ONYANGO ACHACHAMAA, AISHITAKI SIMBA TFF

STAA aliyerejeshwa kikosini na Yanga dakika za lalasalama za dirisha la usajili, Tuisila Kisinda anatarajiwa kutua nchini muda wowote, lakini beki kisiki wa Simba, Joash Onyango ameibua jipya.

Mwanaspoti limejiridhisha kwamba Mkenya huyo amepeleka rasmi barua Shirikisho la Soka la Tanzania(TFF) akiomba kutengua mkataba wake na Simba kwa kile kilichoelezwea kwamba haoni kesho yake kwenye kikosi cha kwanza cha Zoran Maki.

Mitandaoni mashabiki wamekuwa wakikejeli kwa kumhusisha na ujio wa Kisinda Yanga ingawa Mwanaspoti linajua kwamba Onyango analazimisha kuondoka Simba baada ya kuona kuna ugumu wa kupata namba mbele ya Mohammed Outtara ambaye ni chaguo la Kocha. Lakini Simba ingawa wako kimya, wameshtukia kwamba Onyango anafosi kuondoka baada ya kupata ofa ya kimyakimya kutoka kwa vigogo wa Singida Big Stars walioanza msimu kwa moto.

Kisinda yeye anarejea Jangwani akitokea RS Berkane ya Morocco alikocheza msimu uliopita baada ya kuuzwa na Yanga mambo yakazidi unga.

Habari za uhakika zinasema kwamba Yanga wameshamtumia tiketi Kisinda kimyakimya na wanataka aje haraka aanze mazoezi kujiweka sawa na mechi zinazoikabili kwenye michuano ya ndani na nje. Yanga chini ya Kocha Mohammed Nabi wamemshusha staa huyo ili kuongeza makali kwenye ushambuliaji ambako nako kuna vichwa vingi.

Ujio wa Kisinda ndani ya Yanga umechomoa jina la Lazarous Kambole ambaye atalazimika kusubiri maelekezo mengine ya Nabi jukwaani kwani hawezi kutumika popote na hayupo kwenye usajili huu.

ONYANGO

Kigogo mmoja ndani ya Simba amesisitiza kwamba hawana mpango wa kuachana na Onyango licha ya yeye kuwaambia kwamba anataka kuondoka na anapambana na wanasheria kupata uhalali wa kuondoka kwa gharama yoyote ambayo Simba hawako tayari kuipokea.

Beki huyo kisiki aliyeunda ukuta wa chuma msimu uliopita akiwa na Henock Inonga hakuwa na Simba iliyokuwa Sudan kwa mechi za kirafiki.

Inaelezwa kwamba mbali ya kukutana na Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi, Salim Abdallah ‘Try Again’ na kudaiwa kumalizana maisha na kila kitu lakini nyota huyo ametinga TFF akiomba wawakomalie Simba wamvunjie mkataba wake wa miaka miwili aliosaini mwishoni mwa msimu uliopita. Moja ya sababu aliyoeleza ni kushindwa kutimiziwa mahitaji yake ya kimkataba. Licha ya Onyango kutopokea simu yake lakini Mwanasheria wa TFF, Herman Kidifu alisema: “Baada ya kukutana na kufanya kikao ndio nitaelewa na kufahamu kama Onyango ameleta barua kuhusu jambo hilo, ila kwa sasa sifahamu lolote.”

Usajili wa Ligi Kuu Bara umefungwa Agosti 31 na Klabu zote ziliruhusiwa kusajili wachezaji wa kigeni wasiozidi 12.

Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 753 336 000 au +255 625 917 902

Masengwa blog Ipo Play Store…Download HAPA ,Uwe unapata habari zote kwa urahisi zaidi
 Bofya Hapa

No comments:

Powered by Blogger.