DC MTATIRO AONGOZA UTOAJI TUZO USIKU WA WADAU SHUPAVU SHINYANGA 2025, AIPONGEZA HOLYSMILE!

 

Na Mwandishi wetu - Malunde 1 blog

Taasisi ya HolySmile imetoa tuzo kwa  wadau mbalimbali wanaofanya vizuri katika utoaji wa huduma na utekelezaji wa miradi yenye manufaa kwa jamii ya Shinyanga katika kutoa hamasa kwa taasisi na kuchagiza uwajibikaji.

Hafla hiyo imefanyika Februari 1, 2025 katika ukumbi wa Makindo uliopo manispaa ya Shinyanga ikihudhuriwa na viongozi wa serikali, wawakilishi wa mashirika na taasisi, na wadau mbalimbali wa maendeleo.

Akizungumza kwenye hafla hiyo ya utoaji tuzo, mgeni rasmi Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Wakili Julius Mtatiro ameipongeza Taasisi ya HolySmile kwa juhudi zake za kutambua na kuthamini mchango wa taasisi na mashirika binafsi katika maendeleo ya jamii na utoaji huduma na kusisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya sekta binafsi na serikali katika kutatua changamoto za kijamii.

Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Wakili Julius Mtatiro

"Nitoe shukurani za dhati kwa HolySmile kwa kuandaa tuzo hizi, kwa taasisi na na mashirika yanayofanya vizuri kwenye sekta mbalimbali ndani ya wilaya yetu, Mashirika na taasisi  zinayopata tuzo leo yameonyesha mfano wa kuigwa katika utoaji wa huduma bora kwa jamii, ni matumaini yangu kuwa haya siyo mafanikio ya mwisho, bali ni chachu ya kufanya zaidi kwa ustawi wa wananchi wa Shinyanga," amesema DC Wakili Mtatiro.

Aidha Wakili Mtatiro ametoa rai kwa wadau na wawekezaji kuendelea kuwekeza ndani ya wilaya ya Shinyanga ili kuongeza fursa kwa wananchi huku akibainisha jitihada zinazofanywa na serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ikiwemo ujenzi wa treni ya umeme pamoja na uwanja wa ndege wa Ibadakuli uliopo manispaa ya Shinyanga.

"Nchi yetu inaendelea kupata maendeleo kwa kasi sana ikiwemo mkoa wa Shinyanga ambapo ni pamoja na ujenzi wa uwanja wa ndege, treni ya umeme maendeleo haya yanayoendelea kutokana na juhudi kubwa zinazofanywa na serikali ya awamu ya sita niwaombe wadau tuendelee kuwekeza Shinyanga ili kuongeza fursa kwa wananchi wa Wilaya hii na Mkoa wa ujumla", ameongeza DC Wakili Mtatiro.

Tuzo zilitolewa kwa mashirika na taasisi zilizojipambanua katika sekta mbalimbali kama elimu, afya, mazingira, na maendeleo ya vijana.

Mkurugenzi wa Taasisi ya HolySmile, Arnold Bweichum amesema kuwa tuzo hizo ni sehemu ya mkakati wa kutambua mchango unaotolewa na  taasisi mbalimbali na kuhamasisha ubora na uwajibikaji kwa mashirika na taasisi zinazojituma kwa dhati kuleta maendeleo.

Mkurugenzi wa Taasisi ya HolySmile, Arnold Bweichum

              













Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 753 336 000 au +255 625 917 902

Masengwa blog Ipo Play Store…Download HAPA ,Uwe unapata habari zote kwa urahisi zaidi
 Bofya Hapa

No comments:

Powered by Blogger.