DKT. SAJAD RAI KUNG’ARA WORLD CEO SUMMIT 2026, KUJADILI NISHATI, VIWANDA NA UWEKEZAJI

  


Dkt. Sajad Habib Rai
***
MTAALAM katika Sekta ya Nishati ya Mafuta nchini, Dkt. Sajad Habib Rai, ameteuliwa kuwa mjumbe na mmoja wa wazungumzaji mashuhuri (Jopo) katika Mkutano wa 'World CEO Summit 2026 Africa' unaotarajiwa kufanyika Novemba 26 hadi 27 jijini Dar es Salaam.

Mkutano huo wa kimkakati utakaojadili masuala ya uwekezaji sambamba na mahusiano ya kibiashara kwa siku hizi mbili, utawakutanisha zaidi ya Wakurugenzi Wakuu (CEOs) 1,000, Wawekezaji, watunga Sera na viongozi wa sekta mbalimbali kutoka zaidi ya nchi 50.

Dkt. Sajad Habib Rai, ambaye ni Meneja Mkazi wa 'Mansoor Industries Limited', anatarajiwa kuzungumza katika Mkutano huo juu ya uzoefu wake kuhusu masuala ya maendeleo ya viwanda, nishati, uwekezaji, uendelevu na ushirikiano wa kimkakati kwa ajili ya kukuza uchumi wa Afrika.

Dkt. Rai atatoa mitazamo na uzoefu muhimu kuhusu maendeleo ya viwanda, nishati, uendelevu, uwekezaji, pamoja na ushirikiano wa kimkakati unaohitajika ili kuimarisha uwezo wa uzalishaji barani Afrika na kuharakisha mabadiliko ya kiuchumi," ilisema taarifa iliyotolewa na waandaji wa mkutano huo utakaofanyika Ocean View Arena.

Aidha, akizungumza kuhusu ushiriki wake katika Mkutano huo, Dkt. Sajad ambaye pia kwa kipindi kirefu amekuwa mshauri katika sekta ya nishati hususani mafuta, amesema pamoja na kuwasilisha uzoefu wake katika Mkutano huo, anatarajia pia kujifunza masuala mengine mengi kutoka kwa wazungumzaji wengine.

"Nimepokea mualiko wa mkutano huo kwa furaha kubwa, lengo ni kuchangia uchumi wa nchi yetu na kuhamasisha uwekezaji, hivyo nami kama mzalendo wa nchi hii nitajifunza mengi lakini pia nitatoa uzoefu wangu ili kwa pamoja tuweze kuijenga Tanzania na Afrika inayojitegemea kiuchumi," amesema Dkt. Sajad.

World CEO Summit / Africa ni mkutano baina ya viongozi wa Kampuni za kibiashara, Serikali na wawekezaji unaolenga kujadili namna ya kukuza biashara na uchumi wa Afrika ambapo kwa huu Kaulimbiu yake inasema “Uniting Leadership, Capital and Policy for Africa’s Transformation” (kuunganisha uongozi, mitaji na sera kwa ajili ya mabadiliko ya Afrika).

Masuala mengine yanayotarajiwa kuzungumziwa katika Mkutano huo ni pamoja na upatikanaji wa mitaji, Maendeleo ya viwanda na biashara, Uongozi na Sera za kiuchumi, Teknolojia, ukuaji na ubunifu wa Akili Unde (AI), Nishati na miundombinu pamoja na Kilimo na usalama wa chakula.

Maeneo mengine ni pamoja na Huduma za kifedha, Afya na mali isiyohamishika,Uendelevu na ukuaji wa biashara,Ushirikiano wa kimkakati, ubia na upanuzi wa masoko.

Post a Comment

0 Comments