YAFAHAMU HAPA MATAMKO YA VIONGOZI WAKUBWA YALIYOTIKISA KWA MWAKA 2017


Ingawa mwaka 2017 nayoyoma, yapo mambo kadhaa ambayo bado yataendelea kubaki katika kumbukumbu za watu.


Miongoni mwa hayo ni matamko kadhaa yaliyotolewa yaliyokuwa yamebeba ujumbe uliopokewa tofauti na wananchi na baadhi yalibatilishwa ama na Rais John Magufuli, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, mawaziri au wakuu wa mikoa.

Miongoni mwa matamko hayo ni kuzuiwa kufunga ndoa mpaka kwa cheti cha kuzaliwa, msichana asiyemaliza kidato cha nne hakuna kuolewa, marufuku mwanafunzi mjamzito kuendelea na masomo, zuio la magari yenye tinted kutembea barabarani.

Agizo la Waziri Majaliwa Mkuu Novemba 9, la kuwaonya mawaziri na viongozi wengine wa umma kuacha kutoa matamko ya aina hiyo kwani yanasababisha mikanganyiko serikalini, lilipoza moto wa viongozi hao.

Waziri Mkuu alitoa ufafanuzi huo wakati akifunga kikao kazi cha mawaziri kilichofanyika mjini Dodoma. Aliwataka kujiridhisha kwanza kama jambo wanalotaka kulitolea tamko halitakuwa na athari za kibajeti na kisera na kama lipo katika bajeti za wizara zao huku akiwataka kuzingatia maadili ya uongozi ili kuithibitishia jamii kuwa Rais John Magufuli aliwateua kutokana na uadilifu na uwezo wao kiutendaji.

Ndoa mpaka cheti cha kuzaliwa

Machi 16, Dk Harrison Mwakyembe, akiwa Waziri wa Katiba na Sheria, alikaririwa akisema mwananchi ambaye hatakuwa na cheti cha kuzaliwa, hataruhusiwa kufunga ndoa.

Alipiga marufuku watu kufunga ndoa ya aina yoyote, iwe ya Serikali, kimila au ya dini bila kuwa na cheti cha kuzaliwa, agizo ambalo alitaka lianze kutekelewa kuanzia Mei Mosi.

Lakini siku moja baadaye, Rais Magufuli alifuta agizo hilo akisema halitekelezeki.

“Dk Magufuli amesema Serikali haiwezi kuruhusu masharti hayo kutumika, kwa kuwa yatawanyima haki ya kuoa na kuolewa Watanzania wengi ambao hawana vyeti vya kuzaliwa, huku utaratibu wa kupata vyeti hivyo ukiwa bado unakabiliwa na changamoto nyingi kwa wanaohitaji,” ilieleza taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa.

Asiyemaliza kidato cha nne hatoolewa
Novemba, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Joseph Kakunda aliwataka viongozi wa dini nchini kujihadhari kuwaozesha wasichana ambao hawajamaliza kidato cha nne akisema wanashindwa kumaliza masomo kwa sababu ya mimba au kuozeshwa jambo ambalo limeendelea kuisumbua Serikali katika juhudi zake za kuhakikisha wanaendelea na masomo.

“Haiwezekani mtu anamkamata mtuhumiwa anatakatisha Sh1 milioni anakosa dhamana, halafu mtu anampa mimba mwanafunzi kisha anapata dhamana siku hiyohiyo, hapa tutakuwa hatuthamini maisha ya mtoto wa kike.”

“Tunapoelekea watoto wote watasoma shule kuanzia darasa la kwanza mpaka form four, sera yetu mpya ambayo tutai – adopt hivi karibuni inasema mwaka mmoja wa shule ya awali, miaka sita shule ya msingi na miaka minne ya sekondari ni lazima. Kwa hiyo tunapoelekea, ili mtoto aolewe lazima aonyeshe cheti cha kumaliza shule ya sekondari... Ndiyo... ili uolewe uonyeshe living certificate au vinginevyo tujue wewe hujasoma kabisa ili tuwahoji wazazi..”

