CHADEMA WAMVAA DED ARUSHA


 Sakata la posho za madiwani katika Jiji la Arusha limeibua vita mpya baina ya Chadema na uongozi wa Jiji huku kila upande ukijaribu kuibua tuhuma dhidi ya mwingine.


Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Athuman Kihamia hivi karibuni alitangaza kukata posho za nauli za madiwani ambao karibu wote wanatoka Chadema kutoka Sh60,000 hadi 10,000 huku akiwataka kurejesha jumla ya Sh40.8 milioni walizolipwa kwa ajili ya mawasiliano na mafuta kuanzia Novemba 2015 hadi Agosti 2016.

Wakati msuguano huo ukiendelea, madiwani hao nao wamedai kupata nyaraka zinazoonyesha kuwa mkurugenzi huyo amejiidhinishia lita 1,900 za mafuta kwa ajili ya gari lake kwa mwezi kinyume na kanuni na Sheria za Serikali za Mitaa.

Imeelezwa kuwa katika bajeti ya Jiji la Arusha, ofisi ya mkurugenzi imetengewa lita 70 kwa wiki sawa na lita 280 hadi 300 kwa mwezi lakini Agosti mwaka huu aliandikiwa dokezo la kuomba lita 900 za mafuta ya dizeli yenye thamani ya Sh1,705,500 kwa Septemba.

Katika dokezo jingine la Agosti 30, mwaka huu, mkurugenzi huyo anadaiwa kuomba lita1,000 kwa ajili ya matumizi ya dharura ya ofisi yake nje ya Wakala wa Huduma za Ununuzi Serikalini (GPSA) ambayo yalinunuliwa kwenye kampuni binafsi.

Akijibu dokezo hilo, ofisa ununuzi alimshauri kuwa Sheria ya Manunuzi ya mwaka 2011 inataka kununua kwa wakala wa Serikali kabla ya kwenda kununua kampuni binafsi.

Pia, Kihamia anadaiwa amekuwa akiidhinisha mafuta na posho kwa ofisi ya mkuu wa wilaya na mkuu wa mkoa kwenye majukumu yasihusu halmashauri hiyo jambo linaongeza mzigo usiokua na msingi.

Hata hivyo, katika taarifa yake kujibu tuhuma hizo, Kihamia hakugusia moja kwa moja maombi ya mafuta hayo, bali alisema jiji hilo hutumia lita 18,900 za mafuta kwa mwezi katika idara 13 na vitengo vyake vitano vyenye magari 48 na mitambo mitano akisema idara za ujenzi na usafishaji mazingira zina matumizi makubwa zaidi.

Alisema Jiji linaweza kununua mafuta kwenye vituo binafsi endapo ikitokea dharura na GPSA ikiwa haina mafuta kwa wakati huo huku sheria ikitaka bei isizidi viwango vya wakala huyo.

Alisema tuhuma zinazomkabili zinatokana na jitihada zake za kutatua kero na kuwahudumia wananchi bila kujali itikadi zao na mpango wake wa kubana matumizi kwa kuondoa posho zisizokuwa na tija kwa madiwani.

“Wapo watu wachache wasiokuwa waaminifu wanaopanga kuchafua kila jema ninalofanya lakini sitavunjika moyo, nitaendelea kuwahudumia wananchi na kusimamia miradi ya maendeleo,” alisema.

Alikanusha tuhuma za kuidhinisha mafuta na posho kwa ofisi ya mkuu wa wilaya na mkoa ambazo hazihusiani na shughuli za halmashauri ya jiji la Arusha.

Hata hivyo, Diwani wa Ngarenaro, Isaya Doita alisema wanazo nyaraka zinazothibitisha madai yao dhidi ya mkurugenzi huyo.

“Tutakutana kwenye kikao cha kamati ya fedha na utawala hivi karibuni huko tutafahamu sababu za matumizi hayo ambayo hayazingatii taratibu, wakati malipo yaliyopitishwa kwa kufuata taratibu hayafanyiki,” alisema Doita.

Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 753 336 000 au +255 625 917 902

Masengwa blog Ipo Play Store…Download HAPA ,Uwe unapata habari zote kwa urahisi zaidi
 Bofya Hapa
Powered by Blogger.