MADIWANI WENGINE WAWILI WA CHADEMA WATIMKIA CCM
Madiwani wawili wa Chadema katika Halmashauri ya Manispaa ya Iringa wamejiuzulu nyadhifa zao na kuhamia CCM.
Wakati diwani wa Ruaha, Tandesy Sanga akitangaza uamuzi huo leo Jumatano Januari 3,2018 jijini Dar es Salaam; mwenzake wa Kwakilosa, Joseph Ryata ametangaza uamuzi huo mjini Iringa.
Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 Chadema ilishinda ubunge wa Iringa Mjini na kupata madiwani katika kata 14 kati ya 18, hivyo kuongoza Halmashauri ya Manispaa ya Iringa kwa mara ya kwanza tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa nchini mwaka 1992.
Ryata aliyewahi kuwa naibu meya wa manispaa hiyo ametangaza uamuzi huo leo alipozungumza na waandishi wa habari, na kuonyesha barua aliyoiwasilisha kwa meya na mkurugenzi mtendaji wa halmashauri Desemba 22,2017.
Chadema imeshapoteza madiwani sita akiwemo wa kata ya Kitwiru, Baraka Kimata aliyejiuzulu na kujiunga CCM ambako alishinda tena katika uchaguzi mdogo uliofanyika Novemba 26,2017.
Madiwani wengine waliojiuzulu na kujiunga na CCM ni aliyekuwa wa kata ya Kihesa, Edger Mgimwa; wa viti maalumu Leah Mleleu na Husna Daudi.
Ryata akitangaza kujiuzulu amedai hajaridhishwa na uendeshaji wa Chadema na wa baraza la madiwani la Halmashauri y Manispaa ya Iringa.
Akiwa ameambatana na Mgimwa alidai amekwepa vitendo vya uongozi wa kidikteta ndani ya Chadema.
Jijini Dar es Salaam, Sanga amesema uamuzi wake wa kujiuzulu unatokana na kuunga mkono jitihada za maendeleo za Rais John Magufuli.
"Huwezi kumsifia Rais wala utendaji wake ukiwa nje ya chama chake, binafsi nimeshaonywa kwenye vikao hata kutishiwa kuvuliwa uanachama kwa sababu hiyo," amesema.
Sanga amesema ilikuwa vigumu kwake kuhudhuria ziara za viongozi wa Serikali kwa kuonekana msaliti hata kama nia yake ilikuwa ya kiuongozi.
"Kwa hiyo bila kutumwa, kushinikizwa wala kununuliwa na yeyote kama inavyodaiwa na baadhi ya watu najiunga na chama kilicho taasisi, si cha mtu mmoja," amesema.
Sanga amesema jingine lililomsukuma kuhama ni tabia ya baadhi ya viongozi kuwa na nguvu kuliko chama chenyewe tofauti na fikra zake wakati alipojiunga Chadema.
NaTumaini Msowoya na Geofrey Nyang’oro, Mwananchi
Masengwa blog Ipo Play Store…Download HAPA ,Uwe unapata habari zote kwa urahisi zaidi
No comments: