BARRICK BULYANHULU YALETA FURAHA SEGESE , KAHAMA KWA UJENZI WA SOKO LA KISASA

    Sehemu ya jengo la soko la Kisasa linalojengwa na fedha za Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) zilizotolewa na Barrick Bulyanhulu 

Baada ya Mwenge wa Uhuru kuwasili kwenye ujenzi wa soko la kisasa Segese , Kahama, Shinyanga na kuwashwa ishara ya utekelezaji ya miradi ya wananchi
Baada ya Mwenge wa Uhuru kuwasili kwenye ujenzi wa soko la kisasa Segese , Kahama, Shinyanga na kuwashwa ishara ya utekelezaji ya miradi ya wananchi
Kiongozi wa Mbio za Mwenge kitaifa , Ismail Ali Ussi (kushoto) akimpongeza kwa niaba ya mgodi wa Barrick- Bulyanhulu Kaimu Meneja wa Kitengo cha Mazingira na Uhusiano wa Jamii Zuwena Senkondo baada ya uwekaji wa jiwe la msingi kwenye ujenzi wa soko la kisasa Segese , Kahama, Shinyanga

Na Mwandishi Wetu, Segese, Kahama

Kampuni ya Barrick inazidi kutekeleza dhamira ya kuboresha maisha ya wananchi wanaoishi maeneo yanayozunguka migodi yake ya Bulyanhulu na North Mara ambapo kupitia fedha za uwajibikaji kwa jamii (CSR) imefanikisha ujenzi wa soko la kisasa pamoja na matundu ya vyoo katika kata ya Segese, Wilayani Kahama , Mkoani Shinyanga kwa gharama ya shingi milioni 304.

Hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi iliyoambatana na kutembelewa na mwenge wa Uhuru imefanyika katika soko hilo na kuhudhuriwa na wananchi kutoka vitongoji mbalimbali , viongozi wa Serikali katika msafara wa mwenge na wafanyakazi wa mgodi wa Barrick Bulyanhulu.

Akiongea kwenye hafla hiyo , Kiongozi wa Kitaifa wa mbio za Mwenge, Bw Ismail Ali Ussi amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kujenga mazingira mazuri ya kuwakwamua wananchi kiuchumi mojawapo ni kuwawezesha wafanyabiashara wadogowadogo n awa kati kufanya biashara zao katika mazingira rafiki kama ambavyo limejegwa soko hili la Segese.

Ussi ameupongeza Mgodi wa Barrick Bulyanhulu kwa kuendelea kutekeleza miradi ya maendeleo hususani katika sekta ya elimu ,afya,miundombinu ambayo inazidi kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi na kuboresha maisha ya wananchi.

Aidha amewataka wananchi na wafanyabiashara watakaonufaika na ujenzi wa soko hilo kulilinda na kulitunza ili waweze kufanya biashara zao katika mazingira mazuri na yenye usalama kwani soko hilo linatarajiwa kuwa na miundombinu ya kisasa ,ikiwa ni pamoja na vizimba vya biashara ,vyoo vya kisasa, sehemu ya kuhifadhia mizigo na maeneo ya huduma za kijamii hivyo kuongeza tija katika sekta ya biashara ndani ya Wilaya ya kahama na Mkoa wa Shinyanga kiujumla .

Awali akisoma taarifa ya ujenzi wa soko hilo Afisa Mtendaji wa Kata ya Segese, Evamary Elias amesema ujenzi wa mradi huo umetekelezwa na mkandarasi ayesimamiwa na Mgodi wa Barrick Bulyanhulu kwa kushirikiana na Halmashauri ya Msalala.

Akizungumza kwa niaba ya Mgodi wa Barrick Bulyanhulu Kaimu Meneja Kitengo cha Mazingira na Uhusiano wa Jamii , Zuwena Senkondo amesema kuwa mgodi utaendelea kutekeleza sera, sheria na kanuni zinazoletwa na serikali kama vile maudhui ya ndani (Local Content) na Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) kwa vitendo .

Ameongeza pia pamoja na mambo mengine mradi huo wa soko utasaidia kuboresha Mazingira ya kufanya Biashara na kuongeza kipato kwa wajasiliamali na wafanyabiashara wadogo wanaojihusisha na biashara sokoni hapo.

Baadhi ya Wananchi waliohudhuria katika hafla hiyo walipongeza Serikali na Mgodi wa Barrick Bulyanhulu kwa kuendelea kutekeleza miradi ya maendeleo katika wilaya yao.
Mkuu wa Wilaya ya Kahama , Frank Nkinda akiongea baada ya kuwasili kwa Mwenge wa Uhuru na uwekaji wa jiwe la msingi wa ujenzi wa soko , Segese , Kahama
Viongozi wa mbio za Mwenge, Wilaya na Mgodi katika picha ya pamoja

Post a Comment

0 Comments