HUU HAPA UKWELI KUHUSU LWANDAMINA KUACHANA NA YANGA NA KWENDA KLABU YA ZESCO

Wakati Yanga ikishuka Uwanja wa Nagwanda Sijaona kuivaa Ndanda leo, wingu zito limetanda juu ya hatma ya kocha George Lwandamina anayehusishwa kutakiwa haraka na mabingwa wa Zambia, Zesco United.

Lwandamina mkataba wake na Yanga utamalizika mwisho wa msimu huu, lakini tayari amehusishwa kutakiwa na Zesco mapema zaidi.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya Zesco, zilizoripotiwa na magazeti ya Zambia mwishoni mwa wiki hii zimedai kuwa Lwandamina anarudi nchini humo baada ya kukaa na Yanga kwa misimu mwili.

“Lwandamina anarudi Zesco, anakuja na msaidizi wake kutoka Yanga, Noel Mwandila. Uongozi wa kampuni (Zesco Limited) ndiyo hasa wanaotaka mkurudisha hapa baada ya aliyekuwa kocha wao Zlatko Krmpotic, kuingia mitini,” kilidai chanzo hicho.

Akizungumza na Mwananchi, Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Mkwasa alisema, uamuzi wa Lwandamina kuachana na Yanga ni masuala binafsi ya kocha huyo raia wa Zambia.

“Mkataba wake unakwisha mwishoni mwa msimu, lakini kama ataamua kuondoka, hayo ni masuala yake binafsi,” alisisitiza Mkwasa.

Naye Lwandamina alipoulizwa alisema yeye ni kocha wa Yanga na habari za kuondoka kwake zitakuwa rasmi kama uongozi wa Yanga utaeleza na siyo kuzipata mahali pengine.

“Kama nitaondoka atasema Mkwasa kwa kuwa ndiye ‘bosi’ wangu, mimi siwezi kuzungumza lolote, isitoshe taarifa hizo sio ‘official’ na sijui ulikozipata, lakini mimi bado niko Yanga,” alisema Lwandamina.

Mkwasa amesisitiza kuwa kocha Lwandamina hajawambia kama ataondoka, lakini akafafanua kuwa hayo ni masuala binafsi ya kocha.

Hata hivyo, kocha Lwandamina ameonekana hana furaha ndani ya Yanga tangu kuanza kwa msimu huu, mara kadhaa amekuwa akirudi kwao Zambia kutokana na matatizo mbalimbali ya kifamilia na kutotekelezwa kwa matakwa yake.

Mapema Septemba, mwaka jana Lwandamina aliomba uongozi wa Yanga kumtafutia mtaalamu wa matibabu ya viungo atakayesaidiana na daktari wa timu hiyo Dk. Edward Bavu ili kupambana na hali ya majeruhi katika timu yake.

Lwandamina alikariwa akisema: “Ni kweli nimewaomba wanitafutie huyo mtu, sawa tuna daktari wa timu, lakini tunatakiwa kufikiria mbali zaidi kumaliza hali kama hii ya kuwa na wachezaji wengi muhimu majeruhi kama hivi na hili linaweza kuwa tatizo zaidi unapokuwa katika mashindano makubwa ya Afrika ambayo hayana muda wa kupoteza kila mchezo ni muhimu.”

Mbali na hilo, Lwandamina alishindwa kufanya kazi kwa muda kutokana na kukosa kibali na tangu wakati huo majukumu makubwa amekuwa akimwachia msaidizi wake Shedrack Nsajigwa.

Nchini Zambia, Kocha wa sasa wa Zesco, Tenant Chembo alikaririwa akisema taarifa za kurejea kwa Lwandamina kuinoa Zesco zimemuathiri.

“Najua kauli mbiu ya Zesco ni weledi na uhusiano wa kazi, lakini mimi ni binadamu, siwezi kuficha presha niliyonayo kuhusu ujio wa kocha mwingine,” alikaririwa Chembo.

Katibu mkuu wa Zesco, Richard Mulenga alikataa kuthibitisha kurejea kwa Lwandamina kukinoa kikosi hicho ambacho alikiacha mwaka 2016 na kujiunga na mabingwa hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

“George bado ana mkataba na Yanga hivyo itakuwa si haki kuanza kumzungumzia kwamba atakuja Zesco. Tuache kuzungumzia kuhusu George, ambaye ana mkataba na Yanga,” alisema Mulenga.

Yanga kuvunja mwiko Mtwara

Yanga ina kazi ya kuhakikisha inavunja mwiko kwa kupata ushindi wa kwanza kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara.

Tangu mwaka 2014, Ndanda ilipopanda Ligi Kuu Bara, Yanga haijawahi kupata ushindi katika uwanja huo zaidi ya kuambulia sare.

Mabingwa hao watetezi wanapewa nafasi kubwa ya kushinda mchezo huo kutokana na ubora wa kikosi chao kuliko Ndanda ambayo imekuwa ikisuasua kwenye ligi msimu huu.

Kocha wa Yanga, Lwandamina alisema amekiandaa vizuri kikosi chake ili kupata matokeo mazuri na kujitengenezea nafasi nzuri kwenye msimamo wa ligi.

Naye kocha wa Ndanda, Malale Hamsini alisema wako kamili kuivaa Yanga na wanahitaji pointi tatu ili kuwaondoa nafasi mbaya waliyopo kwenye msimamo wa ligi. Yanga ipo nafasi ya pili kwa pointi 37 Ndanda ina pointi 18 ikiwa nafasi ya 13 kwenye msimamo wa Ligi Kuu.

Post a Comment

Previous Post Next Post