CRDB YAKABIDHI MEZA NA VITI SHULE YA SEKONDARI NGURUKA

   

Benki ya CRDB imeendelea kuonesha uzalendo na moyo wa kusaidia jamii kwa vitendo kupitia kampeni yake ya Keti Jifunze, kwa kutoa msaada wa meza na viti kwa wanafunzi wa shule ya sekondari Nguruka, Wilaya ya Uvinza, mkoani Kigoma.

Katika hafla iliyofanyika jana Julai 22, 2025, CRDB ilikabidhi meza 40 na viti 40, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi wa shule hiyo.

Madawati hayo yalikabidhiwa rasmi na Meneja wa Kanda ya Magharibi wa CRDB, CPB Jumanne Wambura Wagana ambaye amesema meza na viti hivyo ni sehemu ya mpango wa benki hiyo wa kuchochea maendeleo ya sekta ya elimu kupitia kampeni ya Keti Jifunze, ambayo inalenga kuhakikisha kila mwanafunzi anakaa kwenye dawati akiwa katika mazingira bora ya kujifunzia.

"Kupitia kampeni ya Keti Jifunze, tumejipanga kuendelea kutoa mchango wetu katika kuinua elimu ya taifa. Tunaamini kwamba mazingira bora ya kusomea yanachangia kwa kiasi kikubwa ufaulu wa wanafunzi. Ndiyo maana CRDB tunaona ni wajibu wetu kushiriki kwa vitendo kusaidia shule zenye uhitaji mkubwa wa madawati kama hii ya Nguruka," amesema Wagana.

Mgeni rasmi katika hafla hiyo alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Uvinza, Mheshimiwa Dinah Mathamani, ambaye amepokea msaada huo kwa niaba ya serikali na kuwapongeza CRDB kwa kuonesha moyo wa kizalendo na kuwekeza kwenye elimu.

"Hili ni jambo la kuigwa. CRDB mmeonesha kuwa mko karibu na jamii. Naomba wadau wengine nao wajitokeze kusaidia sekta ya elimu kama sehemu ya kuchochea maendeleo ya Taifa," amesema Mhe. Mathamani.

Kampeni ya Keti Jifunze imekuwa chachu ya kuboresha miundombinu ya shule mbalimbali nchini kwa kushirikisha sekta binafsi katika kuunga mkono jitihada za serikali kuinua elimu.
Meneja wa CRDB Kanda ya  Magharibi CPB Jumanne Wambura  Wagana (kulia) akikabidhi meza Mkuu wa Wilaya ya Uvinza Mhe. Dinah Mathamani
Meneja wa CRDB Kanda ya Magharibi CPB Jumanne Wambura Wagana akitoa salamu kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Benki  ya CRDB.
Meneja wa Tawi la Nguruka   Nassoro Mogaeka akizungumza wakati wa Makabidhiano

Post a Comment

0 Comments