MASHABIKI WA SOKA TANZANIA HAYA YANAWAHUSU


HAKUNA mtu mwenye lawama duniani kama shabiki wa mpira. Ndiye mtu anayejua kila kitu kwenye mpira. Yaani yeye ndiye mjuaji kuliko kocha, mchezaji au mtaalamu yeyote. Tunajijua wenyewe.

Hata kabla mpira haujaanza ameshaucheza na ana matokeo yake mfukoni. Hiyo inatokea kwenye Ligi zetu za Bongo mpaka Ulaya. Lakini kwa hapa Tanzania bado kuna udhaifu mkubwa ambao hauendani na hali au neema tuliyonayo kwenye mpira wetu.

Mashabiki wa Tanzania hawajui kushangilia. Hawajui kusapoti timu zao zinapokuwa uwanjani iwe kwenye Simba na Yanga, Namungo, Mwadui mpaka hata katika timu za Taifa.

Hapa kwetu shabiki anakuwa rafiki wa mchezaji kwenye furaha tu. Sehemu kama Rwanda, Uganda au hata Ulaya tuchukulie mfano Liverpool, Newcastle United, Real Madrid muda wote mashabiki wanapokuwa eneo la uwanja wanakuwa kama machizi, wanashangilia tangu basi la wachezaji linaingia, wanapasha wanacheza.

Wana nyimbo zao mbalimbali na namna nzuri za kushangilia na kuchangamsha uwanja na kupandisha mzuka wa wachezaji wao. Timu iwe imepoteza, inashambuliwa au inaongoza muda wote wako nyuma ya wachezaji wao wakishangilia hata kuzomea wapinzani. Ili mradi tu wachezaji wachangamke na wasijisikie wapweke.

Lakini kwa Tanzania pamoja na mzuka wa soka tulionao, hili halipo. Mashabiki hawajui kuwasapoti wachezaji wao ndani ya uwanja. Mashabiki wanashangilia matukio tu, muda mwingine wanakuwa wametulia tu kama kwamba hakuna kinachoendelea.

Nadhani kuna haja ya mashabiki kubadilika kuanzia sasa na kujifunza kutoka kwa wenzetu namna nzuri ya kuwapa sapoti wachezaji haswa wakati huu ambao ligi zinakwenda kuanza.

Ni wajibu wa shabiki kuwa mchezaji wa 12, ili kunogesha mchezo na kupata kile anachokitaka kutoka kwa mchezaji kuliko kuishia kulaumu tu. Naamini kwamba kama mashabiki elfu 60 wakiamsha mzuka kuishangilia Simba, Azam au Biashara kwenye michuano ya kimataifa hakuna mgeni ambaye atatamani kukanyaga kwenye Uwanja wa Mkapa au hata Uhuru.

Lakini tabia za mashabiki wakati mwingine zimekuwa zikiwapa nafasi timu pinzani bila sababu za msingi. Mashabiki waangalie namna nzuri kuanzia sasa ya kubadilika na kusapoti vitu vyao. Hii itaongeza zaidi morali kwa wachezaji husika na wao kujisikia wana deni zaidi ya kuwa wanalaumiwa kila mara pale wanapoharibu tu.

Lakini vilevile huu ndio wakati wa kusapoti klabu zao kiuchumi kwa kununua jezi, vifaa mbalimbali na kwenda kwa wingi viwanjani ili kukuza uchumi wa klabu na kuzisaidia kujiendeleza kiuchumi kwa vile hali halisi ya timu zetu za Tanzania inafahamika.

Kila mmoja ajitathmini upya, mashabiki wana nafasi kubwa kwenye kuchangamsha mchezo kuliko kuishia zaidi kwenye kulaumu. Mashabiki wa Tanzania tubadilike na kujifunza si tu kuuelewa mchezo lakini tusapoti wachezaji wetu kwenye shida na raha. Hayo mambo mengine tuachie makocha na viongozi. Tujiongeze.

Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 753 336 000 au +255 625 917 902

Masengwa blog Ipo Play Store…Download HAPA ,Uwe unapata habari zote kwa urahisi zaidi
 Bofya Hapa

No comments:

Powered by Blogger.