ALIYEFUKUZWA KAZI KWA KUMKASHIFU RAIS SAMIA NA KUPINGA TOZO AKAMATWA

TAARIFA zilizotufikia hivi punde Jeshi la Polisi kanda maalum ya Dar es Salaam limemkamata aliyekuwa Meneja wa TRC mkoa wa Dar es Salaam ambaye alifukuzwa kazi kwa kukosoa tozo za miamala, Jonas Afumwisye, akiwa nyumbani kwake na kumpeleka katika kituo cha polisi cha kati.

Wakili wake Peter Kibatala akizungumza na MwanaHALISI Online kwa njia ya simu leo Ijumaa tarehe 26, Agosti, 2022, amesema Afumusye amempigia simu na kumweleza kuwa Polisi wamemfuata nyumbani kwake na kuondoka naye kuelekea Central Polisi.

Bado haijafahamika sababu hasa za kukamatwa kwa Ofisa huyo ambaye kufukuzwa kwake kazi kuliibua mjadala katika mitandao ya kijamii na vyombo mbalimbali vya habari hapa nchini.

Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Masanja Kadogosa alimwandikia barua Afumwisye kumjulisha kuhusu kufukuzwa kazi Agosti 19, 2022, kwa kile alichoeleza ni kuthibitika kwa tuhuma zilizo kuwa zikimkabili.

Barua hiyo inaeleza Afumwisye alienda kinyume na kanuni ya 42 jedwali la kwanza, sehemu A kipengele cha 10 cha kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2003.

“Kati ya Julai 10 na Septemba 25 mwaka 2021, kupitia makundi ya kijamii, ulipinga juhudi za Serikali kuanzisha tozo kwenye miamala ya simu,” inasomeka barua ya Kadogosa.

Ofisa huyo pia anatuhumiwa kupinga juhudi za Serikali kuwapa chanjo wananchi kuepuka milipuko ya magonjwa. Kosa jingine Kadogosa amesema ni kukashfu viongozi wakuu wa nchi akiwemo Rais Samia Suluhu Hassan na Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson kupitia makundi ya kijamii.

“Kutokana na tuhuma zote kuthibitika, bodi ya wakurugenzi wa shirika kwa mamlaka iliyopewa chini ya kifungu cha 13(f) cha Sheria ya Reli namba 10 ya mwaka 2017 imeamua ufukuzwe kazi kuanzia Agosti 19, 2022.

Endapo hautaridhika na uamuzi huu, unayo haki ya kukata rufaa Tume ya Utumishi wa Umma ndani ya siku 45 kuanzia tarehe ya kupokea barua hii. Hii ni kwa mujibu wa kanuni ya 60 ya kanuni za utumishi wa umma za mwaka 2003,” inaeleza barua hiyo iliyosainiwa na Kadogosa.

Post a Comment

Previous Post Next Post