiga nchini Tanzania.
Waziri wa Nishati na Mlezi wa Mkoa wa Shinyanga Kiserikali, Mhe. Deogratius Ndejembi akiongea na waandishi wa habari baada ya kukagua maendeleo ya mradi huo
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita akiongea na waandishi wa habari wakati wa ziara hiyo.
**
Waziri wa Nishati na Mlezi wa Mkoa wa Shinyanga Kiserikali, Mhe. Deogratius Ndejembi, amemtaka Mkandarasi wa ujenzi wa Barabara ya Kahama–Bulyanhulu Jct–Kakola, M/s China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC), kuongeza kasi ya utekelezaji wa mradi huo ili ukamilike kwa wakati na kuwawezesha wananchi kuanza kunufaika na miundombinu hiyo.
Mradi wa ujenzi wa barabara barabara hiyo kwa kiwango cha lami yenye kilomita 73 unatekelezwa kwa uwezeshaji wa migodi ya Barrick-Twiga nchini ya Bulyanhulu na North Mara kwa gharama ya shilingi bilioni 101.2 na umeanza kutekelezwa mwaka juzi kwa usimamizi wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS).
Akiongea baada ya kutembelea barabara hiyo amemtaka mkandarasi kuongeza kasi ili barabara hiyo iweze kumalizika katika muda uliopangwa na kuwaondolea wananchi wanaotumia barabara hiyo kero ya usafiri ambapo amesema kuwa hadi kufikia sasa kilomita 32 kati ya 73 zimekamilishwa kwa kuwekwa lami, huku kazi nyingine za ujenzi zikiendelea katika maeneo mbalimbali ya mradi.
“Sina mashaka na ubora wa kazi inayofanywa na Mkandarasi, lakini anatakiwa kuongeza kasi ili barabara ikamilike kwa wakati. Wananchi wanataka kuona barabara yao inakamilika na kuanza kuitumia,” amesema Mhe. Ndejembi.
Amesisitiza kasi ya utekelezaji inapaswa kuendana na ubora wa kazi, akieleza kuwa kukamilika kwa barabara hiyo kutarahisisha usafirishaji wa watu na bidhaa pamoja na kuchochea shughuli za kiuchumi katika maeneo inayopitia.
Aidha, Mhe. Ndejembi ameuagiza Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Shinyanga kumsimamia kwa karibu Mkandarasi huyo na kuhakikisha kasi ya utekelezaji inaongezeka ili mradi ukamilike ndani ya muda uliopangwa.
Sambamba na hilo, amesisitiza umuhimu wa kuzingatia usalama wa watumiaji wa barabara kwa kuhakikisha barabara zinazojengwa kwa kiwango cha lami zinawekewa taa za barabarani, hususan katika maeneo yenye shughuli nyingi za kijamii na kiuchumi.
Amesema uwekaji wa taa hizo ni sehemu ya maelekezo ya Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi, kwa lengo la kuimarisha usalama na kuwezesha wananchi kutumia barabara kwa usalama zaidi nyakati za usiku.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, amesema Serikali imetoa zaidi ya Shilingi trilioni 2 kwa Mkoa wa Shinyanga kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimkakati na aliahidi kusimamia kwa karibu ujenzi wa Barabara ya Kahama–Bulyanhulu Jct–Kakola ili fedha zilizotolewa na Serikali na maelekezo ya Mhe. Rais yatekelezwe kwa wakati na alitoa pongezi kwa kampuni ya Barrick yenye ubia na Serikali nchini kupitia kampuni ya Twiga kwa kutoa fedha za utekelezaji wa mradi huo.
Akitoa taarifa ya maendeleo ya mradi huo, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Shinyanga, Mhandisi Ntuli Mwaikokesya, amesema ujenzi wa Barabara ya Kahama – Bulyanhulu Jct–Kakola wenye urefu wa kilomita 73 unagharimu Shilingi bilioni 100.6.
Amesema mradi huo ulipangwa kukamilika mwezi Septemba 2026, hata hivyo, kutokana na changamoto mbalimbali zilizojitokeza wakati wa utekelezaji, Mkandarasi ameomba kuongezewa muda wa kukamilisha kazi.
Kwa mujibu wa Mhandisi Mwaikokesya, iwapo muda wa nyongeza utaidhinishwa, mradi huo unatarajiwa kukamilika ifikapo Desemba 2026.
Kukamilika kwa barabara hii ambayo ilianza kujengwa mnamo mwezi Julai mwaka juzi kutafungua fursa za kiuchumi za madini, Kilimo, Misitu na Utalii katika mikoa ya Shinyanga, Geita, Tabora, Kagera na Kigoma.
Pamoja na Barabara hiyo kufungua fursa za kiuchumi za madini, kilimo, misitu na utalii katika mikoa ya Shinyanga, Geita, Tabora, Kagera na Kigoma mara baada ya kukamilika pia barabara hiyo ni muhimu katika shughuli za kiuchumi na kijamii kwa Mkoa wa Shinyanga hususani Manispaa ya Kahama ambako kuna mkusanyiko mkubwa wa Wasafirishaji wa mizigo kutoka bandari kuu ya Tanzania kwenda nchi za jirani za Rwanda na Uganda.
Mkakati endelevu wa kampuni ya Barrick ambayo inafadhili inawezesha ujenzi huo unabainisha kuwa Uchimbaji madini ukifanyika kwa umahiri ni nguvu kubwa ya kuleta maendeleo na Jamii zinazoishi kwenye maeneo ya shughuli zake zikipata mafanikio ni mafanikio yake pia.
0 Comments