KAULI YA KINGUNGE YAWAIBUA WAPINZANI
Viongozi wa vyama vya upinzani wamesema kauli ya mwanasiasa mkongwe nchini, Kingunge Ngombale Mwiru kwamba CCM ni chama chake, ni maoni yake binafsi na hayaondoi ukweli kuwa ameshiriki kukijenga chama hicho tawala.
Akizungumza na Rais John Magufuli aliyemtembelea hospitalini juzi, Kingunge alisema: “CCM ni chama changu, nimetoka tu, nimeachana. Lakini nimefanya kazi zote. Nimejipinda mimi kwelikweli. Kwa hiyo hakiwezi kuwa kinyume changu hata kidogo.”
Kauli hiyo ilitafsiriwa na Rais Magufuli kuwa Kingunge bado ni CCM moyoni, lakini wapinzani waliohojiwa na Mwananchi wana maoni yao.
“Hiyo huwa haibadiliki. Ukiasisi chama na ukiachana nacho, utaendelea kuwa muasisi wake,” alisema mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya CUF, Julius Mtatiro ambaye pia sema kauli ya mwanasiasa huyo mkongwe pia ililenga kumkumbusha Rais kwamba pamoja na yote yaliyotokea, Kingunge ataendelea kuwa muasisi wa CCM.
“Nadhani hicho ndicho alichokilenga Kingunge. Ni kama alikuwa anamkumbusha Rais,” alisema Mtatiro.
Kingunge aliyetengaza kuhama CCM Oktoba 4, 2015 alitoa kauli hiyo juzi akiwa kitandani Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ambako anatibiwa majeraha ya kung’atwa na mbwa takribani siku sita zilizopita.
Katika maelezo yake, Mtatiro alisema Kingunge ana haki ya kutoa maoni na kwamba huo ndio ukweli.
“Tangu kuanzishwa kwa TANU wao ndiyo waliokipigania na kuunda CCM na ndiyo wazee ambao wamekifikisha kile chama kilipo leo. Waliopo sasa wamekikuta na kuendeleza walipoishia wao,” alisema Mtatiro.
“Kauli yake inamaanisha kuwa hata akipata matatizo, wana-CCM hawataweza kumkimbia pamoja na kwamba alijitoa.”
Alisema japokuwa mwanasiasa huyo hakuwahi kusema amejiunga na chama gani, aliondoka CCM vizuri na aliweka wazi sababu za kukikimbia chama hicho.
Naye katibu mkuu wa NLD, Tozi Matwange alisema kauli ya Kingunge haumaanishi kuwa anaweza kurejea.
Alisema kauli ya mwanasiasa huyo inaonyesha dhahiri kwamba CCM ni chama chake kwani alishiriki kukiasisi, kukisimamia.
“Ametoka huko na hatabadilika,” alisema.
Katibu mkuu wa NCCR– Mageuzi, Danda Juju alisema Kingunge amefanya kazi kubwa akiwa ndani ya CCM katika kipindi chote cha maisha yake, hivyo kauli hiyo anatafsiri kuwa kumbukumbu zake bado zipo katika chama hicho japokuwa amekiacha.
Wakati huohuo, mtoto wa mwanasiasa huyo, Kinje Mwiru ameliambia gazeti la Mwananchi kuwa juzi mchana walimpa taarifa Kingunge kuhusu kifo cha mkewe, Pares na jana akaridhia azikwe Alhamisi.
Pares alifariki dunia Januari 4 saa 8:00 mchana akiwa wodi ya Sewahaji alikokuwa amelazwa, tangu Oktoba 3 mwaka jana.
“Mzee ametupa mwongozo wa nini cha kufanya. Mazishi yatafanyika Alhamisi katika makaburi ya Kinondoni,” alisema.
“Mpaka sasa ratiba bado haijapangwa na leo jioni (jana) familia itakutana na kutakuwa na kikao pale nyumbani,” alisema.
Na Herieth Makwetta, Mwananchi
Masengwa blog Ipo Play Store…Download HAPA ,Uwe unapata habari zote kwa urahisi zaidi
No comments: