Video : MZIMU WA LOWASSA WAMTESA MWAKYEMBE SAKATA LA RICHMOND..AMTUHUMU MBUNGE NASSARI KUINGIA BUNGENI NA KONYAGI
Iikiwa
imepita miaka tisa tangu alipojiuzulu aliyekuwa Waziri Mkuu wa kwanza
wa Serikali ya Awamu ya Nne, Edward Lowasa, mzimu wake umeendelea
kumtesa Dk. Harrison Mwakyembe, aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati Teule ya
Bunge kuhusu suala la Richmond.
Hatua
hiyo inatokana kuibuka kwa suala la Richmond bungeni juzi, hali
iliyosababisha kutupiana vijembe kati yake na Mbunge wa Arumeru
Mashariki, Joshua Nassari (Chadema).
Juzi,
Dk. Mwakyembe ambaye sasa ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na
Michezo, akijibu matamshi ya Nassari, alidai mbunge huyo aliingia
bungeni akiwa amelewa.
Alidai mkakati uliopo wa Chadema kumsafisha Lowassa hautafanikiwa.
Jana,
akizungumza bungeni wakati wa kutihimisha mjadala wa hotuba ya
makadirio ya matumizi ya fedha ya Ofisi ya Rais Tamisemi pamoja na ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk. Mwakyembe, alijibu tena
‘makombora’ yaliyorushwa kwake na Nassari juzi.
“Suala
la Richmond limeibuliwa jana (juzi) na Mbunge wa Arumeru Mashariki,
Mheshimiwa Nassari kwamba Kamati Teule iliyochunguza suala hilo,
haikumtendea haki Mheshimiwa Edward Lowassa kwa sababu haikumuhoji.
“Mimi
naelewa ni kazi mgumu sana leo (jana) hii kutaka kumsafisha Mheshimiwa
Edward Lowassa na kesi ya Richmond ilikwisha na ndiyo maana sioni ajabu
kusema aliyoyasema ilibidi Nassari anywe pombe kwanza.
“Na nayasema haya kiongozi wa upinzani bungeni ajue kwamba tuna tatizo hilo na mimi nawapongeza
sana vijana wetu wa usalama waliokamata hiyo chupa na angeruhusiwa na
hiyo chupa huenda angeweza akatapikia hata rangi zetu za Taifa humu
ndani ingekuwa ni scandal (kashfa) kubwa.
“Mheshimiwa
mimi nimelezea mara nyingi sana katika Bunge hili, hata Bunge la tisa
lililoshughulikia suala la Richmond kuwa Kamati Teule iliyoundwa na
Bunge hili kazi yake ilikuwa kuchunguza siyo kutoa uamuzi,” alisema Dk. Mwakyembe.
Msomi
huyo na mwalimu wa sheria, alisema wakati wa kufanya uchunguzi suala
la kusikiliza upande mwingine halipo, upo wakati wa uamuzi na ndiyo
maana kamati yake iliwasilisha ripoti bungeni ikiwa na mashahidi 40 nje
ya Bunge.
“Aliyetakiwa kuhojiwa hapa akajiuzulu, unamlaumu Mwakyembe kwa hilo? Naomba msipotoshe umma kuwa hakuhojiwa, ahojiwe vipi?
“Unajua
ni aibu, ni sawa na mtu anaenda mahakamani anasema unajua polisi
hawakunipa haki ya kuhojiwa….polisi? Uko mahakamani ndiyo pa kukuhojiwa
hapo,” alisema.
Alisema kamati yake ilikuwa na nyaraka za Serikali 104 na iliwahoji watu 75 ambao waliulizwa maswali 2,717.
Dk. Mwakyembe alisema, kwa sababu hiyo kamati yake haikuona sababu yoyote ya kumuhoji Lowassa kwa sababu ilikuwa na kila kitu.
“Mimi
niombe Mheshimiwa mwenyekiti, kama kuna mtu yeyote hapa bado
anakereketwa na kesi ya Richmond, aache maneno maneno hapa, leta hiyo
kesi hapa kama hatujawanyoa nywele kwa kipande cha chupa.
“Ileta hapa, acha maneno ya kienyeji hapa, tumeshachoka, jamani hee…ileteni hiyo kesi hapa, mnaruhusiwa na kanuni.
“Naomba
nimalizie kwamba, mimi naahidi, siku ambayo kuna mmoja atakuwa jasiri
wa kusema analeta suala la Richmond hapa, mimi naahidi nitamuomba
Mheshimiwa Rais anipumzishe uwaziri niweze kuishughulikia hiyo kesi kwa
ukamilifu iishe moja kwa moja.
“Mheshimiwa
Mwenyekiti kuna hoja nyingine ambayo aliieleza kwenye andiko langu la
Shahada ya Uzamivu niliandika kuhusu Serikali tatu lakini hivi sasa
nasema kuhusu Serikali mbili,” alisema Dk. Mwakyembe.
Akizungumza
matamshi ya Nassari juzi kuwa hiyo inaonyesha jinsi Waziri huyo alivyo
kigeugeukwa kuandika kuwa ili Tanzania iende mbele inahitaji serikali
tatu, lakini akageuka wakati wa Bunge Maalumu la Katiba na kuunga mkono
serikali mbili, Mwakyembe alisema: “Alilewa (Nassari), ndiyo maana alikuwa anasema tu, alikuwa ameambiwa, hajasoma hata hilo andiko,” na kuongeza:
“Na
hapa ndiyo unaelewa watu wasio na integrity, unawajua hapa. Ambao
wanakesha miaka mitano kumtukana mtu kwa kumwita fisadi, leo
wanamkumbatia wanalamba na nyayo zake, ndiyo vigeugeu namba moja hao”.
Hata
hivyo, kabla hajamaliza kuzungumza alisimama Mbunge wa Ubungo, Saed
Kubenea (Chadema) na kuomba mwongozo na utaratibu kwa mujibu wa Kanuni
ya 64(1).
Alisema: “Kwa
mujibu wa Hansard za Bunge, Dk. Mwakyembe alisema Mheshimiwa Edward
Lowassa alijiuzulu kwa mambo yaliyofanywa na walio chini yake, leo
(jana) Dk. Mwakyembe anasema ana ushahidi wa asilimia 100 kwamba Lowassa
alihusika 100 kwa 100 na jambo hilo.
“Naomba
kwa idhini yako unipe muda niwasilishe Hansard hapa kwenye Bunge hili
kuthibitisha maneno ya Dk. Mwakyembe ya Februari mwaka 2008”.
Kubenea
alisema jambo la pili ni kuhusu tuhuma za Dk. Mwakyembe kwamba juzi
Nassari alikuwa na chupa ya Konyagi na aliingia nayo bungeni.
“Siyo
kweli, nina uwezo wa kulithibitishia Bunge hili kwamba Nassari jana
hakuwa amelewa. Tulikuwa naye mchana kutwa na alikuwa amekuja bungeni
na soda ambayo ilikuwa imewekwa kwenye chupa,”alisema.
Baada
ya maelezo hayo, Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge, alisema kwa
taarifa alizo nazo, chupa anayodaiwa kuwa nayo Nassari ilikuwa ni nje
ya Bunge wala siyo ndani ya Bunge kama inavyodaiwa.
Nje
ya Ukumbi wa Bunge, Nassari alisema alijibu tuhuma hizo za Dk.
Mwakyembe kwa sababu kitendo cha Serikali kuhangaika naye tangu juzi
ni kwamba amewagusa sehemu nyeti na Waziri huyo (Dk. Mwakyembe) si mtu
wa kuaminika.
MSIKILIZE HAPA MWAKYEMBE AKIZUNGUMZA BUNGENI
MSIKILIZE HAPA MWAKYEMBE AKIZUNGUMZA BUNGENI
Masengwa blog Ipo Play Store…Download HAPA ,Uwe unapata habari zote kwa urahisi zaidi