
Takriban watu 18 wamepoteza maisha na wengine 19 kujeruhiwa kutokana na moto mkubwa uliozuka Mashariki mwa Korea Kusini, huku zaidi ya watu 27,000 wakilazimika kuhama makazi yao baada ya mamia ya majengo kuharibiwa.
Maeneo kadhaa ya urithi wa kitamaduni pia yameathiriwa, ikiwa ni pamoja na hekalu la Wabuddha la umri wa miaka 1,300 ambalo liliharibiwa, hukui hazina nyingine za kitaifa zikihamishwa.
Maelfu ya maafisa wa zima moto na wanajeshi wapatao 5,000 wamepelekwa kudhibiti moto huo, zikiwemo helikopta kutoka kwa jeshi la Marekani lililoko Korea.
Katika kaunti ya Uiseong, ambapo moto ulianza, watu 14 wamefariki dunia, huku wengine wanne wakiripotiwa kufariki kutokana na moto mwingine katika kaunti ya Sancheong. Wengi wa waathirika ni watu wa umri wa miaka 60 na 70.
Rais wa muda, Han Duck-soo, amesema wanatumia rasilimali zote zinazopatikana, ikiwa ni pamoja na msaada kutoka jeshi la Marekani ili kukabiliana na moto huu mkubwa, huku hali ya hewa na upepo mkali vinachangia ugumu wa kudhibiti moto huu.
Maafisa wa usalama wanahofia kuwa mabadiliko ya tabianchi yanaweza kuchochea mara kwa mara kwa matukio ya moto wa misitu kama huu huku mamlaka zikiendelea kuchunguza chanzo halisi cha moto huo.
0 Comments