DC GEITA AIPONGEZA ESAP KWA UWEKEZAJI KATIKA SEKTA YA MADINI

  

Mkuu wa Wilaya ya Geita, Hashim Komba, ameipongeza Kampuni ya ESAP Mining Services Limited kwa uwekezaji wake katika sekta ya madini kupitia uzinduzi wa mtambo wa kisasa wa MMU (Mobile Manufacturing Unit) wenye uwezo wa tani 15 kwa ajili ya uzalishaji na uchaji wa vilipuzi vinavyotumika katika shughuli za ulipuaji wa miamba migodini.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo uliofanyika Juni 22, 2026 katika eneo la Soko la Dhahabu la Manispaa ya Geita, Komba alisema uwekezaji huo unaendana na dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuwawezesha wazawa kushiriki kikamilifu katika mnyororo wa thamani wa sekta ya madini.

“Kwanza niwapongeze sana ESAP kwa uthubutu huu na hii inaendana sambamba na dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita kuweka mazingira wezeshi kwa wazawa katika mnyororo wa thamani ya madini nchini,” amesema Komba.

Mkurugenzi wa ESAP Mining Services Limited, Mhandisi Yahya Rashid Puyaga, amesema mtambo huo umegharimu zaidi ya shilingi milioni 700 na utasaidia kuongeza ufanisi wa huduma za ulipuaji migodini ili kukidhi mahitaji ya soko.

Kwa upande wake, mwakilishi wa Afisa Madini Mkazi (RMO) Mkoa wa Geita, Adisa, amesema Tume ya Madini itaendelea kutoa ushirikiano kwa kampuni hiyo katika utekelezaji wa majukumu yake, huku Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Geita, Keneth Mwakasitu, akieleza kuwa matumizi ya mtambo huo yatasaidia kuongeza usalama na kupunguza ajali zinazoweza kutokea wakati wa shughuli za ulipuaji wa miamba migodini.

Post a Comment

0 Comments