LOWASA AMPONGEZA MAGUFULI KWA KUFANYA HAYA
ALIYEKUWA Mgombea Urais Kupitia Tiketi ya Chadema katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana Edward Lowassa amempungeza Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Rais John Magufuli kwa kufanya jambo ambalo yeye hakutegemea kuwa atafanya.
Lowassa ambaye ni Mjumbe wa kamati kuu ya Chamacha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), amepongeza litendo cha Rais Magufuli kumteua Emmanuel Nchimbi aliyekuwa kwenye kambi ya yake (team Lowassa) wakati wa mbio za kuelekea uchaguzi mkuu mwaka jana.
uteuzi huo umezihirisha wazi kua rais Magufuli sio mtu wa kulipa visasi.
Akizungumza na JAMBO LEO jana, Lowassa aliyechuana kuwania urais na Rais Magufuli baada ya kuhamia Chadema kutoka CCM, alisema ni jambo jema kushirikisha viongozi kuongoza nchi na kubainisha kuwa mbali na Dk. Nchimbi uteuzi wa mabalozi wengine pia umemfurahisha.
Wakati Lowassa (pichani) ambaye pia Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema akipongeza uteuzi wa mabalozi hao wanaosubiri kupangiwa vituo vyao vya kazi, wasomi waliozungumza na gazeti hili walisema uteuzi wa Dk. Nchimbi unalenga kumaliza mvutano na mgogoro ulioibuka ndani ya CCM wakati wa mchakato wa chama hicho kupata mgombea wake wa urais katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana.
Juzi Rais Magufuli aliteua mabalozi 15 wakiwemo mawaziri wa zamani, watoto wa viongozi na makada wa CCM kujaza nafasi zilizo wazi katika Balozi za Tanzania nchi mbalimbali na wengine sita watakaoliwakilisha Taifa kwenye balozi zake mpya sita.
Julai 10 mwaka jana baada ya Kamati Kuu ya CCM kutangaza majina matano ya waliowania kuteuliwa kugombea urais na chama hicho, Dk. Nchimbi na wajumbe wenzake wawili wa Kamati Kuu, Sophia Simba na Adam Kimbisa walitoka hadharani wakisema wanajitenga na uamuzi ya kamati hiyo kwa kuwa imekiuka Katiba ya CCM.
Nchimbi ambaye wakati huo alikuwa Mbunge wa Songea Mjini, aliitisha mkutano na waandishi wa habari na kueleza wanapinga uamuzi huo ambao hawakuutaja, wakidai kuwa si majina yote yaliyowasilishwa mbele ya kamatihiyo.
Akiwa pamoja na wenzake hao, Dk. Nchimbi alisema kikao hicho hakikufuata kanuni kwa kuwa majina machache yaliwasilishwa na hayakuhusisha mgombea anayekubalika.
Ingawa hawakumtaja mgombea huyo waliyesema anatajwa na wengi, makada hao walifahamika kuwa wanamuunga mkono Lowassa. Mchakato huo ulimaliza kwa Dk. John Magufuli kupitishwa kupeperusha bendera ya CCM katika uchaguzi huo na kumshinda Lowassa ambaye baada ya jina lake kukatwa alihamia Chadema na kupitishwa kuwania urais kwa tiketi ya chama hicho na Ukawa.
Baada ya Rais Magufuli kupitishwa kuwania urais, Dk Nchimbi alikaririwa na vyombo vya habari akisema kambi yao inamuunga mkono kwa kuwa ni mtendaji mzuri wa kazi anazopewa na mifano ipo mingi katika wizara alizoziongoza.
Katika uchaguzi huo, Dk Magufuli alipata kura milioni 8.8 sawa na asilimia 58.47, akifuatiwa na Lowassa aliyepata kura milioni 6.07, sawa na asilimia 39.97.
