MAFURIKO YASOMBA NYUMBA 2,701 KILOSA


IDADI ya watu walioathiriwa na mafuriko ya mvua katika kata 11 za vijiji 16 wilayani Kilosa, Morogoro, imeongezeka kutoka kaya 1,831 zilizokuwa na watu 7,261 na kufikia kaya 2,701 zenye watu 9,345.

Aidha, mafuriko hayo yamesababisha uharibifu wa miundombinu mbalimbali zikiwemo barabara na madaraja. Mafuriko hayo yamesababisha pia kubomoka kwa nyumba 377 za makazi ya watu katika maeneo ya vijiji hivyo na nyingine 2,266 kuzingirwa na maji hayo.

Katika taarifa ya Kamati ya Maafa ya Wilaya ya Kilosa iliyosomwa juzi na Katibu wa Kamati hiyo, Simfrosa Mollel kwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Kebwe Stephen Kebwe, Mollel alisema takwimu hizo ni za kuanzia tangu kutokea kwa athari za mafuriko hayo Januari 8 hadi 12, mwaka huu.

Mafuriko hayo yalisababishwa na mvua zilizonyesha katika baadhi ya maeneo ya Kilosa na mikoa ya jirani, ikiwamo Dodoma na Manyara na kusababisha maji kujaa Mto Mkondoa, kubomoa sehemu ya kingo ya tuta na kuingia katika makazi ya watu na mashamba.

Alizitaja kata hizo zenye vijiji 16 kuwa ni pamoja na Mkwatani, Chanzuri, Berega, Kidete, Magomeni, Masanze, Mbumi, Tindiga, Mbigiri na Mabwerebwere. Mjumbe wa Kamati hiyo, Meja Yenu Mgugule alimfahamisha Dk Kebwe kuwa, licha ya athari hizo, pia nyumba 63 zimeezuliwa mapaa kutokana na upepo mkali uliotokea katika vitongoji vya Vikwalaza na Tambuka Reli vilivyopo Kata ya Mikumi.

Alisema nyumba 53 ziliezuliwa na upepo mkali katika Kitongoji cha Vikwalaza na nyingine10 katika Kitongoji cha Tambuka Reli na kwamba, hakuna maafa zaidi yaliyoripotiwa kutokana na nyumba hizo kuezuliwa.

Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Dk Halima Mangiri alisema hawajapata taarifa yoyote kuhusu kutokea kwa magonjwa ya mlipuko licha ya visima zaidi ya 13 vya maji ya kunywa kuathiriwa na vingine kubomoka.

Dk Mangiri alisema hatua zilizochukuliwa ni pamoja na usambazaji wa pakiti za dawa ya kutibu maji aina ya “waterguard” zipatazo 15,810 zilizogawiwa katika kata zilizokumbwa na athari hizo ili kutibu maji na kujikinga na magonjwa.

IMEANDIKWA NA JOHN NDITI,HABARILEO KILOSA

Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 753 336 000 au +255 625 917 902

Masengwa blog Ipo Play Store…Download HAPA ,Uwe unapata habari zote kwa urahisi zaidi
 Bofya Hapa

No comments:

Powered by Blogger.