WASHIRIKA WENZAKE NA SABAYA WAACHIWA



WASHIRIKA wanne wa aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya katika kesi ya uhujumu uchumi na rushwa, wameachiwa huru baada ya kusota mahabusu kwa siku 458.

Katika Gereza Kuu la Karanga Moshi, washtakiwa hao wamesota mahabusu kwa siku 95 na katika Gereza la Kisongo lililoko mkoani Arusha, walikaa kwa siku 363.

Walioachiwa huru baada ya kuingia makubaliano (Plea Bargaining) na Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP), ni mshtakiwa wa pili, Sylvester Nyegu, John Aweyo, Nathan Msuya na Antero Assey.

Ombi la kuwaachia huru washtakiwa hao liliwasilishwa jana jioni Septemba 6 na Mkurugenzi Msaidizi wa Kurugenzi ya Kutenganisha Upelelezi na Mashtaka kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP), Maternus Marandu.

Kesi hiyo ilikuwa inasikilizwa na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Salome Mshasha anayesikiliza kesi hiyo Namba 2 ya Mwaka 2022 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi.

Akiwa mahakamani hapo, Mkurugenzi huyo kutoka Ofisi ya DPP, alidai kuwa washtakiwa waliandika barua ya kuomba kufanya makubaliano na DPP Agosti 3 mwaka huu.

"Nimeamua kuwaondoa katika shtaka hilo la uhujumu uchumi, namba 2 la mwaka 2022. Tunaomba mahakama hii iwaondolee mashtaka mshtakiwa wa pili, tatu, nne na tano.

"Chini ya kifungu cha 91 (1) cha Sheria ya Mwendendo wa Makosa ya Jinai kama ilivyofanyiwa Marejeo Mwaka 2002."

Washtakiwa hao wameamriwa na Mahakama hiyo, kulipa fidia ya Sh.milioni moja kwa kila mtu na kulipa faini ya Sh.50,000 kwa kila kosa.

Kabla ya kuwaachia huru, Hakimu, Salome Mshasha, alisema amewatia hatiani kwa makosa mawili waliyoshtakiwa nayo likiwamo la kimsaidia Lengai Ole Sabaya kujipatia fedha.

"Kwa kuwa hamna pingamizi, nimewaondolea mashtaka ya uhujumu uchumi, isipokuwa mshtakiwa wa kwanza ambaye atakuja mahakamani Septemba 12 na kwa sasa yuko chini ya uangalizi wa magereza,"alisema Hakimu Mshasha

Imeandikwa na Godfrey Mushi na Mary Mosha - IPP MEDIA

Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 753 336 000 au +255 625 917 902

Masengwa blog Ipo Play Store…Download HAPA ,Uwe unapata habari zote kwa urahisi zaidi
 Bofya Hapa

No comments:

Powered by Blogger.