MABILIONI YA MRABAHA KUTOKA BARRICK NORTH MARA YAANZA KUTEKELEZA MIRADI YA MAENDELEO KWA KASI TARIME VIJIJINI

   

Wenyeviti wa vijiji vya Kewanja, Kerende, Genkuru, Nyamwaga na Nyangoto wakiwa katika mojawapo ya matukio ya kupokea gawio la mrahaba kutoka Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara mwaka 2025.

Miradi mipya ya kijamii imeanza kutekelezwa kwa kasi katika vijiji vitano kutokana na fedha za gawio wa mrabaha zilizotolewa na Mgodi wa Dhahabu wa North Mara katika miaka ya hivi karibuni ambazo zimekuwa zinawekwa kwenye akaunti za benki kwa muda mrefu bila matumizi yoyote ya miradi ya kuwaletea maendeleo wananchi wa vijiji hivyo.


Kila robo ya mwaka vijiji vya Genkuru, Nyangoto, Kerende, Nyamwaga na Kewanja ambavyo vipo katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Mkoani Mara vimekuwa vikipokea gawio la mrabaha kutokana na haki ya kuchimba dhahabu katika shimo la Nyabigena (ambalo ni sehemu ya Mgodi wa Barrick North Mara) kabla ya kampuni ya Barrick kukabidhiwa kuendesha mgodi huo kwa ubia na Serikali kupitia kampuni ya Twiga Minerals kuanzia mwaka 2019.

Viongozi wa vijiji hivyo waliwaeleza waandishi wa habari mwishoni mwa wiki kuwa fedha hizo za mrabaha ambazo vimekuwa vikipokea mara kwa mara kutoka mgodi wa North Mara kutokana na makubaliano sasa zzimeanza kueelekezwa kwenye miradi ya kijamii inayogusa mahitaji ya wananchi wengi badala ya kukaa benki bila matumizi kutokana na kutoibuliwa miradi mipya.

Katika kijiji cha Genkuru pekee, zaidi ya shilingi bilioni 2 zilizotokana na mrabaha zimeelekezwa kwenye ujenzi na ukarabati wa miradi mbalimbali ya elimu, afya, barabara na ununuzi wa eneo la kujenga soko.

“Tulianza na ukarabati wa barabara yenye urefu wa kilomita 7.8 na nyingine yenye urefu wa kilomita zaidi ya tatu inayounganisha kijiji chetu cha Genkuru na kijiji jirani cha Msege, na utekelezaji wa miradi hii umefikia asilimia 90.

“Kwa upande mwingine, tumetumia sehemu ya fedha yetu ya mrabaha kununua mashine ya usingizi ya Kituo cha Afya Genkuru,” alisema Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Genkuru, Juma Elias Kegoye.

Kegoye anaongeza kuwa wametumia sehemu ya fedha hiyo pia kununua (microscope) ya kupima wagonjwa na kwenye ujenzi wa nyumba pacha ya watumishi katika kituo hicho cha afya.

Pia alisema wanakarabati nyumba ya mwalimu katika Shule ya Sekondari Bwirege, nyumba saba za walimu katika Shule ya Msingi Genkuru na ujenzi wa jengo la utawala wa shule ya msingi mpya ya Kerondo.

“Miradi mingine inayotekelezwa ni ujenzi wa jengo la utawala katika shule ya msingi mpya ya Kuruya na ununuzi wa viti 350 na meza zake kwa ajili ya wanafunzi wa kidato cha kwanza Shule ya Sekondari Bwirege,” aliongeza Kegoye.

Alitaja mradi mwingine uliyo kwenye mpango wa kutekelezwa kutokana na fedha za mrabaha kuwa ni ujenzi wa nyumba ya walimu katika Shule ya Msingi Rewandwi.

“Tunajenga pia vyumba vinne vya madarasa na kuchimba matundu sita ya vyoo katika shule hiyo ya Rewandwi,” aliongeza Mwenyekiti Kegoye.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Kewanja, Joshua Chacha alisema: “Sisi tumeelekeza fedha za mrabaha kwenye ujenzi wa nyumba pacha (two in one) ya walimu katika Shule ya Msingi Kewanja.”

