YANGA YAWEKA FUNGU LA MAANA ILI WAFANYE VIZURI KWENYE MICHUANO IJAYO
INAWEZEKANA ni kweli Yanga ina hali mbaya kiuchumi, lakini hilo halijawafanya mabosi wa klabu hiyo kujiweka sawa kwa michuano ya kimataifa wakiwa na kiu ya kuona wanafika mbali ili wavune fedha za kutosha CAF.
Wakitambua kuwa mapema mwakani wataanza kibarua cha ushiriki wa Ligi ya Mabingwa Afrika, vigogo wa Yanga wamesema wamezichanga na kutenga bajeti ya maana ili kuweza kumudu ushiriki wao wa mechi za kimataifa.
Kaimu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga alisema wameandaa bajeti ya maana isiyopungua Sh300 milioni ili kuhakikisha Yanga inavuka kwenye makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Sanga ambaye kitaaluma ni Mhandisi alisema katika michuano hiyo wametenga fedha hizo wakiamini zitawasaidia kuwarahisishia kazi na kufanya vyema katika Ligi ya Mabingwa ambayo msimu uliopita walitolewa raundi ya kwanza na Zanaco FC ya Zambia kwa faida ya bao la ugenini.
Bosi huyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi alisema endapo kiasi hicho kitafanikiwa kupatikana, huku wachezaji wao wakiwa vizuri kiafya kila kitu kinawezekana kwao kuweza kupambana na kikosi chochote.
Alifichua kuwa kwa sasa wamefanikiwa kupiga hatua kubwa ya kumaliza sehemu kubwa ya malipo stahiki ya wachezaji wao ambapo bado wataendelea kumaliza kila kitu taratibu huku akikiri wazi kuwa, pengo la Manji katika kuendesha kikosi chao ni kubwa lakini wataendelea kupambana.
“Kama unavyoona tunaendelea kupambana tunatambua kwamba kuna hayo mashindano makubwa ya Afrika yanakuja, mimi sio mtu wa kukata tamaa lakini nakuhakikishia kikosi chetu kitaingia na akili ya kushindana.
“Kama kiongozi kwa uzoefu wangu katika mashindano haya bajeti ya kiasi hicho cha fedha kitatusaidia kupambana na tunaamini tukitinga makundi tutapunguza makali kwa kuvuna fedha nyingi za Caf,” alisema Sanga.
Yanga imepangwa kuanza kibarua cha CAF kwa kuvaana na St Louis ya Shelisheli na kama itavuka hapo itakutana na El Merreikh ya Sudan ama Township Rollers ya Botswana kabla ya kuingia makundi.
Yanga ilikuwa klabu ya kwanza nchini kucherza makundi ya Ligi ya Mabingwa mwaka 1998 na kurejea tena kuwa ya kwanza kwa klabu za Tanzania kuingia makundi ya Kombe la Shirikisho mwaka jana tu, japo mara zote ilifanya vibaya. Kwa sasa inajiandaa na mchezo wao wa Ligi Kuu dhidi ya Mbao FC.
MWANANCHI
Masengwa blog Ipo Play Store…Download HAPA ,Uwe unapata habari zote kwa urahisi zaidi
No comments: