Mauaji ya walinzi tishio Geita, mwingine auawa akilinda maduka 15


Mkuu wa Wilaya ya Geita, Herman Kapufi
 Mauaji ya walinzi mkoani Geita yameendelea kuwa tishio kwa usalama wao baada ya mlinzi mwingine aliyekuwa akilinda maduka yapatayo 15, kuuawa kwa kupigwa na kitu chenye ncha kali kichwani. 

Mauaji ya mlinzi huyo Kisusi Iddy (40) aliyekuwa akilinda maduka hayo kwenye Mtaa wa Mwatulole, ni muendelezo wa matukio ya kuuawa walinzi wa maduka na mali mbalimbali kwani katika kipindi cha miaka miwili  jumla ya walinzi 20 wameuawa. 

Taarifa zilizopatikana jana kuhusu mauaji ya mlinzi huyo na kuthibitishwa na mwenyekiti wa mtaa huo, Fikiri Toi zilieleza kuwa tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia Januari Mosi na wauaji hao hawakuiba kitu chochote. 

Mwili wa Iddy ulikutwa umefunikwa kwa shuka lake alilokuwa akilitumia lindoni, huku likiwa limetapakaa damu. 

Kutokana na tukio hilo, Mkuu wa Wilaya ya Geita, Herman Kapufi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama amefuta vibali vyote vya waganga wa tiba za asili kwa madai wao ni moja ya chanzo cha imani za kishirikina zinazosababisha mauaji hayo.

 Alisema kutokana na kukithiri kwa mauaji hayo, mamlaka yake inakusudia kufufua Jeshi la Jadi (Sungusungu) ili kusaidia kuyadhibiti. 

Hata hivyo, Kapufi alisema uchunguzi wa awali ulionyesha kuwa wakati wa uhai wake, Iddy alikuwa analinda maduka ya wafanyabiashara yanayofikia 15 na kwamba baada ya kufuatilia, hakuwa na mafunzo yoyote ya ulinzi.

 Aliyepigwa na wafugaji Moro afariki 
Fabian Bago (21) anayedaiwa kushambuliwa na wafugaji katika Kijiji cha Kolelo, Morogoro, amefariki dunia katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Morogoro alikokuwa akipatiwa matibabu. 

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Frank Jacob alisema kijana huyo alifariki dunia saa 11 jioni jana akiwa kwenye wodi ya wagonjwa wanaohitaji uangalizi wa karibu na kwamba mwili wake umehifadhiwa kusubiri taratibu nyingine za kipolisi.

 Dk Jacob alisema mara baada ya kufikishwa hospitalini hapo, kijana huyo alifanyiwa vipimo na matibabu lakini alifariki dunia kutokana na majeraha makubwa kichwani yaliyoharibu sehemu ya ubongo. 

Baba mzazi wa kijana huyo, Alan Bago alisema ameshatoa taarifa polisi kuhusina na kifo cha kijana wake na sasa anasubiri maelekezo ya polisi ili aweze kuendelea na taratibu za mazishi.

Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 753 336 000 au +255 625 917 902

Masengwa blog Ipo Play Store…Download HAPA ,Uwe unapata habari zote kwa urahisi zaidi
 Bofya Hapa
Powered by Blogger.