BUSWITA MDOGOMDOGO AITEKA YANGA

Unahitaji kitu gani cha ziada kutoka kwa Pius Buswita. Nyota huyo ni fundi wa mpira. Anavutia kumtazama kila anapokuwa uwanjani. Ni staa asiyedeka.

Kwenye kila mechi atakupa kile unachokitaka. Ana utulivu mkubwa pindi anapokuwa na mpira. Ana maamuzi sahihi pindi anapokuwa na mpira, hana papara hata kidogo.

Ni wachezaji wachache wa Tanzania wenye uwezo huo. Baada ya Obrey Chirwa, Buswita ndiye mchezaji anayeibeba zaidi Yanga msimu huu.

Anaitendea haki nafasi anayocheza. Maamuzi yake mara nyingi yamekuwa sahihi. Ni katili pia mbele ya lango, na ndiyo maana anafunga kila siku.

Ndani ya kikosi cha Yanga, mbali na Ibrahim Ajibu, mchezaji mwingine mwenye kipaji halisi ni Buswita. Anaupa mpira masharti na unayatii.

Hana mbwembwe nyingi kama Ajibu, lakini anafanya mambo ya msingi uwanjani. Hivi majuzi pale Mtwara alikuwa akifunga bao lake la tano katika mashindano yote tangu timu hiyo iliporejea kwenye mashindano ya Mapinduzi mapema mwaka huu.

Uzuri wa Buswita ni kwamba anamudu kucheza nafasi zote kuanzia kiungo mshambuliaji, winga na straika. Anaweza kuwapikia wenzake mabao na anajua pia kufunga.

Kwa Tanzania ya sasa ni nadra kumpata mchezaji aina ya Buswita. Ana kipaji na pia ni mpambanaji. Muda mwingi uwanjani kuna kitu anakitafuta. Huwa napenda kumuita staa asiyedeka. Anajituma kama hakuna kesho.

Wachezaji wengi wa kariba ya Buswita siyo wapambanaji. Wachezaji wengi wa aina yake si wapenzi wa mazoezi, lakini kwake ni tofauti.

Hii ndiyo sababu leo Buswita amekuwa staa mkubwa kuliko Ajibu. Ikitokea kocha anataka kuchagua kati ya Ajibu na Buswita, bila shaka atamchagua Buswita. Atakupa vitu vingi zaidi uwanjani.

Walichofanikiwa Yanga kwa sasa ni kumfanya Buswita acheze katika ubora wake. Wamempa uhuru wa kucheza anavyojisikia.

Unapokuwa na mchezaji mwenye kipaji halisi hupaswi kumpa masharti mengi uwanjani. Wachezaji wengine wanapaswa kufanya kazi kwaajili yake. Anachopaswa kufanya ni kuipa timu matokeo ya ushindi. Hii ndiyo kazi yake ya msingi.Unaanzaje kuwaambia Ajibu na Buswita wakabe sana? Hapana. Kazi hiyo unawapa Pato Ngonyani, Raphael Daudi na Papii Tshishimbi.

Kazi ya Ajibu na Buswita ni kuufanyia mpira maajabu tu. Yanga wamefanikiwa katika hili.

Buswita anafanya kile ambacho kilikuwa kikifanywa na staa wa zamani wa Simba, Haruna Moshi 'Boban'. Anaufanya mpira kuwa kitu rahisi. Anawafanya wenzake kutabasamu muda mwingi.

Habari mbaya kwa Simba ni kwamba wana mchezaji wa aina ya Buswita lakini wameshindwa kuupata ubora wao msimu huu.

Ni Mohammed Ibrahim. Staa huyo ana kipaji kama kile cha Buswita. Ni fundi wa mpira kweli kweli. Ni hatari kila anapokuwa na mpira. Anamudu pia kucheza nafasi zote za ushambuliaji.

Msimu uliopita angalau waliupata ubora wake. Ibrahim alibadilisha mchezo kila alipoingia uwanjani. Macho ya wengi yalitamani kumtazama.

Mara nyingi Ibrahim asipofunga basi atatoa pasi ya bao. Asipotoa pasi ya bao atatengeneza nafasi ambayo inaweza kuzaa bao, hawezi kutoka uwanjani bila kufanya kitu chochote cha maana.

Bahati mbaya msimu huu ameshuka kidogo. Amekuwa mvivu wa mazoezi. Upambanaji wake umeshuka, tofauti na Buswita.

Tatizo kubwa la wachezaji aina ya Buswita, MO Ibrahim na Ajibu wana tabia ya kudeka. Si watu wanaopenda kufokewa sana. Si watu wanaopenda kupangiwa maisha sana.

Wachezaji wengi wa kariba hiyo wanafahamu wazi kuwa wanajua mpira, hivyo wanapenda kudekezwa. Siyo wachezaji wanaopenda sana kukaa benchi. Si wachezaji wanaopenda sana kufanyiwa mabadiliko.

Hiki ndicho ambacho kinamsumbua MO Ibrahim kwa sasa. Anaona kama wachezaji wengi wanaocheza hawana uwezo mkubwa kama wa kwake, wanabebwa tu. Anaona kama benchi la ufundi linamwonea.

Hilo pia lilikuwa likimsumbua Ajibu alipokuwa Simba. Alipowekwa benchi, hakupenda hata kidogo. Siku zote aliamini yeye ana kipaji kikubwa kuliko wachezaji wengine wa Simba. Na ndiyo ukweli wenyewe.

Pamoja na yote, Buswita kama ataendelea na upambanaji wake anaweza kuwaacha MO Ibrahim na Ajibu wakicheza hapa hapa. Hakuna kocha ambaye ataacha kuvutiwa kumsajili. Miguu yake ina ushawishi mkubwa.

Post a Comment

Previous Post Next Post