Lakini jana, Lowassa alipoulizwa kuhusu uteuzi huo kutokana na ukaribu wake Dk. Nchimbi alisema: “Ni vizuri kuwashirikisha viongozi katika kuongoza nchi. Ni jambo jema sana kuteuliwa kwa Nchimbi. Ni kitu kizuri.”
Hata hivyo, wakati Lowassa alisema hataki kuzungumzia kiundani uteuzi huo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), Dk. Benson Bana alisema: “Nchimbi alikuwa analalia upande wa Lowassa hilo lipo wazi…,nadhani msimamo wake unabaki palepale licha ya kutojiuzulu na kuendelea kubaki kuwa mjumbe wa kamati kuu ya CCM.”
“Alieleza maoni yake wazi na hajawahi kujitokeza hadharani kukana yale aliyokuwa akiyaamini. (Nchimbi) alikubaliana na uamuzi wa chama (kumpitisha Dk. Magufuli), chama kimeona ni kada wake muhimu, imetokea fursa na hajabaniwa. Ni uamuzi wa Mwenyekiti wa CCM kutaka kusawazisha mambo, kutokaa na mtu na kinyongo.”
Alisema huenda ikatokea siku Rais Magufuli akakutana na wote ambao walionekana kutokuwa na msimamo wa kumuunga mkono wakati wa mchakato wa CCM kupata mgombea wake wa urais. “Sidhani kama Nchimbi akionekana hadharani atatembea kwa raha maana wapo wanaomuita msaliti aliyebaki CCM, lakini kwa uteuzi huu shutuma hizi zitapungua.
Alitajwa kugombea uspika wa Bunge ila taarifa zikafifia, hata wajumbe wa Kamati Kuu nao walikuwa wakimnyoshea kidole maana alionekana mtu asiyemuunga mkono sana Magufuli,” alisema.
Alisema uteuzi huo unalenga kumwondoa katika kundi la watu wanaomtuhumu: “Akiwa Dar es Salaam utasikia yuko Masaki kwa kujificha…, uswahiba ni uswahiba tu haufutiki kwa sababu za kisiasa.” “Sasa akionekana na mheshimiwa aliyekuwa akimuunga mkono watu wanaweza kuchombeza mengine. Uteuzi huu unapunguza hako ka mvutano ndani ya chama.”
Dk. Bana alienda mbali zaidi na kufafanua kwamba, uteuzi huo utawajengea uzoefu wateule hao na baadaye wanaweza kurejea nchini na kuwania ubunge na kushinda kama ilivyokuwa kwa Dk. Deodorus Kamara ambaye alikuwa Balozi nchini Ubeligiji kabla ya kurejea nchini na kushinda ubunge Jimbo la Nkenge.
Mhadhiri mwingine wa chuo hicho, Dk James Jesse alisema: “Kwenye siasa kuna ambao utakuwa nao pamoja na wengine hawatokuunga mkono. Katika kuwania urais lazima kuwe na kambi na chama kama CCM huwezi kushangazwa na kambi.”
Aliongeza: “Kambi zinaweza kuonekana adui wakati wa uchaguzi, ila ukimalizika kambi hizo hazipaswi kuendeleza uadui maana anayeteuliwa na chama kugombea anabeba bendera na akishinda uchaguzi ni rais wenu iwe mlimpinga au kumuunga mkono.” Alibainisha kuwa mtu yeyote anayeelewa huweka tofauti pembeni baada ya kumalizika kwa uchaguzi.
“Uteuzi huu ni ishara nzuri ya (Rais Magufuli) kuwambia wana CCM kwamba pamoja na kutofautiana naye katika mchakato wa chama hicho kusaka mgombea, washirikiane naye katika kufanya kazi. Ni nia njema na inaondoa tofauti za maoni na mtazamo,” alisema.
Dk. Jesse alisema jambo hilo linapaswa kuigwa hata na wafuasi wa CCM waliohamia vyama vya upinzani.
Masengwa blog Ipo Play Store…Download HAPA ,Uwe unapata habari zote kwa urahisi zaidi