
UJANJA kupata. Hiyo ndio kauli pekee unayoweza kuitaja unapowazungumzia baadhi ya mastaa wa soka wanaokipiga Ligi Kuu Bara ambao ukizubaa tu kwenye kuwakaba, imekula kwako.
Mastaa hao ambao wengi wao ni mastraika, wana uwezo mkubwa wa kumiliki mpira na kupiga chenga, hivyo ukiwakaba kizembe kama hujasababisha penalti basi ni faulo.
Mastaa hao pia wamekuwa wajanja wa kutengeza faulo zinazowagharimu wapinzani wao kutokana na aina ya uchezaji wao wa kutumia akili ya ziada pindi timu zinapokuwa zina wakati mgumu wa kupata matokeo.
Unawafahamu mastaa hawa? Mwanaspoti linakuletea orodha ya nyota hao ambao kuwakaba inahitaji akili ya ziada, vinginevyo itakugharimu.
Hassan Kessy-Yanga
Ni kati ya wachezaji wanaojua kutengeza faulo ili timu yake ifanikiwe. Uchezaji wa Kessy ni ule anaowavuta wapinzani mpaka eneo lao la hatari na kuwafanya wacheze rafu pasipo kutarajia.
Mara kibao Yanga imenufaika na faulo za Kessy, ikiwamo penalti aliyotengeza wakati walipocheza mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya St. Louis wikiendi iliyopita. Kama si Obrey Chirwa kuipoteza, Yanga ingenufaika nayo. Katika mchezo huo Yanga iliibuka na ushindi wa bao 1-0.
Kama utakumbuka vizuri mchezaji wa St. Louis, Tahiry Andriamandimby, alijikuta akimchezea rafu Kessy mapema kipindi cha kwanza baada ya kupinduliwa kama samaki na kuachwa kwenye mataa.
Ibrahim Ajib-Yanga
Aina ya uchezaji wa Ajibu ni ile ya kutumia akili. Anajua kuvuta mipira kutoka katikati huku akikimbia kwa kasi kwenda eneo lao la hatari la wapinzani. Kwa iel kasi yake mabeki hujikuta wakimsindikiza na maji yapowafika shingoni hulazimika kumchezea rafu.
Achilia mbali hilo, Ajibu pia ni mchezaji anayejua kuzicheza faulo, unayakumbuka yale mabao yake ya faulo dhidi ya Njombe Mji na Stand Unite? Ule ndio ubora wake bwana.
Enock Atta-Azam
Kutokana na aina ya uchezaji wake, ni rahisi mabeki kujikuta wakimfanyia makosa na kutengeza faulo ambazo zinakuwa na manufaa ‘Watoto hao wa Bakhresa’.
Usumbufu wa Atta husababisha mabeki kupandwa hasira na kutoka mchezoni kwani humchezea faulo ambazo pia huwagharimu kadi.
Kwenye mechi yao dhidi ya Simba, kama si busara za mwamuzi, basi huenda angeipatia timu yake penalti ya dakika za lala salama baada ya Yusuf Mlipili kumkwatua kwa miguu miwili.
Shiza Kichuya-Simba
Anatumia miguu yote na ana kasi ya kukimbia na mipira jambo linalowafanya mabeki kujikuta wakimchezea rafu na kutengeza faulo.
Licha ya ufupi wake pamoja na umbo dogo, wapinzani wamejikuta wakiambulia maumivu kwa namna ambavyo anatumia akili ya kuwaingiza mkenge wa faulo.
Kichuya ambaye anautumia vizuri zaidi mguu wake wa kushoto, amekuwa hatari kwenye kupiga penalti pia akiwa hajawahi kukosa hata mara moja katika penalti sita alizopiga Msimbazi.
Emmanuel Okwi-Simba
Staa huyu wa Simba anatumia akili nyingi katika kufunga mabao yake, jambo linalowapelekea wapinzani kujikuta wakimchezea rafu ambazo zinazaa faulo na kujikuta wakipata adhabu ya kadi.
Okwi si mchezaji wa kutumia mabavu, bali anaangalia ni namna gani anaweza akamwingiza mkenge beki ili akwatuliwe ndani ya 18. Moja ya faulo muhimu alizotengeneza ni ile iliyozaa bao la nne dhidi ya Gendarmerie ya Djibouti wikiendi iliyopita katika mechi ya Kombe la Shirikisho barani Afrika.
Peter Mapunda-Majimaji
Winga wa Majimaji, Peter Mapunda, naye yumo bwana. Ni mzuri katika kuitafutia timu yake mipira ya adhabu kutokana na kuangushwa mara kwa mara. Mapunda ana uwezo mkubwa wa kumiliki mpira, kupiga chenga na kufunga.
Kutokana na tabia yake ya kupenda kukokota mipira, mara nyingi amekuwa akikwatuliwa na kuizawadia timu yake faulo kadhaa. Kwenye mechi yao dhidi ya Yanga juzi Jumatano, alikwatuliwa mara kadhaa na kuizawadia timu yake faulo za kutosha, ni basi tu hawakuweza kuzitumia vyema.
Tags:
michezo