Hata hivyo, siku moja baada ya kauli hiyo kusambaa katika mitandao ya kijamii, Serikali ilikanusha. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi ), Selemani Jafo alisema habari hizo kuwa msichana atatakiwa kuwa na cheti cha kidato cha nne kabla ya kuruhusiwa kufunga ndoa ni za upotoshaji.

Marufuku magari yenye ‘tinted’

Novemba hiyohiyo, aliyekuwa Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda maalumu ya Dar es Salaam, Lucas Mkondya alipiga marufuku vioo vya magari kuwekewa tinted.
Alisema imebainika kuwa magari hayo hutumika kwa ujambazi na uvunjifu mwingine wa maadili ikiwamo ngono na kwamba Jeshi la Polisi litafanya operesheni maalumu ya kukamata magari hayo kwa kuwa yanavunja sheria za barabarani.

Hata hivyo, siku moja baadaye, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda alibatilisha tamko hilo akisema kuna mambo ya msingi yanayosababisha madereva kuweka vioo vya tinted hivyo huwezi kupiga marufuku bila kujiridhisha.

Alisema wapo wanaoweka tinted kwa sababu za kiusalama hasa wanawake wanaoogopa kuvamiwa wawapo peke yao lakini pia wengine wanabeba fedha nyingi hivyo kuwakataza watu kuweka si sawa.

Maoni ya wadau

Katika maoni yake kuhusu matamko hayo, Profesa Benson Bana wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), alisema viongozi wanapaswa kuwa werevu hasa kipindi hiki cha vyama vingi ambacho Serikali inafanya kazi na upinzani kama paka na panya.

“Unapokuwa serikalini wewe ni panya na upinzani ni paka, hivyo mara zote kuwindana ni jambo la kawaida cha msingi ni kuwa makini na matamshi yako,” alisema.
Alisema kwa sasa mawaziri wengi ni wageni hivyo Waziri Mkuu akiwa kiongozi wao ni lazima ahakikishe anasimamia wanasema nini, wakati gani na yataleta madhara gani kwa jamii.”

Alitoa mfano wa kauli iliyotolewa na waziri mmoja kwamba hata vyerehani vinne ni kiwanda, akisema haikupaswa kutolewa na waziri.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Helen Kijo Bisimba alisema kitendo cha viongozi kutoa matamko bila kufuata taratibu hakiakisi utawala bora.

Alisema Waziri Mkuu ana jukumu la kuhakikisha anawarejesha katika mstari mawaziri na viongozi wote wenye tabia za kutoa matamko yasiyotekelezeka kwa kuwa ni kiongozi wa mawaziri hivyo ni vizuri kuwarudisha katika mstari ili kuhakikisha hawatoi matamko yatakayoiweka Serikali njia panda.

“Kuna waziri aliwahi kusema ili kuolewa ni lazima mtoto amalize kidato cha nne, hivi wasiofika ndiyo wasiolewe?” alihoji.

“Wengine wanasema watafanya mambo makubwa ya maendeleo ilhali wanajua kabisa hayatekelezeki, ni vizuri kusema kitu unachokiamini na unachoweza kukifanya.”

Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema) Peter Msigwa alisema viongozi wengi wa juu wamekuwa na tabia ya kutoa matamko bila kujua madhara yake.
Alisema viongozi wanapaswa kujihoji kabla ya kutoa matamko yanayoweza kuwachanganya wananchi hasa katika utekelezaji wake na kujikuta wakishindwa kufanya hivyo.

“Kiongozi lazima uongozwe na sheria na kanuni lakini busara zaidi inahitajika katika kuamua masuala mbalimbali, wananchi sasa siyo wajinga wanaelewa mambo,” alisema.

Hata hivyo, Msigwa ambaye ni mmoja wa makamishna wa Bunge alisema kitendo cha kutoa matamko ambayo hayatekelezeki mfumo ulioanza tangu zamani.

“Cha msingi ni kuhakikisha viongozi wanawajibika na matamko yao na siyo kutoa matamko yasiyotekelezeka kwa maana hali hiyo haijaanza leo wala jana,” alisema

Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 753 336 000 au +255 625 917 902

Masengwa blog Ipo Play Store…Download HAPA ,Uwe unapata habari zote kwa urahisi zaidi
 Bofya Hapa

No comments:

Powered by Blogger.