RASMI CHAMA AOMBA KURUDI BONGO, AITAJA TIMU ANAYOTAKA KUJA KUCHEZEA
KUFUATIA ugumu wa maisha anaokutana nao katika timu ya RSB Berkane ya nchini Morocco, kiungo wa zamani wa Simba, raia wa Zambia, Clatous Chota Chama, sasa rasmi ameomba kurudi kwa mabosi wake wa zamani Simba.
Chama aliachana na Simba, mwishoni mwa msimu ulipita akijiunga katika klabu ya RSB Berkane ya Morocco kwa mkataba wa miaka mitatu, akiwa sambamba na winga wa zamani wa Yanga, raia wa DR Congo, Tuisila Kisinda, baada ya kupendekezwa na kocha wao Florent Ibenge aliyekuwa As Vita msimu uliopita.
Chanzo chetu kutoka ndani ya Simba, kimeliambia Championi Ijumaa kwamba, hivi karibuni Chama alimpigia simu, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’, akimuomba wamfanyie mchakato wa kumrejesha Simba, kwani hana furaha ndani ya klabu ya RSB Berkane.
“Nasikia watani huko wanazidi kutamba eti wanaweza kumleta Chama msimu ujao, jambo ambalo siyo kweli kabisa, kwani mimi kama mmoja wa watu wa karibu na uongozi wa Simba, nilibahatika kusikia maongezi ya Mwenyekiti wetu na Chama, akiomba wamfanyie mpango wa kuvunja mkataba ili arejee kikosini.
“Maombi ya Chama yaliendana na malalamiko ya kukosa furaha ndani ya muda mfupi katika klabu hiyo, huku akilalama kushindwa kuipeleka familia yake huko, jambo ambalo linamfanya ahitaji zaidi kurejea Simba ili awe karibu na familia yake kwani nchi yetu ina amani kubwa kuliko huko na kwamba hakuna tatizo kubwa la maambukizi ya covid.
“Chama alimuomba Try Again amsaidie hilo kufuatia mkataba wake na RSB Berkane, unamruhusu kurejea Simba tu endapo atahitaji kuvunja mkataba na kucheza Afrika tena, zaidi ya hapo haruhusiwi kwani Simba wana asilimia 60 za kumrejesha na si timu nyingine kama ilivyovuma kuwa anakuja Yanga.
“Kimsingi baada ya chama kutoa maombi hayo, Try Again alimpigia Mohamed Dewji ‘Mo’ akimuombea Chama, lakini Mo alimwambia Try Again, amtafute CEO Barabra Gonzalez ili wajadiliana kama uwezekano huo upo, jambo ambalo waliahidi kulikalia kikao baada ya kumaliza machakato wa kocha.
“Kwa maana hiyo sasa ni rasmi Simba tutamrejesha Chama tena na hakuna klabu nyingine yoyote nchini yenye uwezo wa kumpata Chama hapa nchini au Afrika, kwani mkataba wake una masharti ya kutoruhusiwa kucheza Afrika tena,” kilisema chanzo hicho.
Kwenye mahojiano maalum ya Championi na Mwenyekiti wa Simba, Murtaza Ally Mangungu naye alikiri wazi kuwa: Hakuna timu yoyote nchini zaidi ya Simba inayoweza kumrejesha Chama, hivyo wanaopiga kelele waache waendelee na kelele zao,” alisema Mangungu.
Lakini pia hivi karibuni Chama mwenyewe alikaririwa akizungumza na mashabiki zake mubashara kupitia ukurasa wake katika mtandao wa Instagram ambapo alisema, yupo tayari kurejea Simba muda wowote endapo akihitajika kuja kutoa msaada wake.
Kuhusu ishu ya Chama na mambo mengine mengi ya Simba, Mangungu amezungumza katika mahojiano Exclusive na gazeti hili katika ukurasa wa 10 na 11.
MUSA MATEJA, Dar es Salaam
Masengwa blog Ipo Play Store…Download HAPA ,Uwe unapata habari zote kwa urahisi zaidi
No comments: