BODI YA WAKURUGENZI SHUWASA YAWAPONGEZA WATUMISHI, MENEJIMENTI KWA MAFANIKIO LUKUKI

Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Shinyanga (SHUWASA), Mhandisi Nicholaus Njumbo, amewapongeza watumishi na menejimenti ya SHUWASA kwa utendaji kazi mzuri ulioiwezesha kupata tuzo mbalimbali.

Akizungumza wakati akifungua kikao cha Bodi ya Wakurugenzi na watumishi wa Mamlaka hiyo, kilichofanyika leo tarehe 27 Aprili 2026, amezitaja tuzo zilizopatikana ndani ya mwaka 2026 kuwa ni Tuzo ya utendaji bora kwa Mamlaka za Kanda ya Ziwa iliyotolewa na Taasisi ya Holly Smile; tuzo ya Ufanisi wa Uendeshaji (Operational Efficiency Excellence Award) iliyotolewa na Wizara ya Maji pamoja na pongezi ya mlipaji mzuri wa ada za Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA).

Mhandisi Njumbo, amewapongeza Watumishi na Menejimenti kwa kuwa na ushirikiano na upendo katika utendaji kazi hali iliyopelekea kuwa na mafanikio makubwa katika utendaji kazi wa Mamlaka. 

Aidha amesisitiza kuendelea kuimarisha upendo  miongoni mwa watumishi na baina ya Menejimenti na Watumishi ili kuendelea kudumisha mafanikio yaliyopatikana.

 Amewataka pia kuendelea kudumisha uadilifu na uaminifu kwa Taasisi na wateja kwa ujumla.

“Mafanikio tuliyopata hayawezi kudumu kama hakuna ushirikiano. Mnaposhirikiana hata jambo kubwa linakuwa ni rahisi kulifanyia kazi na kunapokuwa hakuna ushirikiano hata jambo dogo linaweza kuwa kubwa na mkashindwa kulitatua,” amesema Mhandisi Njumbo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi an Usafi wa Mazingira Shinyanga (SHUWASA), Mhandisi Yusuph Katopola, amesema Mamlaka hiyo imeendelea kutekeleza jukumu lake kuu la kuhakikisha upatikanaji wa huduma ya majisafi ndani ya  eneo la huduma inapatikana kwa wastani wa saa 23.

Amesema SHUWASA imeendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo mradi wa majisafi na usafi wa mazingira Shinyanga unaotekelezwa kwa mkopo nafuu kutoka Benki ya Maendeleo ya Ufaransa (AFD), kwa Ushirikiano na Serikali ya Tanzania.

Amesema tayari Mkataba na Mkandarasi wa Ujenzi umeshasainiwa na Mkandarasi anaendelea kujipanga kuanza kazi.

Aidha amesema pia wanaendelea na mradi wa usafi wa mazingira  wa IFF-OBA na kwamba tayari gari la majitaka limeshanunuliwa na lipo tayari kuanza kazi wakati wowote.

Ameongeza kuwa SHUWASA imekuwa ikitekeleza maelekezo ya Serikali juu ya matumizi ya mifumo ya TEHAMA.

Post a Comment

0 Comments