HII MPYA!!! AJIB AFANYA JAMBO JIPYA KWA CANNAVARO

UKISEMA Ibrahim Ajib ni jeuri utakuwa hujakosea, kutokana na kile alichokifanya mazoezini jana baada ya kuwagawia fedha wachezaji wenzake, zikiwa ni zile alizozawadiwa na mashabiki kwa kung’ara kwenye mechi za timu hiyo za Ligi Kuu Tanzania Bara.

Mara baada ya mazoezi yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam, Ajib aliona ni vema kuwagawia wenzake Sh 400,000 kama sehemu ya shukrani kwani nao walichangia mafanikio yake kwa kuibuka nyota wa mchezo katika mechi mbili dhidi ya Kagera Sugar na Stand United.

Ajib alimkabidhi fedha hizo nahodha wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, ambapo beki huyo alimshukuru mno nyota wao huyo mpya aliyetua Jangwani msimu huu akitokea Simba.

“Kwa niaba ya wachezaji wenzangu napenda nimshukuru sana Ajib kwa moyo wake wa upendo, hili si jambo dogo kutoa fedha kama hizi tugawane, huu ni moyo wa kipekee sana ambao anao jamaa na Mungu atamzidishia,” alisema Cannavaro.

Cannavaro alisema fedha hizo walizopewa na Ajib watazitumia kama kichocheo cha kufanya vizuri katika michezo ya Ligi Kuu Bara inayokuja wakianzia na Singida United Jumamosi kwenye Uwanja wa Namfua, Singida.

Tangu atue Yanga, Ajib ameonyesha kiwango kizuri kiasi cha mashabiki wa timu hiyo kuamua kumzawadia fedha kama sehemu ya kuthamini mchango wake, lakini pia kumfanya apambane zaidi na zaidi.

Mbali ya Ajib, wachezaji wengine wa Yanga waliowahi kuzawadiwa fedha na mashabiki kwa kung’ara katika mechi za timu hiyo ni Kabamba Tshishimbi, Youthe Rostand na Kelvin Yondani.

Katika hatua nyingine, benchi la ufundi la timu hiyo jana lilionekana kutilia mkazo zoezi la umaliziaji kwa washambuliaji wa timu hiyo kabla ya kuwavaa Singida United wikiendi hii.

Katika mazoezi hayo, Kocha Mkuu wa Yanga, George Lwandamina, aliwapa nyota wake mbinu za namna ya kupachika mabao yatokanayo na krosi kutoka upande wa kulia na kushoto.

Mawinga Juma Mahadh, Said Barhuan na Said Mussa, ndio waliopewa kazi za kupiga krosi za upande wa kulia, huku kushoto kukiwa na Geoffrey Mwashiuya na Emmanuel Martin.

Katika zoezi hilo, mshambuliaji Obrey Chirwa aling’ara vilivyo baada ya kuwatungua makipa Youthe Rostand na Ramadhan Kabwili.

Goli la kwanza Chirwa alilifunga kutokana na krosi ya Mwashiuya huku lile la pili akilifunga baada ya kuunganisha krosi ya Juma Abdul.

Wakati huo huo, kikosi cha wachezaji 24 wa timu hiyo kinatarajia kuondoka alfajiri ya leo kuelekea Singida kucheza na Singida United Jumamosi, ukiwa ni mchezo wa raundi ya tisa ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.

Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 753 336 000 au +255 625 917 902

Masengwa blog Ipo Play Store…Download HAPA ,Uwe unapata habari zote kwa urahisi zaidi
 Bofya Hapa
Powered by Blogger.