
Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) ambaye ni mdhamini mkuu wa Ligi Kuu ya NBC imekabidhi basi jipya kwa Coastal Union FC ya Tanga.
Coastal Union inakuwa klabu ya nne ya ligi kuu kunufaika na mpango huo unaohusisha mkopo nafuu kutoka benki ya NBC baada ya klabu za KMC, Singida Black Stars na Namungo FC
Mkopo wa basi la hilo unaifanya benki ya NBC kuwa imetoa jumla ya mikopo yenye thamani ya sh. bilioni 1.2 kwenye usafiri wa vilabu hivyo vinne vilivyonufaika na mpango huo.
Hafla ya makabidhiano ya basi hilo iliyohusisha paredi maalum la basi hilo katika maeneo mbalimbali ya jiji la Tanga, imefanyika leo kwenye tawi la benki ya NBC Tanga ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Lushoto Zephania Stephan Sumaye aliemuwakilisha Mkuu wa Mkoa huo Balozi Dkt. Batilda Burian.
Akizungumza kwa niaba ya Dkt. Burian, DC Sumaye pamoja na kuipongeza benki hiyo kwa hatua hiyo muhimu, amesema hatua hiyo imekuja wakati sahihi...
“Kilichofanywa na NBC leo ni kama kuunga mkono muitikio wa wito huu wa Rais Samia. Nimevutiwa zaidi kuona NBC wanagusa hadi masuala ya bima kwa wanamichezo hilo ni jambo zuri zaidi. Ombi Langu kwa wachezaji na viongozi wa klabu ni kuhakikisha kwamba jitihada hizi zinatoa majibu kwenye matokeo ya uwanjani,’’ amesema.
Mkurugenzi wa Biashara wa Benki ya NBC, Elvis Ndunguru amesema basi hilo ni sehemu ya mpango wa utoaji wa mikopo yenye masharti nafuu kwa vilabu vinavyoshiriki ligi hiyo.
Amesema ukosefu wa vyombo vya usafiri maalum kwa ajili ya timu zinazoshiriki ligi kuu ya NBC imekuwa ni moja ya chanzo cha vikwazo vingi katika gharama za uendeshaji na utendaji wa timu husika.
"Jitihada zetu kama wadhamini haziishii hapa tu kwenye mikopo ya usafiri bali tunagusa maboresho ya baadhi ya viwanja vinavyotumia kwenye ligi hii, tunatoa bima za afya kwa wachezaji na mabenchi ya ufundi na zaidi tunatoa huduma za kifedha ikiwemo elimu ya kifedha kwa wadau wa michezo wakiwemo wachezaji,’’ amesema.
Naye Mwenyekiti wa Coastal Union amekiri kuwa klabu hiyo ilikuwa ikikabiliwa na changamoto ya usafiri bora hali ambayo iliongeza changamoto katika ubora wa timu.
“Tanga sasa tumeweka alama kupitia benki ya NBC. Kupitia usafiri huu sasa tuna uhakika wa kusafirisha wachezaji wetu kwenda popote, wakati wowote tena wakiwa na utulivu zaidi.Ni wazi sasa tunakwenda kuongeza ushindani zaidi kwenye ligi kupitia hatua hii ya leo,’’ amesema Muhsin.
0 Comments