CCM YAMUWAHI NYALANDU BUNGENI

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimeliandikia Bunge la Tanzania kuliarifu kwamba Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu amepoteza sifa za kuwa mwanachama wake, siku chache baada ya mbunge huyo kutangaza kuwa amejiuzulu nyadhifa zake zote katika chama tawala.

Kwa hatua hiyo, Ofisi ya Spika wa Bunge la Tanzania, Nyalandu aliyewahi kuwa Waziri katika Serikali ya Awamu ya Nne, amepoteza sifa ya kuwa mbunge. Hayo yamebainishwa kwenye taarifa iliyotolewa jana na Ofisi ya Spika ikithibitisha kupokea barua ya CCM iliyotumwa kwenye ofisi hiyo Oktoba 30, mwaka huu. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Nyalandu amevuliwa ubunge huo baada ya kupokea barua kutoka CCM ikiiarifu Ofisi ya Spika kuwa amekosa sifa za kuwa mwanachama wa CCM.

Barua ya CCM iliyoandikwa na Katibu Mkuu wa chama, Abdulrahman Kinana kwenda Ofisi ya Spika ilibainisha kuwa kwa muda sasa chama hicho kilishaanza kumchukulia Nyalandu hatua za kiudhibiti na kinidhamu dhidi ya vitendo na kauli zake zisizoridhisha kinyume cha msingi, falsafa na itikadi ya chama hicho.

“Hivyo, Chama Cha Mapinduzi kuanzia tarehe ya barua yao kimemjulisha Mheshimiwa Spika kuwa Ndugu Lazaro Nyalandu amepoteza sifa za uanachama wa Chama Cha Mapinduzi, na hivyo kupoteza nafasi zote za uongozi wa ndani wa chama hicho na ubunge kwa mujibu wa Ibara ya 13 ya chama hicho,” ilieleza taarifa ya ofisi ya Spika.

Kutokana na kupokea barua ya CCM, ofisi ya Spika ilibainisha kuwa, kutokana na Ibara ya 71(1) (e) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Nyalandu si mbunge tena. Kwa mujibu wa Ibara ya 71(1) (e) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ‘Mbunge atakoma kuwa Mbunge na ataacha kiti chake cha Ubunge iwapo litatokea lolote kati ya mambo yafuatayo: (e) iwapo Mbunge ataacha kuwa mwanachama cha chama alichokuwamo wakati alipochaguliwa au alipoteuliwa kuwa Mbunge.”

“Mheshimiwa Spika, angependa kuwaarifu Watanzania kwamba, kwa barua hiyo kutoka mamlaka halali ndani ya Chama Cha Mapinduzi ambacho Ndugu Lazaro Nyalandu alipata Ubunge na kwa mujibu wa Ibara ya 71(1) (f) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Lazaro Nyalandu si mbunge tena na hatua stahiki za kuiarifu Tume ya Taifa ya Uchaguzi zinaendelea kuchukuliwa,” ilifafanua taarifa hiyo.

Aidha, Ofisi ya Spika ilizidi kubainisha kuwa mpaka jana ilikuwa haijapokea barua ya Nyalandu ya kujiuzulu ubunge. “Ofisi ya Spika inapenda kuwaarifu kwamba mpaka sasa (jana) haijapokea barua kutoka kwa aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Singida Kasikazini (CCM), Lazaro Nyalandu ambayo amekuwa akiarifu kwamba amemwandikia Spika kumtaafiru kujiuzulu wake,” alibainisha.

Jumatatu wiki hii akiwa jijini Arusha, Nyalandu aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii wakati wa Serikali ya Awamu ya Nne na aliyejitosa kuwania Urais wa Tanzania kupitia chama hicho tawala, alitangaza kujiuzulu nyadhifa zake zote ndani ya CCM ikiwemo ubunge. Nyalandu alidai amechukua uamuzi huo kutokana na kutokuridhishwa na mwenendo wa sasa wa siasa, ukiukwaji wa haki za kibinadamu na kutokuwepo kwa mipaka baina ya mihimili ya dola- Serikali, Bunge na Mahakama.
Chanzo-Habarileo

Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 753 336 000 au +255 625 917 902

Masengwa blog Ipo Play Store…Download HAPA ,Uwe unapata habari zote kwa urahisi zaidi
 Bofya Hapa
Powered by Blogger.