JE, LEO YANGA WATATOBOA?
HIVI umeshautazama msimamo wa Ligi Kuu Bara? Yanga na pointi zake 21 imeachwa nyuma kwa pointi tano na vinara wa ligi hiyo. Vinara wenyewe ni Simba. Unaona mambo yalivyo matamu. Lakini, Yanga wanaamini, mechi tano zijazo wanatoboa. Ndivyo wanavyoamini.
Unajua kwanini? Yanga wametazama ratiba yao, kisha wakatazama ile ya mahasimu wao hao wa Msimbazi, wakacheka sana na kusema hilo pengo la pointi tano wanalikata fasta tu, kabla hata hawajaenda kwenye mechi zao za kimataifa mapema Februari. Kwenye mechi hizo, Yanga wameihesabia Simba mechi tatu ngumu kabisa, hivyo wanaamini hawawezi kumaliza mechi hizo bila ya kuangusha pointi hapo. Ratiba inasomeka kwamba Simba kwenye mechi hizo tano, itacheza nyumbani mechi nne na moja tu itakuwa ugenini.
Kwanza Simba itacheza na Singida United, halafu Kagera Sugar huko Kaitaba, kisha Majimaji, Ruvu Shooting na kumalizia na Azam FC. Simba huwa haina rekodi nzuri sana inapocheza na Kagera na hilo ndilo linalowafanya Yanga kuwa na jeuri zaidi wakiamini watatumia nafasi hiyo kupunguza pengo hilo la pointi. Lakini, Simba hao hao watakabiliana na timu nyingine mbili zilizopo ndani ya Tatu Bora, Singida na Azam FC. Huo ndiyo mtihani unaowakabili. Kwenye karatasi hizi si mechi rahisi kabisa kwa wababe hao wa Msimbazi, hivyo kuzoa pointi zote kwenye mechi hizo si kitu rahisi. Hata hivyo, Simba yenye mastaa walio kwenye viwango bora kabisa kwa sasa wakiwamo Emmanuel Okwi, John Bocco na Shiza Kichuya, itabaki kuwa ni timu ngumu kushindika.
Yanga wao kwenye mechi zao tano zijazo, watakuwa na mechi tatu za ugenini na mbili watacheza nyumbani. Lakini, ugenini watakuwa na mechi dhidi ya Ruvu
Shooting, Lipuli na Azam FC. Wanachokiamini ni kwamba mechi ngumu kwao ni ile dhidi ya Azam tu ambao kimsingi ni wapinzani kwenye mbio za ubingwa wa ligi hiyo msimu huu. Yanga pia itacheza na Mwadui na Njombe Mji ndani ya Jiji la Dar es Salaam, eneo ambalo wanaamini hizo ni pointi ambazo wanazivuna bila ya mashaka. Ligi Kuu Bara msimu huu imekuwa na ushindi mkali kweli kweli kutokana na kuwapo kwa pointi tano tu zinazoitofautisha timu inayoongoza hadi inayoshika nafasi ya tano, Mtibwa Sugar.
Simba na Azam zimekamatana kwa pointi, kila moja inazo 26 katika mechi 12 na wanatofautiana na mabao tu, Simba ikiwa imeweka kwenye nyavu za wapinzani mara 25 na wao kufungwa sita tu, huku Azam wao wakifunga 12 na kufungwa matatu. Singida wako kwenye nafasi ya tatu na pointi zao 23 walizovuna kwenye michezo 12, huku wakiwa wamefunga mabao 12 na kufungwa sita, ndipo wanapofuatia mabingwa watetezi Yanga na pointi zao 21 walizovuna kwenye mechi 12, wamefunga mabao 17 na kufungwa saba. Mtibwa pia wamekusanya pointi 21. Simba na Azam FC ndizo timu pekee ambacho hazipoteza mechi kwenye ligi hiyo kufikia sasa.
Azam wao mechi zao tano zijazo watacheza na Majimaji, kisha Prisons, zote zikiwa ugenini kabla ya kurudi nyumbani huko Chamazi Complex kukipiga na Yanga na Ndanda FC kisha watoka tena kwenda kucheza na Simba.
WAKONGWE WAKAZIA
Katika hatua nyingine mastaa wa zamani wa Yanga wamekiri kuumizwa na kipigo cha mabao 2-0 kutoka Mbao, lakini wakawatia moyo vijana wao kuwa wakaze tu, kwani bado wana nafasi kubwa ya kutetea ubingwa msimu huu.
Sekilojo Chambua, Henry Morris na Abeid Mziba ‘Tekelo’ kwa nyakati tofauti walisema Yanga haina haja ya kupaniki na badala yake waelekeze nguvu zao katika Kombe la Mapinduzi na wakirudi wawe wameiva kuweza kufanya kweli katika ligi.
Chambua alisema kwa uzoefu alionao katika ligi, anajua namna wachezaji na mashabiki wanavyoumia kwa kulinganisha matokeo yao na watani zao Simba, lakini bado hawapaswi kukata tamaa.
“Benchi la Ufundi lisahaulishe wachezaji kipigo cha Mbao na kuelekeza nguvu katika mashindano yaliyopo mbele yao ikiwamo Mapinduzi na Ligi ya Mabingwa Afrika na hata mechi zao zilizosalia za Ligi Kuu,” alisema.
Naye Mziba alisema ligi bado ndefu, hivyo haoni sababu ya wachezaji kuumia na kuona wameishashindwa vita.
“Wachezaji wanapaswa kutambua kwamba wapo vitani, matokeo hayo yawatie moyo kwa kujipanga zaidi badala ya kunyosheana vidole,” alisema Mziba.
Kwa upande wa Morris alisema safu ya ulinzi ya Yanga haikuwa na mawasiliano hivyo kuruhusu mabao, lakini bado Yanga ina kikosi kizuri na kama itajipanga kwa mechi zijazo itatetea taji lake kwa mara ya nne mfululizo.
Kiungo wa zamani wa Simba na Yanga, Ally Yusuf ‘Tigana’ alisema tatizo la klabu kongwe ni kutopenda kufungwa, lakini ukweli soka ndivyo lilivyo na Yanga ijipange tu bila kujali kama wameachwa pointi tano na Simba.
Yanga ilikumbana na kipigo hicho cha tatu mfululizo katika mechi zake dhidi ya Mbao za kwenye Uwanja wa CCM Kirumba. Msimu uliopit a ilifunga mara mbili kwa bao 1-0 katika nusu fainali ya Kombe la FA na mechi ya mwisho ya ligi.
Masengwa blog Ipo Play Store…Download HAPA ,Uwe unapata habari zote kwa urahisi zaidi
No comments: