TAKUKURU SHINYANGA YAWAFIKISHA MAHAKAMANI WATUMISHI WA KANISA LA AICT KWA KUTAFUNA MILIONI 63.4
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Shinyanga
imewakamata na kuwafikisha mahakamani watumishi watatu wa Hospitali
binafsi inayomilikiwa na Kanisa la AICT Shinyanga wakituhumiwa kwa kosa
la kuisababishia hasara serikali kiasi cha shilingi milioni 63.4.
Watumishi waliofikishwa mahakamani ni pamoja na aliyekuwa mganga mkuu wa
hospitali hiyo, Dkt. Elimeleki Katani, wakuu wa idara ya uhasibu, Hamis
Batano na Samson Maselle.
Watumishi hao wote kwa pamoja mbali ya mashitaka ya kuisababishia hasara
serikali pia wanashitakiwa kwa makosa ya matumizi mabaya ya madaraka
yao ikiwemo matumizi mabaya ya fedha ya ruzuku inayotolewa na serikali.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa waandishi wa habari na Ofisa
Uhusiano na habari wa TAKUKURU makao makuu Mussa Misalaba, watumishi hao
wanashitakiwa kwa makosa manne ikiwemo kulipa mishahara hewa na
kuwasilisha michango hewa NSSF kwa mstaafu aliyetajwa kwa jina la Dkt.
Emmanuel Mwandu.
Misalaba alisema katika shitaka la kwanza washitakiwa hao wanadaiwa kati
ya Juni 10, 2011 na Januari 1, 2016 walitumia madaraka yao vibaya kwa
kushindwa kurejesha kwa mlipaji mkuu wa serikali mshahara wa mstaafu,
Dkt. Emmanuel Mwandu kiasi cha shilingi 63,479,800.
Shitaka la pili inadaiwa washitakiwa hao kati ya Septemba 18, 2013 na
Agosti 21, 2014 waliandaa na kupeleka katika Shirika la Hifadhi ya Jamii
(NSSF) kiasi cha shilingi 14,361,124 ikiwa ni michango ya mstaafu, Dkt.
Emmanuel Mwandu.
Shitaka la tatu linamuhusu mshitakiwa Batano anayedaiwa kati ya Mei 30,
2011 na Januari 6, 2014 alitumia madaraka yake vibaya na kuandaa orodha
ya malipo kama mshahara wa mstaafu Dkt. Emmanuel Mwandu kiasi cha
shilingi 14,361,124 huku shitaka la nne la kuisababishia hasara serikali
kiasi cha shilingi 63,479,800 likiwahusu washitakiwa wote.
Tayari washitakiwa wote wamesomewa mashitaka yao na mwendesha mashitaka
wa TAKUKURU, Carson Nkya mbele ya Hakimu mkazi mfawidhi, Rahimu Mushi na
wamekana mashitaka yote ambapo kesi hiyo imeahirishwa mpaka Mei 3,
mwaka huu itakapotajwa tena mahakamani hapo. Washitakiwa wote wako nje
kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya dhamana.
Wakati huo huo ofisi ya TAKUKURU mkoani Shinyanga imepokea jumla ya
taarifa 36 za matukio ya rushwa yaliyoripotiwa ndani ya kipindi cha
miezi tisa iliyopita (Julai 2016 hadi Machi 31, 2017) zikihusisha idara
ya mahakama, polisi, ardhi, afya, elimu, taasisi binafsi, madini,
biashara, michezo na siasa.
Akitoa taarifa ya utendaji kazi ya taasisi yake, Kamanda wa TAKUKURU
mkoa wa Shinyanga, Gasto Mkono alisema tayari wanaendelea na uchunguzi
wa kina juu ya taarifa zilizopokelewa kwa kufungua majalada ya uchunguzi
kwa ajili ya kuchunguza taarifa zote zilizopokelewa.
Mbali ya kupokea taarifa za matukio ya rushwa pia TAKUKURU mkoani humo
katika kipindi hicho cha miezi tisa imefanikiwa kuokoa kiasi cha
shilingi 114,479,838.28 kutoka idara za Afya, Elimu na kilimo zilizokuwa
zitumike kinyume cha utaratibu ikiwemo ulipaji mishahara hewa.
“Katika kipindi cha miezi tisa iliyopita tumepokea taarifa 36
zinazohusiana na masuala ya rushwa na tayari tumefungua majalada 23 ya
uchunguzi kuhusiana na taarifa hizo, taarifa hizi zinahusu upande wa
idara za elimu, michezo, biashara na siasa, na tayari kesi tatu
zimefikishwa mahakamani”.
“Lakini pia zipo kesi tisa zinazoendelea mahakamani zikihusisha idara
za fedha katika halmashauri, afya, elimu na Jeshi la Polisi ambapo
katika kipindi hiki tumeshinda kesi tatu huku tukishindwa kesi nne na
kesi tisa bado zinaendelea kusikilizwa”,aliongeza Mkono.
Alieleza kuwa ofisi yake inaendelea na utafiti na udhibiti ya mianya ya
rushwa katika idara mbalimbali za serikali na taasisi binafsi ikiwemo
pia kufuatilia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika
halmashauri za manispaa na wilaya ili kubaini iwapo inatekelezwa kwa
kiwango kinacholingana na fedha zilizotolewa.
Aidha Kamanda huyo wa TAKUKURU aliwapongeza wakazi wa mkoa wa Shinyanga
ikiwemo vyombo vya habari kwa msaada mkubwa wanaoutoa na kuweza
kufanikisha kukabiliana na matukio ya rushwa katika idara mbalimbali za
umma na hivyo kudhibiti upotevu wa fedha za serikali kwa njia ya ulipaji
mishahara hewa.
“Tunawashukuru wakazi wa mkoa wa Shinyanga ikiwemo wana habari kwa
msaada mkubwa wanaotupatia katika mapambano haya dhidi ya vitendo vya
rushwa katika mkoa wetu, na tunawaomba wasichoke waendelee kutupatia
taarifa mbalimbali zitakazosaidia kuwakamata na kuwafikisha mahakamani
watuhumiwa wote”, alieleza Mkono.
Masengwa blog Ipo Play Store…Download HAPA ,Uwe unapata habari zote kwa urahisi zaidi