“Vilevile, tunajenga nyumba pacha ya watumishi katika zahanati ya kijiji chetu,” aliongeza Chacha na kubainisha kuwa miradi yote hiyo ilitengewa shilingi milioni 280 zilizotokana na gawio la mrabaha.

Naye Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Nyamwaga, Emmanuel Wankaba, alitaja miradi inayotekelezwa katika kijiji hicho kutokana na fedha za mrabaha kuwa ni pamoja na ujenzi wa vyumba saba vya madarasa ya shule ya msingi mpya ya Maika.

“Sambamba na vyumba hivyo vya madarasa, tunajenga jengo la utawala na nyumba ya kuishi familia mbili za walimu na tunakarabati nyumba ya mwalimu katika Shule ya Msingi Nyamwaga,” aliongeza Wankaba.

Alitaja miradi mingine iliyo kwenye mpango wa kutekelezwa kijijini hapo kuwa ni ukarabati na uzibuaji wa barabara mbili zenye urefu wa kilomita zaidi ya 10 na uwanja wa michezo wa Shule ya Msingi Nyamwaga.

Viongozi hao wa vijiji walisema utekelezaji wa miradi mingi uko katika hatua za mwisho kukamilika na kwamba wananchi wameipokea kwa furaha - wakitarajia kuona maboresho ya huduma za kijamii na kuchochea maendeleo katika maeneo yao.

Aidha, walieleza kuwa matumizi ya fedha za mrabaha yamezingatia vipaumbele vya wananchi, baada ya kufanyika kwa vikao vya ushirikishwaji na kubaini mahitaji muhimu zaidi.

Walisema uwekezaji wa fedha za mrabaha katika miradi ya kijamii ni hatua muhimu katika kuhakikisha madini yanawanufaisha wananchi wa maeneo yanayozalisha rasilimali hizo.

Mgodi wa Dhahabu wa North Mara unaendeshwa na kampuni Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia kampuni ya Twiga Minerals.

Viongozi hao wa vijiji walipongeza Kampuni ya Barrick kwa uwajibikaji wa kutoa gawio la mrabaha kwa vijiji husika, wakisema ni mfano mzuri wa matumizi ya mapato ya madini kwa maendeleo ya jamii.

“Mafanikio haya yote ni matunda ya ushirikiano mzuri kati ya mgodi wa Barrick North Mara na jamii inayouzunguka. Fedha hizi kwakweli zimefanya mambo makubwa, wananchi walikuwa hawaoni babarara , sasa hivi wanaziona barabara, tumenunua vifaa tiba , walikuwa hawana soko sasa watakuwa na soko ,” alisema Mwenyekit Kegoye akieleza na chanzo cha mrahaba unatoka mgodi huo kilivyo na manfuaa kwenye kijiji chake.

Taarifa zilizopo zinaonesha kuwa mgodi wa Barrick North Mara ulitoa kiasi cha shilingi bilioni 8.383 bilioni ikiwa ni gawio la mrahaba huo kwa vijiji hivyo kati ya Juni 2023 hadi Mei 2025.

Fedha hizi za mrabaha ni tofauti na mabilioni ya fedha yanatolewa na mgodi huo kila mwaka kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ndani ya vijiji vyote vya halmashauri ya wilaya ya Tarime kupitia sera ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) kila mwaka .

Kwa mujibu wa takwimu zilizopo mgodi huo umetumia zaidi ya shilingi bilioni 26.86 katika kutekeleza miradi ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) zaidi ya 255 katika sekta mbalimbali, ikiwemo elimu ya msingi na sekondari, afya, miundombinu ya barabara, maji, miradi ya kiuchumi na mazingira tangu mwaka 2019 ulipokuwa chini ya kampuni ya Barrick na Serikali ya Tanzania kupitia kampuni ya Twiga.

Post a Comment

0 Comments