POLISI DAR WAACHANA NA DK. LOUIS SHIKA

Jeshi la Polisi limeamua kuachana na Dk Louis Shika, yule msomi aliyefika bei ya kununua majengo matatu ya mfanyabiashara Said Lugumi.

Novemba 9, kampuni ya udalali ya Yono kwa niaba ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) iliendesha mnada wa nyumba mbili za Lugumi zilizopo Mbweni JKT na moja Upanga jijini Dar es Salaam ambazo zote Dk Shika alifikia bei ya kuzinunua kwa Sh3.2 bilioni.

Hata hivyo, msomi huyo wa taaluma ya udaktari kutoka Urusi alishindwa kulipa asilimia 25, kwa mujibu wa taratibu za minada na hivyo kukamatwa kisha kushikiliwa na jeshi hilo kwa siku kadhaa kabla ya kuachiwa kwa kujidhamini mwenyewe.

Akizungumza na gazeti hili jana, kamanda wa polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa alisema kesi waliyomfungulia Dk Shika ya kuharibu mnada hawataendelea nayo kwa kuwa nyumba za Lugumi alizoahidi kuzinunua zote zipo.

Mambosasa alisema kesi hiyo haina mashiko kwa kuwa msomi huyo hajatia hasara yoyote.

Alisema Dk Shika alikuwa akitamba kuwa ana fedha kumbe uwezo wake ni mdogo na kusababisha kushindwa kulipa asilimia 25 kwa kila nyumba.

‘‘Dk Shika ni wa kumuonea huruma hana kitu, tulisema tunamchunguza na tutampeleka mahakamani lakini tumeona kesi yake haina mashiko, ndiyo maana hatuendelei nayo,” alisema Mambosasa.

Katika mnada huo msomi huyo aliyejizolea umaarufu baada ya tukio hilo alifikia bei kununua nyumba za Mbweni JKT kwa Sh900 milioni na nyingine Sh1.1 bilioni, huku ya Upanga alifika bei ya Sh1.2 bilioni.

Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 753 336 000 au +255 625 917 902

Masengwa blog Ipo Play Store…Download HAPA ,Uwe unapata habari zote kwa urahisi zaidi
 Bofya Hapa

No comments:

Powered by Blogger.